Mwenyekiti
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Mjini Magharibi, Borafya
Silima.
---
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar
kimeitaka serikali ya Mapinduzi kuifuta mara moja Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara
ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) kwa kuwa inafanya kazi kinyume na malengo yake
usajili.
Kauli hiyo imetolewa jana katika mkutano wa
hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mabata huko Magomeni Mjini Unguja na
kuhudhuriwa na wanachama wa CCM na wafuasi wa CUF ambapo mgeni rasmi wa mkutano
huo alikuwa ni Mwenyekiti wa Mkoa wa Mjini Magharibi Borafya
Silima.
Akizungumza katika mkutano huo Katibu wa
Vijana wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mohammed Ali Khalifa alisema chama cha CCM
kinamuomba msajili wa taasisi za kiraia achukue uamuzi wa kuifuta jumuiya hiyo
ya Uamsho ili isiwepo kabisa katika kumbukumbu za asasi za kiraia hapa
Zanzibar.
Alisema
taasisi hiyo haiendeshi shughuli zake za kidini licha ya kuwa imesajiliwa kwa
misingi ya kuendesha mambo ya dini lakini imepoteza muelekeo na imekuwa ikifanya
kazi za kisiasa jambo ambalo linakwenda kinyume na malengo ya jumuiya
hiyo.Aidha alisema Uamsho ina mkono wa watu wakubwa ndani ya serikali na
ndio muda wote imekuwa ukinyamaziwa na hivyo kuitaka serikali kuwa macho na
watendaji wake na kuwachukulia hatua wale wote ambao wamehusika katika kuwaunga
mkono na kuwakamta kwa kuwafikisha katika vyombo vya
sheria.
Kwa upande wake Mgeni rasmi wa mkutano huo,
Borafya Silima alisema jeshi la polisi limefanya kazi nzuri sana ya kuhakikisha
linawakamata wahalifu wote na kuwafikisha katika vyombo vya sheria na kuwataka
waendelee na kazi hiyo.
Borafya alisema haiwezekani viongozi wa
dini ambao hawana elimu kuachiwa kutamba na kuiharibu nchi kwa kisingizio cha
kutangaza dini wakati wanachokitangaza ni siasa huku akikishutumu chama cha
wananchi CUF kuwa kinahusika moja kwa moja na vurugu zilizotokea kwa kuwabariki
viongozi hao wa Uamsho.
“Mtu hana dini yenyewe haijui leo hii
tumwite sheikh kwani kuvaa kanzu ndio sheikh? Alihoji huku akishangiriwa na
wafuasi wa chama hicho.
Mwenyekiti huyo ambaye amechaguliwa hivi
karibuni amesema kwamba nafasi aliyopata ni muhimu katika siasa za Zanzibar na
kwamba ataitumia vizuri na kuwataka wapinzani wake wajipange vizuri ili
kukabiliana nao kwani wameingizwa madarakani kwa
maridhiano.
Borafya alisema Maalim Seif amekuwa amepewa
wizara zisizo na uzito wowote serikali na hivyo amekuwa akimuonea choyo makamo
wa pili wa rais, Balozi Seif Ali Idd kwa kuwa yeye ndio mshughulikiaji wa wizara
zote za serikali.
Mazungumzaji katika mkutano huo ambao kwa
kiasi kikubwa wote waliohutubia walimlenga na kumshutumu moja kwa moja Makamo wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na kumtaka aachie ngazi kwa
kuwa ameshindwa kutekeleza yale ambao aliapa kuyasimamia wakati akiingia
madarakani.
Mbali na matusi ya nguoni na kumshutumu
kwamba anahusika na kundi la Uamsho walisema Maalim Seif hafai kuwa kiongozi
kutokana na kuwa mbinafsi kwa kuwa ameisema serikali yake mbele ya viongozi wa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) kwa kuwaeleza kwamba jeshi la
polisi na vikosi vya SMZ vinahitaji mafunzo ya kukabiliana na vurugu ili waweze
kupata mafunzo ya kukabiliana na vurugu hizo bila ya kuvunja haki za
binaadamu.
“Huyu Maalim Seif anawaambia UNDP kwamba
jeshi letu la polisi linahitaji mafunzo ya kuwakamata wahalifu sisi tunamwambia
polisi wetu na vikosi vyetu havihitaji mafunzo wewe ndio unahitaji mafunzo kwa
sababu kwani wewe unalindwa na nani? Si hawa hawa polisi” alisema
Khalifa.
Katika hatua nyengine viongozi hao wa CCM
walimtaka Maalim Seif kuachia ngazi kwa kwa kumsema rais wake Dk Shein hadharani
kitendo ambacho walisema ni kwenda kinyume na kiapo chake cha kuheshimu, kulinda
na kutotoa siri za serikali.
Hivi karibuni katika mkutano wake Maalim
Seif alimtaka Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein kutekeleza ahadi yake ya
kuwalinda wananchi wote bila ya ubaguzi na kuhakikisha vyombo vya ulinzi
vinasitisha ukiukwaji wa haki za binaadamu kwa kuwa wananchi wamechoshwa na
ukandamizaji wanaofanyiwa katika nchi yao.
Post a Comment