Waziri Mkuu wa Kenya Raila
Odinga
ANAYEDHANI kwamba kiongozi wa nchi tajiri na yenye nguvu kuliko zote duniani, Rais Barrack Obama wa Marekani, ndiye analipwa mshahara mkubwa kuliko viongozi wengine duniani, anajidanganya.
Lakini na yule anayedhani Kenya iko nyuma katika kuwalipa mishahara viongozi wao wakuu, bora aangalie upya dhana hiyo.
Mwanasiasa machachari wa mageuzi nchini Kenya, Raila Odinga ambaye kwa sasa ni waziri mkuu, anatajwa kama kiongozi anayelipwa mshahara mkubwa hata kumzidi waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron.
Kidunia, kiongozi anayelipwa mshahara mkubwa kuliko wote duniani ni Waziri Mkuu wa Singapore, Lee Hsien Loong.
Hsien analipwa dola 2,856,930 kwa mwaka, sawa na Sh. 4.5 bilioni au Sh. 375 milioni kwa mwezi. Singapore, nchi ya kisiwa kidogo kusini mwa Bara la Asia, ni miongoni mwa nchi za eneo hilo zenye uchumi imara.
Nchi hiyo, pamoja na nyingine ndogo ndogo katika eneo hilo la Asia (Malaysia, Thailand, na Taiwan) zinajulikana kama Chui wa Asia (Asian Tigers) kutokana na hatua kubwa za kiuchumi na maendeleo walizofikia.
Kwa mfano kiwango cha maisha ya wananchi wa Malaysia kilikuwa sawasawa na wananchi wa Tanganyika miaka 50 iliyopita wakati nchi hizi mbili zilipopata uhuru kutoka kwa Waingereza. Lakini Malaysia sasa iko mbele ya Tanzania kimaendeleo karibu mara elfu moja.
Obama analipwa mshahara wa dola 400,000 kwa mwaka, sawa na Sh. 640 milioni, ambazo hukatwa kodi. Kutokana na fomu zake za kodi za mwaka jana, rais Obama alionyesha alikuwa na kipato cha dola 5.5 milioni kwa mwaka uliotangulia – 2009.
Hata hivyo nyingi ya fedha hizo zilitokana na mirahaba ya mauzo ya vitabu vyake viwili alivyotunga – The Audacity of Hope (Jeuri ya Matumaini) na Dreams from My Father (Ndoto za Baba Yangu), vitabu vilivyokuwa na mauzo makubwa mwaka 2009.
Ifuatayo ni
orodha ya wakuu wa nchi duniani wanaolipwa mishahara mikubwa.
- Lee Hsien Loong – Waziri Mkuu wa Singapore: Dola 2,856,930 (Tsh 4.5bn) kwa mwaka.
- Donald Tsang – Mtawala Mkuu wa Hong Kong ambayo sasa ni sehemu ya China: Dola 513,245 (Tsh 821m/-) kwa mwaka.
- Raila Odinga – Waziri Mkuu wa Kenya: Dola 427,886 (TSh 684m/-) kwa mwaka.
- Barack Obama – Rais wa Marekani: Dola 400,000 (Tsh 640m/-) kwa mwaka.
- Nicolas Sarkozy – Rais wa Ufaransa – Dola 345,423 (TSh 552.6m/-) kwa mwaka.
- Stephen Harper – Waziri Mkuu wa Canada: Dola 296,400 (Tsh 474.2m/-) kwa mwaka.
- Mary McAleese – Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Ireland: Dola 287,900 (Sh. 460.6 milioni) kwa mwaka.
- Julia Gillard – Waziri Mkuu wa Australia: Dola 286,752 (Sh. 458.8 milioni) kwa mwaka.
- Angela Merkel – Waziri Mkuu (Chancellor) wa Ujerumani: Dola 283,608 (Sh. 453.7 milioni) kwa mwaka.
- Naoto Kan – Waziri Mkuu wa Japan: Dola 273,676 (Sh. 437.8 milioni) kwa mwaka.
- Jacob Zuma – Rais wa Afrika ya Kusini: Dola 272,280 (Sh. 435.6 milioni) kwa mwaka.
- John Key – Waziri Mkuu wa New Zealand: Dola 271,799 ( Tsh 434.8m/-) kwa mwaka.
- David Cameron – Waziri Mkuu wa Uingereza: Dola 215,390 (Sh. 344.6 milioni) kwa mwaka.
- Ma Ying-jeu – Rais wa Taiwan: Dola 184,200 (Sh. 294.7 milioni) kwa mwaka.
- Lee Myung-bak – Rais wa Korea Kusini: dola 136,669 (Sh. 218.6 milioni) kwa mwaka.
"AFRICAN POLITICIAN NI ZAIDI YA UWAJUAVYO"