Utangulizi
Mheshimiwa Dkt. Amani Abeid Karume, Makamu
Mwenyekiti
wa CCM na Rais Mstaafu wa Zanzibar;
Ndugu Pius Msekwa, Makamu Mwenykiti wa CCM wa
Bara;
Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Ndugu Benjamin William
Mkapa;
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania;
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi;
Waziri Mkuu;
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
;
Viongozi Wakuu Wastaafu;
Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Wilson Mukama;
Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM;
Wageni wetu waalikwa kutoka vyama rafiki,
Ndugu zetu wa Vyama vya Siasa Nchini;
Waheshimiwa Mabalozi,
Viongozi wa Dini,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana;
Kama ilivyo ada, naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu,
mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa Dodoma, siku
ya leo, kwenye Mkutano Mkuu wa Nane wa Chama cha
Mapinduzi.
Ndugu Wajumbe;
Karibuni Dodoma. Karibuni Mkutanoni. Nawapeni pole kwa safari.
Tunamshukuru Mungu kwa kutuwezesha kufika salama na tuombe turejee makwetu
salama. Kwa niaba yenu, niruhusuni niwashukuru wenyeji wetu, yaani wana-CCM na
wananchi wote wa Dodoma, wakiongozwa na Alhaji Adam Kimbisa, Mwenyekiti wa CCM,
Mkoa wa Dodoma na Mkuu wa Mkoa Dkt. Rehema Nchimbi, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya
Taifa. Tunawashukuru kwa kutupokea vizuri na kwa ukarimu wao unaotufanya
tujisikie tuko nyumbani katika huu mji ambao ndiyo Makao Makuu ya nchi yetu na
Chama chetu.
Ndugu Wajumbe;
Napenda kuchukua nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa
Halmashauri Kuu ya Taifa kwa matayarisho mazuri ya Mkutano huu wa Nane wa Taifa
wa CCM. Natoa pongezi maalum kwa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa chini
ya uongozi mahiri wa Katibu Mkuu Ndugu Wilson Mukama na Kamati zote za
Maandalizi ya Mkutano kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya ya kuwezesha Mkutano
huu kufanyika. Kwenu nyote nasema hongereni na asanteni sana.
Ndugu Wajumbe;
Karibuni tena Kizota. Nasikitika kwamba matumaini yangu ya
kufanya Mkutano Mkuu katika ukumbi wetu wenyewe hayakutimia. Hii ni kwa sababu
kazi ya matayarisho imechukua muda mrefu kuliko nilivyotazamia. Tumechelewa
kupata kiwanja kilichokidhi mahitaji yetu na matazamio yetu. Kwanza tulipata
kiwanja nyuma ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Lakini tukaona ni mbali mno na
walipo wananchi. Tukaja kupata kiwanja kingine juu ya Kilimani Club ambacho
hakikuwa kikubwa cha kutosha. Mapema mwaka huu ndipo tulipopata kiwanja eneo la
Makulu ambacho kinakidhi sifa za kuwa kikubwa cha kutosha na kuwa karibu na
katikati ya mji wa Dodoma. Tumekiafiki na matayarisho ya kuanza ujenzi
yamekamilika. Leo asubuhi tumeweka jiwe la msingi kuzindua ujenzi wa Ukumbi wa
Mkutano (Dodoma Convention Centre). Baadae utafuta ujenzi wa jengo la Makao
Makuu ya CCM na jengo la Hoteli ya Kisasa.
Wageni Karibuni
Ndugu Wajumbe;
Kama mjuavyo Chama cha Mapinduzi kina marafiki wengi Afrika na
kwingineko duniani. Tumekuwa na mazoea ya kualikana katika mikutano mikuu
yetu. Safari hii tumefanya hivyo tena. Kwa niaba yenu niruhusuni niwashukuru
sana wageni wetu wote wa kutoka vyama rafiki Afrika na duniani kwa kukubali
mwaliko wetu na kuja kujumuika nasi siku ya leo. Kuwepo kwao ni kielelezo tosha
cha udugu na urafiki uliopo baina ya vyama vyetu na nchi zetu ambao hatuna budi
kuudumisha, kuuendeleza na kuukuza. Hali kadhalika, nawashukuru Mabalozi wa
Nchi za Nje na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa walioweza kuja kushiriki
nasi katika sherehe za ufunguzi wa Mkutano wetu.
Ndugu Wajumbe;
Tunawakaribisha kwa furaha na upendo mkubwa viongozi na wawakilishi wa
vyama vya siasa vya hapa nchini kwa kukubali mwaliko wetu na kuja kuhudhuria
Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM siku ya leo. Tunawashukuru kwa moyo wao wa
uungwana kwani tofauti za vyama si uadui. Wamethibitisha jinsi demokrasia ya
vyama vingi inavyozidi kustawi na kukomaa hapa nchini.
Nawashukuru sana pia, viongozi wetu wa dini na wananchi mbalimbali
waliojumuika nasi. Kuwepo kwao ni jambo la faraja kubwa. Dua za viongozi wa
dini zitasaidia kuponya na kuupa baraka mkutano wetu uende salama, uwe wa
mafanikio na kuwafanya wale wote wasiokiombea mema Chama chetu watahayari na
kufadhaika.
Karibuni Diaspora
Ndugu Wajumbe;
Napenda kuwatambua na kuwakaribisha viongozi na wananchama wa Chama
chetu waliopo nje, Marekani, Italia, India na Uingereza. Ndugu zetu hawa kwa
upenzi wao kwa Chama wamesafiri masafa marefu kuja kushiriki nasi. Hawa
wanastahili pongezi maalum kwa jinsi wanavyopeperusha bendera ya CCM na kueneza
sera zake. Naomba tuwape makofi ya nguvu.
Agenda ya Mkutano
Ndugu Wajumbe;
Agenda ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa Nane wa Chama cha Mapinduzi
ina mambo makuu manne. Kwanza kufanya marekebisho ya Katiba ya Chama cha
Mapinduzi. Mengi ya marekebisho hayo yanatokana na uamuzi wa Halmashauri Kuu ya
Taifa katika kikao chake cha trehe 11 – 12 Aprili 2011 wa kufanya mageuzi ndani
ya Chama. Miongoni mwa matunda ya mageuzi hayo ni kuundwa kwa Baraza la Ushauri
na Wajumbe wa NEC kuchaguliwa Wilayani badala ya
Mikoani.
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Halmashauri Kuu ya Taifa ina mamlaka ya
kufanya marekebisho ya Katiba na marekebisho hayo kutumika. Hata hivyo,
marekebisho hayo hayana budi kuletwa katika Mkutano Mkuu wa Taifa ili yaingizwe
rasmi kwenye Katiba.
Ndugu Wajumbe;
Jambo la pili litakuwa ni kwa Serikali zetu mbili kutoa
taarifa za maendeleo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2010 – 2015 tangu
baada ya uchaguzi mkuu hadi sasa. Vile vile, tutapokea Taarifa ya Halmashauri
Kuu ya Chama kuhusu kazi za Chama kwa miaka mitano iliyopita. Jambo la nne na
la mwisho ni kufanya uchaguzi wa Mwenyekiti, Makamu wake wawili na Wajumbe wa
NEC wa Kundi la Zanzibar na Tanzania Bara.
Ndugu Wajumbe;
Tofauti na mikutano iliyopita, Halmashauri Kuu ya Taifa inapendekeza
kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wajigawe katika makundi matano kujadili
taarifa ya kazi za Chama na zile za utekelezaji wa Ilani. Kisha kila kikundi
kitatoa taarifa ya maoni na mapendekezo yake. NEC ilifikiria iwe hivyo ili
kutoa muda wa kutosha kwa wajumbe kujadili taarifa hizo muhimu katika utaratibu
wa zamani wa mtu mmoja kila mkoa kuitwa kusoma, wajumbe hawapati fursa ya
kutosha ya kuzijadili taarifa zinazotolewa.
Kuimarisha Chama Kazi Endelevu
Ndugu Wajumbe;
Katika hotuba yangu ya kushukuru baadaya kuchaguliwa kwa mara
ya kwanza kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kwenye Mkutano Mkuu wa Taifa
Maalum wa tarehe 25 Juni, 20067, pamoja na kuzungumzia mambo mengine,
nilisisitiza umuhimu wa kuimarisha Chama chetu. Nilitoa maoni yangu kwa upana
kiasi kuhusu mambo ya kuzingatia. Leo tena, katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu huu
narudia kusisitiza jambo hili. Nafanya hivyo kwa sababu hilo ndiyo jukumu la
kudumu na jukumu la kwanza na la msingi kwa kila kiongozi na kila mwanachamawa
CCM. Isitoshe, kwa hali ilivyo sasa, kuimarisha Chama cha Mapinduzi lazima iwe
agenda kuu ya kila mmoja wetu. Ni ukweli ulio wazi kuwa ustawi na uhai wa Chama
unategemea viongozi na wanachama kufanya kazi ya ziada kuimarisha Chama
chao.
Ndugu Wajumbe;
Bahati nzuri, chini ya uongozi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu
Lt. Yusuf Rajab Makamba tarehe 19 Desemba, 2006 ulianzishwa Mradi wa Kuimarisha
Chama. Mradi huo ndiyo uliokuwa dira na mwongozo wetu wa kufanya kazi za Chama
tangu wakati huo mpaka leo. Wajibu wa kila kiongozi na kila mwanachama na kila
kikao cha kila ngazi vimeainishwa vizuri. Pia, uliwekwa utaratibu mzuri wa
kufuatilia utekelezaji wake. Bila ya shaka mtakumbuka kuwa utaratibu maalum
uliwekwa wa kutoa tuzo kwa Mikoa iliyofanya vizuri katika utekelezaji wa
vipengele mbalimbali vya uimarishaji wa Chama kwa mujibu wa Mradi
huo.
Ndugu Wajumbe;
Kazi ya kuimarisha Chama chetu ni jukumu endelevu kwa kila mwanachama wa
CCM, kila kiongozi wa CCM na kila mtumishi wa CCM. Kwa sababu hiyo, Mradi wa
Kuimarisha Chama ni mchakato usiokuwa na ukomo. Ni kazi ya kudumu na wala siyo
tukio lililoanzishwa na Katibu Mkuu Lt. Yusufu Rajabu Makamba na kukoma siku
alipostaafu.
Tuongeze Wanachama
Kazi ya kuingiza wanachama wapya ni ya kudumu katika uhai wa
Chama cha Mapinduzi. Hii siyo kazi ya msimu wa uchaguzi wa ndani ya Chama au
wakati wa kura za maoni na hivyo kugeuzwa kuwa ni kwa ajili ya kuwapigia debe
watu wanaotafuta vyeo. Lazima wakati wote tuwe tunaingiza wanachama wapya
lakini pia lazima tuzingatie utaratibu ulioelekezwa na Katiba ya CCM. Hatuna
budi kuhakikisha kuwa tuna wanachama walio waumini wa kweli na wapenzi wa dhati
wa CCM, itikadi yake na sera zake na zile za Serikali
zake.
Ndugu Wajumbe;
Wanachama ndiyo nguvu kuu ya uhai na ushindi wa CCM. Lazima Chama
chetu kiwe na Jeshi kubwa la wanachama walio tayari kukijenga, kukisemea na
kukipigania. Kuwa na Wanachama wengi ambao ni waumini wa kweli wa Chama chetu
ina maana ya kuwa na kura nyingi za msingi za kuanzia katika uchaguzi wa dola.
Pia wanachama ni nyezo muhimu ya CCM kupata kuungwa mkono na wananchi hasa pale
ambapo wanachama wataifanya ipasavyo kazi ya Chama ndani ya umma. Kila
mwanachama akifanya kwa mafanikio kazi ya kushawishi wananchi kupigia kura
wagombea wagombea wa CCM tutapata kura nyingi za
uhakika.
Tuwe na Viongozi Wazuri
Ndugu Wajumbe;
Kazi ya kuhakikisha kuwa Chama cha Mapinduzi kina viongozi
wazuri ni ya kudumu na wala siyo ya msimu wa kuchuja majina ya wagombea. Lazima
Chama chetu kiwe na viongozi ambao ni waumini wa dhati wa itikadi yetu na
wanaozijua vyema sera za Chama cha Mapinduzi na Serikali zake. Wao ndio
wanaotarajiwa kuonesha njia kwa kuelimisha wanachama na wananchi. Viongozi wa
CCM lazima wawe hodari wa kufafanua sera na masuala mbalimbali yahusuyo Chama
chetu na Serikali zake. Hawataweza kufanya hivyo kama wao wenyewe ni maamuma.
Kiongozi mzuri wa Chama cha Mapinduzi ni yule ambaye ni jasiri kukitetea Chama
cha Mapinduzi na kama hapana budi yuko tayari kujitolea muhanga. Kuwa na
kiongozi ambaye haguswi wala kusikitishwa na hali mbaya ndani ya Chama au hujuma
dhidi ya Chama ni sawa na kutokuwa na kiongozi. Bora asiwepo. Na kuwa na
kiongozi ambaye yeye mwenyewe anafanya vitendo viovu dhidi ya CCM na Serikali
zake ni kuwa na nyoka ndani ya nyumba. Ni jambo hatari lisilokubalika na
halistahili kuvumilika. Tukiwajua tuwaseme, tuwashughulikie, wachague
wanapotaka kwenda.
Ndugu Wajumbe;
Kiongozi mzuri wa CCM lazima awe muaminifu na muadilifu na lazima
wanachama na jamii imuone hivyo. Chama chetu kinashindania kushinda akili na
mioyo ya Watanzania na hiyo ndiyo kazi tunayomtarajia kiongozi wetu afanye
katika jamii. Hii ndiyo hasa kazi ya Chama ndani ya umma. Lakini, ili kiongozi
wetu aweze kuifanya kwa mafanikio taswira yake mbele ya jamii ni kitu muhimu.
Awe na taswira nzuri mbele ya wananchi. Kama jamii inamuona kuwa si mtu
muadilifu itakuwa taabu sana kwake kufanikisha jukumu la msingi la Chama chetu.
Hivyo ndugu zangu, lazima tuhakikishe kuwa viongozi wetu wanakuwa waadilifu ili
wasigeuke kuwa balaa na hasara kwa Chama.
Ndugu Wajumbe;
Baada ya kukamilisha mchakato wa uchaguzi ngazi ya taifa,
tutatengeneza na kutekeleza programu maalum ya kutoa mafunzo kwa viongozi wa
Chama kuanzia ngazi ya Tawi hadi Taifa. Hali kadhalika, tutaendeleza na
kukamilisha kazi ya ukarabati na upanuzi wa Chuo cha Ihemi ili kiwe kitovu cha
kutoa mafunzo ya siasa kwa makada na viongozi wa Chama na Jumuiya zake kama
ilivyokuwa inafanywa katika Chuo cha CCM cha Kivukoni na vyuo vyake vya
kanda.
Ndugu Wajumbe;
Bahati nzuri vyama vya ukombozi vya nchi za Mashariki, Kati na Kusini
mwa Afrika vimekubaliana kuwa Chuo cha Ihemi kiwe Chuo cha Mafunzo ya siasa kwa
makada wa vyama vyao pia. Ni heshima kubwa kwa CCM, lakini pia inakipa Chama
chetu wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa Chuo hicho kinawekwa katika viwango vya
kimataifa. Tuko tayari na tutajipanga ipasavyo kutimiza wajibu wetu huo wa
kihistoria.
Vikao Vifanyike Ipasavyo
Ndugu Wajumbe;
Ni kazi endelevu kwetu sote, wanachama na viongozi, kuhakikisha kuwa
vikao vinafanyika kwa wakati na kwamba mikutano inaendeshwa vizuri na ina agenda
zenye maslahi ya kujenga Chama na kuendesha nchi. Pia, ni muhimu kuhakikisha
kuwa kinachoamuliwa kinatekelezwa ipasavyo. Naamini kwamba mafunzo tutakayotoa
kwa viongozi na watendaji wa Chama kuhusu wajibu wao na jinsi ya kuutekeleza
yatasaidia sana kuimarisha CCM.
Watendaji Mahiri
Ndugu Wajumbe;
Kwa Chama chetu kuwa na watendaji wazuri ni jambo lisilokuwa na
mjadala. Lazima tuwe na watendaji ambao ni makada wazuri na watu mahiri kwa
kazi zao. Wawe ni watu ambao wana uelewa mzuri wa sera za Chama na kwamba
wanaweza kuzifafanua, kuzieneza na kuzitetea. Pia, wawe ni watu wanaojua vyema
kazi yao ya utendaji, kwa mujibu wa shughuli zao wanazozifanya. Ni vyema kwa
kazi za kitaalamu tukapata watu wataalamu wa kazi hizo. Ni muhimu sana
tukayazingatia haya kwani utendaji mzuri katika Chama ni nguvu muhimu sana ya
kukifanya Chama chetu kuwa imara. Chama chetu kiwe na mipango thabiti ya
kuwaendeleza watumishi wake na kama hapana budi kuwadhamini wakasome. Tufanye
hivyo.
Bila ya shaka mtakumbuka kuwa tarehe 3 Novemba, 2007, pale Kizota,
niliahidi kuwa tutaboresha maslahi ya watumishi wa Chama. Tumetimiza ahadi
hiyo. Leo nasema kuwa tutajitahidi kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi
wetu kadri uwezo utakavyoruhusu.
Tujitegemee
Ndugu Wajumbe;
Lazima Chama chetu kiwe na uwezo wake chenyewe wa kujisimamia na
kujiendesha. Kiwe na fedha za kutosha na vitendea kazi. Hivi sasa hatuko
hivyo. Hatuna budi kuongeza maarifa na juhudi za kukiwezesha Chama cha
Mapinduzi kujitegemea kifedha bila ya kujali kama kuna ruzuku au hakuna. Jambo
hili sasa liwe ni la kufa na kupona kwetu kuhakikisha linakuwa. Iwe agenda kuu
ya Chama katika ngazi zote. Kila mmoja afikirie nini cha kufanya na kifanywe.
Jambo la kuzingatia ni kufanya shughuli halali. Fursa zipo tuzitumie.
Tusikubali kushindwa kwenye azma kwani hiyo itakuwa maangamizi wa CCM. Lazima
tushinde.
Ndugu Wajumbe;
Mtakumbuka pia kwamba niliahidi kuimarisha usafiri ndani ya Chama.
Ahadi hiyo tumeitimiza. Kila Mkoa na kila Wilaya imepata gari mpya tena gari
nzuri na imara. Gari hizi tukizitunza vizuri zitatuwezesha katika uchaguzi
ujao bila ya taabu. Kwa Mikoa na Wilaya mpya mipango ya kuwapatia magari iko
mbioni. Kila Jumuiya tuliipatia magari yasiyopungua
matatu.
Jumuiya za Chama
Ni wajibu wa kudumu wa Chama chetu kuhakikisha kuwa Jumuiya zake
zinaimarika na kutimiza ipasavyo wajibu wake. Jumuiya ndiyo mkono mrefu wa
Chama cha Mapinduzi kuufikia umma mpana wa Watanzania hasa wale ambao si
wanachama. Jukumu letu ni kuhakikisha kuwa watu hao wanakuwa wanachama au
wapenzi na marafiki wa CCM. Kwa hiyo, kuwepo kwa Jumuiya ni fursa nzuri kwa
Chama cha Mapinduzi kuungwa mkono na watu wengi ili wakati wa uchaguzi tuweze
kupigiwa kura na kupata ushindi. Jumuiya lazima zihakikishe kuwa zinatimiza
ipasavyo wajibu wake ili wasiipotezee CCM fursa hii
adhimu.
Ndugu Wajumbe;
Kwa muhtasari, hayo ndiyo baadhi ya mambo ya msingi ya mradi
wa kuimarisha Chama. Mtakubaliana nami kuwa haya yote ndiyo kazi na wajibu wa
kila mmoja kufanya. Ni kazi endelevu isiyokuwa na ukomo. Tupo kwa ajili hiyo
na rai yangu kwenu ni kuhakikisha kuwa kila mwanachama na kila kiongozi
anatimiza ipasavyo wajibu wake.
Mageuzi Ndani ya Chama
Ndugu Wajumbe;
Kwa dhamira ya kuendelea kukiimarisha zaidi, Chama cha
Mapinduzi, katika mkutano wake wa tarehe 11-12 April, 2011, Halmashauri Kuu ya
Taifa iliamua kuanzisha mchakato na kufanya mageuzi ndani ya Chama. Lengo kuu
la uamuzi huo ni kukiwezesha Chama chetu kuwa na taswira inayovutia katika
mitazamo na hisia za wanachama wake na wananchi.
Kimsingi NEC inataka tukiwezeshe Chama cha Mapinduzi kiendelee kupendwa
na kuaminiwa na wananchi wote wa Tanzania. Tunataka wanawake na wanaume, wadogo
na wakubwa, maskini na matajiri, wanyonge na wenye nguvu waone kuwa CCM ndiyo
kimbilio lao.
Ndugu Wajumbe;
Kwa ajili hiyo mageuzi ya ndani ya Chama yamejengeka juu ya misingi
ifuatayo:-
1. Kukiwezesha Chama cha Mapinduzi kuwa na makada na viongozi mahiri,
waadilifu na waaminifu kwa Chama chao;
2. Kukiwezesha Chama kuwa na sera zinazojali maslahi ya wengi na kusukuma
mbele kwa kasi maendeleo ya taifa letu;
3. Kukiwezesha Chama kuwa na muundo na mfumo wa uendeshaji ulio nyumbulifu
na unaokifanya kuwa karibu na wanachama na wananchi;
4. Kukiwezesha Chama kujitegemea kimapato na kiuchumi ili kiweze kuendesha
shughuli zake kwa uhakika, uhuru na heshima;
5. Kukiwezesha Chama kuwa na watu hodari wa kazi na Makada wazuri ambao
wanalipwa vizuri na kuwezeshwa kutekeleza majukumu yao;
6. Kukiwezesha Chama kuwasiliana na umma kwa urahisi na kupambana na
propaganda chafu za vyama vya siasa; na
7. Kukiwezesha Chama cha Mapinduzi kupambana na maovu ndani ya Chama na
katika jamii likiwemo tatizo la rushwa na mengineyo.
Ndugu Wajumbe;
Katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa iliamuliwa kuwa
kutokana na umuhimu wa hoja na haja ya kufanya mageuzi ndani ya Chama
utekelezaji wa mageuzi uanze mara moja. Aidha, pawepo na progamu ya utekelezaji
unayoainisha nini kinafanyika lini na mhusika ni nani! Bila ya shaka mtakumbuka
kuwa katika kikao kile, tuliunda upya Kamati Kuu na kuteua Sekretarieti mpya.
Vile vile iliamuliwa kuwa tufanye marekebisho katika muundo wa Chama na moja ya
matokeo yake ni Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kuchaguliwa kutoka
wilayani. Nafasi za NEC za mikoa zikafutwa na zile za taifa zikapunguzwa.
Aidha, limeundwa Baraza la Taifa la Ushauri ambalo wajumbe wake ni viongozi
wakuu wa Chama wastaafu. Wanapata fursa ya kukaa na kutoa ushauri kwa Chama na
viongozi wake.
Ndugu Wajumbe;
Tuliamua, pia, kuunganisha chaguzi za Chama na Jumuiya
zifanyike mwaka mmoja. Shabaha ya uamuzi huo ni kutaka kujipa muda wa kutosha
wa kujenga Chama na Jumuiya zake na kujiandaa kwa chaguzi za dola. Uamuzi huo
umeokoa takriban mwaka mzima ambao tulikuwa tunautumia kwa uchaguzi. Vile vile
Halmashauri Kuu ya Taifa iliamua kwamba mgao wa fedha unatokana na mapato Chama
zinazopelekwa kwenye Matawi na Mashina uongezwe. Lengo ni kuziwezesha ngazi
hizi muhimu za Chama kufanya kazi vizuri zaidi.
Ndugu Wajumbe;
Suala la nidhamu na maadili ya viongozi na wanachama
lilisisitizwa sana kwa sababu ya umuhimu wake kwa taswira ya Chama chetu mbele
ya jamii na wanachama wake. Pia, kutokana na ukweli kwamba ni kilio cha
wanachama na wananchi cha kutaka tuiondowe taswira mbaya dhidi ya Chama iliyopo
katika jamii kuwa ni Chama kisichokerwa na rushwa. Hicho ni kilio cha dhati kwa
watu wenye nia njema na CCM: Chama chao, wanachokipenda na kukiamini. Chama
ambacho bado hakina badala yake wa kuiongoza vyema nchi yetu na watu
wake.
Halmashauri Kuu ya Taifa iliamua mambo mawili yafanyike. La
kwanza, mfumo mzima wa kushughulikia masuala ya usalama na maadili katika Chama
utazamwe upya na uimarishwe. Pili, Chama kichukue hatua na lazima kionekane
kinachukua hatua dhidi ya viongozi na wanachama wasiokuwa waadilifu na waaminifu
wanaofanya sura ya Chama ichafuke mbele ya jamii. NEC iliagiza wenyewe wajipime
na kuamua na wasipofanya hivyo vikao husika katika Chama vichukue
hatua.
Ndugu Wajumbe;
Hayo ni baadhi tu ya mambo muhimu yaliyoamuliwa yafanyike
katika kufanya Mageuzi Ndani ya Chama. Utekelezaji wake umeanza. Yapo
yaliyokamilika na yapo yanayoendelea kutekelezwa. Yapo mambo mengi ambayo ni
endelevu kama vile mapambano dhidi ya rushwa. Hatuna budi kuendelea kulikemea
na kusimama kidete kupambana na tatizo hili mpaka likomeshwe. Ni kwa maslahi na
heshima ya Chama chetu kuendesha mapambano haya bila ya woga mpaka tushinde.
Tukishindwa itakuwa hatari kwa uhai wa Chama chetu.
Umoja ni Ushindi
Ndugu Wajumbe;
Mara ya mwisho tulipokutana tarehe 11 Julai, 2010, tulikuwa
tunajipanga kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Mliniteua mimi na Dkt.
Mohamed Ghalib Billal kupeperusha bendera ya CCM kwa nafasi ya Rais na Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia tulipitisha Ilani ya Uchaguzi ya
2010-2015. Siku moja kabla ya Mkutano Mkuu, Halmashari Kuu ya Taifa ilikuwa
imemteua Dkt. Ali Mohamed Shein kupeperusha bendera yetu kwa nafasi ya Rais wa
Zanzibar.
Bahati nzuri tumepata ushindi kwa nafasi zote hizo za juu za uongozi wa
taifa letu. Pia tulifanikiwa kupata Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
wengi zaidi kuliko vyama vya upinzani. Kwa sababu hiyo, tumeunda Serikali zote
mbili za nchi yetu na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi unaendelea
vizuri.
Ndugu Wajumbe;
Kwa upande wa Zanzibar, tuna Serikali ya Umoja wa Kitaifa na
mambo yanakwenda vizuri. Tuzidi kuunga mkono na kuwatakia heri Rais wa Zanzibar
Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Seif Sharif Hamad
na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd. Tunawapongeza sana kwa
mafanikio yaliyopatikana. Zanzibar ina amani na umoja unaozidi kuimarika.
Tunatakiwa tuendelee kuiunga mkono Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili ifanikiwe
zaidi.
Ndugu Wajumbe;
Uchaguzi uliopita kwa upande wa Tanzania Bara ulikuwa na
changamoto nyingi ambazo hatukuzizoea wala kujiandaa nazo. Zinaelezea matokeo
tuliyoyapata jambo ambalo linatulazimu kuwa makini zaidi katika uchaguzi ujao.
Tusikubali kushtukizwa tena. Lakini, jambo moja lililo dhahiri ni kwamba umoja
na mshikamano miongoni mwa wana-CCM ndiyo uliotuwezesha kukabili changamoto hizo
na kupata ushindi tulioupata. Bila ya hivyo, mbinu hasi zilizotumika
zingetufanya tushindwe.
Napenda ukweli huu uwepo katika vichwa na mioyo ya wana-CCM na sisi
viongozi wao tuliochaguliwa hivi majuzi na watakaochaguliwa katika Mkutano huu.
Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere alisema: Umoja ni Nguvu, ni
kweli kabisa na sisi ni mashahidi. Nami napenda kuongeza kwa kusema
kuwaUmoja ni Ushindi.
Ndugu Wajumbe;
Nawaomba wakati wote wa mkutano na baada ya mkutano tukumbuke
na kuzingatia Umoja. Tuishikilie kamba ya Umoja isituponyoke. Tuimbe Umoja
kimoyo moyo na tubainishe wazi wazi kwa kauli na matendo yetu kuwa: Umoja ni
Nguvu Utengano ni Udhaifu! Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi!. Napenda
kuona kuwa tunatoka hapa tukiwa kitu kimoja, tukiwa watu tunaopendana na
tulioshikamana. Nataka tuondoke katika Mkutano sote tukivuta kamba upande
mmoja badala ya kuvutana. Nataka tuazimie kukabiliana na kauli, matendo au watu
wanaopandikiza chuki na kuhatarisha umoja ndani ya Chama chetu na miongoni
mwetu. Nataka kaulimbiu ya ujumbe wa Mkutano huu uwe Umoja ni Ushindi!
Umoja na Ushindi! Tukiendelea kuwa watu tunaovutana na kuhasimiana
hatutaweza kukijenga Chama chetu wala kuwatafutia ushindi wagombea wa Chama
chetu. Tutakuwa sawa na ule msemo wa Kiswahili usemao: “vita vya panzi
furaha ya kunguru” Tusijigeuze panzi na wala tusikifikishe Chama chetu kiwe
hivyo.
Ndugu Wajumbe;
Mtakubaliana nami kuwa harakati za kutafuta uongozi ndani ya
Chama au uteuzi wa kugombea katika chaguzi za dola imekuwa ndiyo chanzo kikuu
kinacholeta mifarakano na kuvuruga umoja ndani ya Chama chetu. Hili ndugu zangu
siyo sawa hata kidogo. Kugombea uongozi ni haki ya msingi ya mwanachama na raia
wa Tanzania. Kwa nini mtu achukiwe au aonekane adui kwa kuamua kuitumia haki
yake hiyo? Kwa nini afanyiwe vitimbi, vitendo viovu au njama za kuhujumiwa?
Nani mwenye haki zaidi ya mwanachama ama raia mwenzake? Ni ubabe na jeuri ya
pesa isiyokuwa na msingi. Ni ubinafsi na uchu wa madaraka uliopitiliza mipaka.
Watu wa namna hiyo ni hatari sana kwani wanaweza hata kuua au kukivuruga Chama
chetu kizuri kama tamaa zao zisipokidhiwa.
Ndugu Wajumbe;
Napenda kutumia nafasi hii kuwasihi wale wote wanaochukiana
kwa sababu ya kugombea watakafakari upya misimamo yao. Wafanyayo siyo sahihi,
wanaathiri nguvu na uhai wa Chama chetu. Naomba Kamati za Siasa za ngazi zote
ziwatambue watu hao na kuwaita kuwapatanisha. Naomba wahusika watoe ushirikiano
wao. Hata wale wanaohisi kuwa hawakutendewa haki katika uchaguzi, walidhulimiwa
au hata kushindwa kwa sababu ya vitendo vya rushwa, wakumbuke kuwa Chama chetu
kina utaratibu wa kushughulikia malalamiko yao. Wautumie utaratibu huo badala
ya kufanya vitendo vinavyokigawa na kukivuruga Chama chetu. Kulalamika katika
vyombo vya habari, kufanya ghasia au kuchochea migawanyiko hakutaleta
ufumbuzi.
Ndugu Wajumbe;
Niruhusuni nitumie nafasi hii kuwasihi wale wote wenye tamaa
ya kugombea uteuzi ndani ya Chama wasituulie Chama chetu. Kuwa na tamaa ya
kugombea Urais, Ubunge na Udiwani si kosa ni haki ya mwanachama na ni haki ya
raia wa nchi hii. Jambo ambalo halikubaliki na gumu kulivumilia ni kufanya
vitendo vya kuwagawa wanachama na Chama chetu. Kuwalazimisha au kuwashinikiza
kujiunga na kundi fulani siyo sawa. Kumchukia mtu kwa sababu naye anagombea au
amekataa kukuunga mkono au kumuunga mkono umpendae ni jambo baya. Unaifanya
demokrasia iwe haina maana au kichekesho. Na, lililo baya kupita kiasi ni
kutumia fedha kushawishi, kuwarubuni au kuwanunua watu kukuunga mkono au
kumuunga mkono mgombea wako au kujiunga na makundi. Hili ni jambo haramu na ni
utovu wa maadili usiokubalika ambao lazima tuukatae, tuukemee na tuupige vita
kwa nguvu zetu zote. Naomba wote tushirikiane katika mapambano haya kwa heshima
ya Chama chetu.
Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi
Ndugu Wajumbe;
Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010 unakwenda
vizuri kwa Serikali zetu zote mbili. Taarifa zitakazotolewa na Waziri Mku,
Mheshimiwa Mizengo Pinda, kwa upande wa Serikali ya Muungano na Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd kwa upande wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, zitathibitisha ukweli huu. Niruhusuni nichukue muda wenu
kidogo nizungumzie baadhi ya mambo yahusuyo shughuli za
Serikali.
Nchi Iko Salama
Ndugu Wajumbe;
Napenda kuanza kwa kuwahakikishia kuwa Tanzania iko salama
pamoja na kuwepo matukio ya hapa na pale. Mipaka yetu iko salama. Hakuna
tishio lo lote la kiusalama la kutufanya tuhamanike. Hata mpaka wetu na Malawi
uko salama pamoja na kuwepo kwa maneno maneno yahusuyo nchi zetu mbili
kutofautiana wapi ulipo mpaka halali. Hakuna jambo lo lote linalofanywa upande
wa wenzetu ambalo linatufanya tuwe na mashaka ya usalama wa nchi yetu kuwa
hatarini. Kwa sababu hiyo hatujaiona haja ya kusogeza Majeshi yetu mpakani na
anayesema tumefanya hivyo ni muongo. Apuuzwe na
kushushuliwa.
Ndugu Wajumbe;
Tumeendelea na juhudi za kuimarisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania kwa kuwajengea uwezo, zana na vifaa vya kisasa vya kivita. Lengo letu
ni kukuza nguvu ya kimapigano ya Jeshi letu na kuimarisha utayari wake kivita.
Hali kadhalika, tumeendelea kuboresha maslahi ya wanajeshi na mazingira yao ya
kufanyia kazi na ya kuishi. Kwa upande wa usalama wa raia, yaani maisha na mali
zao, matukio ya uhalifu yanaendelea kupungua. Hali hii inaashiria kuwa Jeshi la
Polisi linafanya kazi nzuri. Kama tufanyavyo kwa JWTZ, tutaendeleza juhudi za
kuimarisha Jeshi la Polisi kwa watu, zana na vifaa vya kisasa vya kufanyia
kazi. Tutaendelea kuboresha maslahi na mazingira ya kufanyia kazi na ya kuishi
ya Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama.
Ndugu Wajumbe;
Pamoja na kutokuwepo kwa tishio lililo dhahiri la shambulio la
kigaidi, wakati wote vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viko katika hali ya
tahadhari kuepuka kushtukizwa. Kama mnavyokumbuka mwaka 1998 Ubalozi wa
Marekani hapa nchini ulishambuliwa na ndugu zetu 11 walipoteza maisha. Hivyo
basi, kuchukua tahadhari ni jambo la busara kufanya. Aidha, tuko katika hali ya
tahadhari dhidi ya uharamia wa kuteka meli katika Bahari Kuu ya Hindi. Takriban
mwaka mzima umepita bila ya matukio ya kutekwa nyara meli katika bahari yetu .
Hata hivyo hatuachi kuchukua tahadhari.
Ndugu Wajumbe;
Matukio ya hivi karibuni ya vurugu zenye mwelekeo wa kidini
yanasikitisha na kusononesha. Ni mambo ambayo hayafanani na sifa ya nchi yetu
ya kuheshimiana na kuvumiliana pamoja na kuwepo tofauti zetu za dini, kabila
rangi au maeneo tutokako. Vitendo hivyo havikubaliki na Serikali haitawavumilia
au kuwaonea muhali wale wote wanaohusika na kuchochea vurugu hizo. Tumechukua
hatua na tutaendelea kuchukua hatua bila ya ajizi. Ombi langu na wito wangu kwa
viongozi na wafuasi wa dini nchini kuhubiri dini zao huku wakitambua na
kuzingatia umuhimu wa kuheshimu imani za wengine na kuvumiliana. Tusipofanya
hivyo nchi yetu tutaingiza kwenye matatizo yasiyostahili
kuwepo.
Ndugu Wajumbe;
Inatia moyo kuona kuwa watu wenye nia njema na nchi yao ni
wengi. Kwa sababu hiyo pamoja na jitihada za baadhi ya watu wasiyoitakia mema
nchi yetu hawajafanikiwa kuwagawa na kuwafarakanisha Watanzania. Nawaomba
Watanzania wenzangu tuwe na moyo huo huo na sisi katika Serikali tutaendelea
kumchukulia hatua mtu ye yote anayetaka kutuvurugia amani na utulivu wa nchi
yetu na watu wake.
Ndugu Wajumbe;
Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali haitamuonea mtu ye yote
asiyehusika. Tutaendelea kuidumisha sifa yetu ya kuendeleza utawala bora,
kuheshimu haki za binadamu na kuzingatia utawala wa sheria. Kadhalika
tutaendelea kuheshimu mgawano wa madaraka miongoni mwa mihimili mikuu ya dola.
Nafurahi kwamba mpaka sasa mambo yanakwenda vizuri.
Muungano Imara
Ndugu Wajumbe;
Muungano wetu ni imara pamoja na kuwepo vitendo vyenye lengo
la kuudhoofisha vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa siasa na wa dini hasa
kule Zanzibar. Jambo linalosikitisha ni watu hao kutumia njia za vitisho na
ghasia ili kuwalazimisha watu kuwaunga mkono. Njia hizo hazikubaliki na wala
hazitavumiliwa.
Inastaajabisha mambo hayo kufanyika hivi sasa wakati kuna Tume ya
Katiba. Kama mtu ana maoni yo yote kuhusu Muungano ayafikishe tu, yatapokelewa
na kupimwa. Vile vile Kamati ya Pamoja ya Serikali zote mbili inayowakutanisha
Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar chini ya Uenyekiti wa Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano imekuwa inafanya kazi nzuri kutatua kero za
Muungano. Kama mtu analo jambo analotaka lipatiwe jawabu awasilishe kwa
wahusika litashughulikiwa.
Hali
ya Uchumi
Ndugu
Wajumbe;
Katika
Mkutano Mkuu Maalum wa Julai, 2010 hapa Kizota, nilielezea mafanikio
tuliyoyapata na changamoto tulizokumbana nazo katika kukuza uchumi wa nchi yetu
na kupunguza umasikini. Nilieleza pia nia yetu ya kuendelea kupambana na
changamoto zilizokuwa mbele yetu pamoja na ugumu unaotokana na hali ya kuyumba
kwa uchumi wa dunia ambamo na sisi pia tumo. Kwa ajili hiyo mwaka 2011
tulizindua Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano(2011/12 –
2015/16).
Mpango
huu ni wa kwanza kati ya mitatu katika safari yetu ya kutekeleza Dira ya
Maendeleo ya mwaka 2025. Kwa mujibu wa Dira yetu hiyo, tunatarajia ifikapo
mwaka 2025 nchi yetu itaondoka katika kundi la nchi maskini sana duniani na kuwa
nchi ya uchumi wa kati. Yaani tunataka pato la wastani la Watanzania litoke
kwenye dola zaKimarekani 545 za sasa hadi kufikia dola za Kimarekani
3,000. Lengo hilo ni kubwa linalohitaji mipango thabiti na uwekezaji makini
wa Serikali na sekta binafsi. Pia inahitaji kuwepo kwa nidhamu ya dhati ya
viongozi na wananchi wa Tanzania.
Ndugu
Wajumbe;
Utekelezaji
wa Mpango wa Maendeleo umekwishaanza. Lengo la jumla katika Mpango wa kwanza
ni Kufungulia fursa kwa ukuaji wa uchumi; wa pili ni Ujenzi wa
mazingira ya maendeleo ya viwanda; na wa tatu ni Kuimarisha ubunifu na
ushindani kimataifa. Tayari miradi ya kimkakati imekwishaainishwa na
inapewa kipaumbele katika bajeti ya Serikali na ubia baina ya sekta binafsi na
sekta ya umma. Katika kila hatua suala la kukuza ajira limepewa umuhimu mkubwa
kwani lengo letu ni kuwa na ukuaji wa uchumi unaojumuisha maisha ya watu.
Vijana ni walengwa wakubwa.
Mwelekeo
wa uchumi wetu ni mzuri. Kasi ya ukuaji wa uchumi iliyokuwa asilimia 6.4 mwaka
wa jana inatarajiwa kufikia asilimia 7 mwaka huu. Mauzo yetu ya nje yanazidi
kukua na kuongezeka. Kwa mfano mwaka 2005 ilikuwa dola za Kimarekani milioni
2,945.5 na sasa ni milioni 7,461.2. Akiba yetu ya fedha ya kigeni
nayo ni nzuri. Hivi sasa ni dola za Kimarekani bilioni 4.1inatuwezesha
kuagiza bidhaa kutoka nje kwa miezi 3.8.
Ndugu
Wajumbe;
Changamoto
kubwa katika uchumi ni mfumuko wa bei. Ni kweli umepungua kutoka asilimia 19.8
Desemba, 2011 hadi asilimia 13.5 Septemba, 2012, hata hivyo kupungua huko ni
kidogo mno. Tunaendelea kuchukua hatua za kudhibiti na kupunguza zaidi mfumuko
wa bei. Kwa vile moja ya sababu ni kupanda kwa bei za mafuta. Tumeipa dhamana
EWURA kusimamia kwa karibu uagizaji na upangaji wa bei ya
mafuta.
Kwa kuwa bei za vyakula hasa mchele na sukari navyo huchangia kupanda kwa
mfumuko wa bei na kuongeza gharama ya maisha mamlaka husika zimeagizwa
kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanawezeshwa kuagiza bidhaa hizo kwa wingi
kutoka kwa nje kwa kuwapatia nafuu ya baadhi ya kodi. Pamoja na hayo jawabu la
kudumu lipo katika kuendeleza mageuzi ya kilimo ili nchi yetu ijitosheleze kwa
chakula na kupata ziada kubwa ya kuuza nje. Hayo ndiyo malengo na hatua
zinazochukuliwa katika ASDP, Kilimo Kwanza na SAGCOT. Ndiyo maana tutaendelea
kutoa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima, kuimarisha masoko na miundombinu
vijijini.
Mapato na Matumizi ya Serikali
Ndugu Wajumbe,
Tunazidi kupata mafanikio ya kutia moyo kwa upande wa ukusanyaji wa
mapato ya Serikali. Makusanyo ya mapato ya kodi Mwezi Agosti 2012, kwa mfano,
yalifikia shilingi bilioni 554.8ikilinganishwa na makusanyo ya
shilingi bilioni 147 mwezi Desemba 2005. Mafanikio haya yametokana na juhudi za
dhati za Serikali katika kusimamia mabadiliko ya sera na kuimarisha mifumo na
taasisi za ukusanyaji wa mapato ya kodi na mengineyo.
Kwa sababu ya kuongezeka huko kwa mapato, bajeti ya Serikali nayo
imeongezeka kutoka shilingi trilioni 4.13 mwaka 2005/06 hadishilingi
trilioni 15.12 mwaka huu. Jambo linaloleta faraja ni kuwa mchango wa
Serikali kutokana na bajeti hiyo nao umeongezeka kutoka shilingi trilioni
2.1 mwaka 2005 hadi trilioni 8.8 mwaka huu. Utegemezi wa wahisani
nao unaendelea kupungua kutokaasilimia 44 mwaka 2005/6
hadi 21.
Ndugu Wajumbe;
Sambamba na kuongeza mapato, nidhamu, udhibiti wa matumizi ya fedha
na mali za umma vinazidi kuimarika. Hii ni kutokana na kuimarika kwa mifumo na
kada ya uhasibu katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Pia ni matokeo ya
kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma. Hati Chafu katika idara za
Serikali zinaendelea kupungua katika taarifa ya ukaguzi kila mwaka. Hivi sasa
tunaelekeza nguvu zetu katika kuhakiki thamani ya fedha zilizotumika na kazi
iliyofanyika au huduma iliyotolewa.
Uwekezaji
Ndugu Wajumbe,
Serikali imechukua hatua kadhaa kuboresha mazingira ya uwekezaji na
ya kufanya biashara hapa nchini. Lengo letu ni kuvutia wawekezaji wa ndani na
nje kuongeza vitega uchumi nchini na kupanua biashara ndani ya nchi na kati ya
nchi yetu na nchi nyingine duniani. Tunafanya hayo kwa kutambua ukweli kwamba
uchumi unakua na kuongezeka pale ambapo uwekezaji unaongezeka. Takwimu
zinaonyesha kwamba uwekezaji umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka katika sekta
ya utalii, viwanda, kilimo, madini, fedha, ujenzi na sasa kwenye utafutaji wa
gesi na mafuta. Tumepata mafanikio makubwa katika utafutaji wa gesi na
nchi yetu itakuwa moja ya mzalishaji mkubwa wa gesi. Mwaka 2011, kwa mfano,
kulikuwa na jumla ya miradi 826 yenye thamani ya dola za
Kimarekani milioni 7,177 itakayozalisha ajira ya watu 79,000.
Haya ni mafanikio madogo lakini tunaweza kufanya vizuri
zaidi.
Tutaendelea kutumia fursa ya kijiografia ya nchi yetu kuvutia uwekezaji na kuifanya
Tanzania kuwa lango kuu la biashara na usafirishaji kwa nchi za Afrika ya
Mashariki na Kati. Ili kufanikisha hayo, tutaendelea kuboresha miundombinu ya
barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege na
teknohama.
Miundombinu
Ndugu wajumbe;
Moja ya vipaumbele vya juu vya Serikali ya CCM ninayoiongoza
ni kuboresha miundombinu ya usafiri wa ardhini, majini na angani nchini.
Tumethibitisha hayo kwa mgao wa fedha za bajeti ya Serikali ambapo miundombinu
ni ya pili baada ya elimu. Mwaka huu ni shilingi trilioni 2.4, ambayo
ni asilimia 16 ya bajeti ya Serikali ukilinganisha na elimu
yenye trilioni 3.6 ambayo ni sawa na asilimia 2.4, na afya yenye
shilingi trilioni 1.5 sawa na asilimia 10 ya bajeti ya Serikali.
Tunafanya hivyo kwa kutambua mchango muhimu wa sekta ya usafiri kwa maendeleo ya
nchi yetu na watu wake. Usafiri unapokuwa bora na wa uhakika, gharama za
usafirishaji zinapungua, shughuli za uzalishaji viwandani na kilimo
zinaimarika. Ni kichocheo kikubwa cha kuibuka kwa fursa mbalimbali za uchumi na
kuongeza kasi ya maendeleo na kukuza kipato cha Watanzania waliopo mijini na
vijijini.
Ndugu Wajumbe;
Tunafanya uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa barabara kuliko
wakati mwingine wo wote katika historia ya nchi yetu. Hivi sasa barabara zenye
urefu wa kilometa 11,154 zinajengwa kwa kiwango cha lami katika sehemu
mbalimbali nchini. Tulijipa lengo la kuunganisha mikoa yote kwa barabara za
lami na barabara zote kuu ziwe za lami.
Nafurahi kusema kuwa utekelezaji wake unakwenda vizuri. Tumeanza
kufanikiwa kuifikia ile mikoa ambayo kwa muda mrefu ilikuwa haifikiki kwa
urahisi kwa kukosa barabara za lami. Katika hotuba yangu ya tarehe 25 Juni,
2006 niliwaambia Wajumbe wa Mikoa ya Ruvuma, Rukwa, Mtwara, Kigoma na Tabora
kuwa kilio chao tumekisikia. Niliahidi kuwa ujenzi wa barabara katika Mikoa
hiyo tutaipa kipaumbele. Tumetimiza ahadi hiyo na kazi inaendelea kwa kasi na
hata wenyewe ni mashahidi. Karibu tunafikia ndoto yetu ya kwamba hakuna mkoa
utakaoachwa nyuma.
Ndugu Wajumbe;
Inafurahisha zaidi kuona kuwa zaidi ya asilimia 60 ya gharama za
ujenzi wa barabara tunazojenga nchini ni fedha zetu wenyewe. Aidha, uwezo wa
Mfuko wa Barabara (Road Fund) nao umeongezeka sana kutoka shilingi bilioni
58 mwaka 2005 hadishillingi bilioni 430. Hali hiyo imeongeza uwezo
wetu wa kujenga na kukarabati barabara mbalimbali nchini. Kwa ajili hiyo
tumeongeza bajeti ya barabara kwenye Halmashauri zote
nchini.
Ndugu Wajumbe;
Pamoja na barabara, tunaendelea kuimarisha viwanja vya ndege, bandari na
usafiri wa reli. Changamoto mbalimbali zinajitokeza katika utekelezaji wa
lengo letu na kubwa zaidi ikiwa ni ile ya gharama za ujenzi na ukarabati wa
miundombinu kuwa kubwa mno ikilinganishwa na uwezo wetu. Tunaendelea kuchukua
hatua mbalimbali kuzikabili changamoto hizo hatua kwa hatua na
tunazipunguza.
Elimu
Ndugu wajumbe;
Tumefanikiwa kupanua sana fursa za kuwapatia elimu vijana wetu katika
ngazi zote. Kuna watoto wengi katika elimu ya awali, na kwa elimu ya
msingi asilimia 97 ya watoto wenye umri wa kwenda shule wamejiandikisha.
Kwa kiwango hicho, tuko mahali pazuri kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka
2015 kama ilvyoagiwa katika Malengo ya Milenia ya Umoja wa Mataifa. Kuhusu elimu
ya Sekondari, wananchi na wadau wengine wameitikia wito wa Serikali wa kila Kata
kuwa na shule ya sekondari. Kwa sababu hiyo idadi yashule
3,165 zimejengwa kati ya 2005 na hivi sasa na idadi ya wanafunzi katika
shule za sekondari imeongezeka kutoka 524,325mwaka 2005
hadi 1,884,272 mwaka huu.
Tumepanua sana mafunzo ya ufundi na elimu ya juu. Hivi sasa nchi yetu
ina vyuo vikuu 27 na wanafunzi waliopo vyuoni humo ni zaidi
ya 166,484 ikilinganishwa na 40,719 wa mwaka 2005. Ili kutoa
fursa sawa kwa wanafunzi wote tumeongeza sana uwezo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu
ya Juu ili iwape wanafunzi wengi mikopo ya elimu. Bajeti ya Bodi hiyo
imeongezeka kutoka shilingi bilioni56.1 mwaka 2005 hadi
shilingi bilioni 306.0 mwaka huu. Wanafunzi wanaopata mikopo
wapo 93,176 ukilinganisha na 16,345 mwaka 2005. Tutaendelea
kuongeza fedha ili tuwafikie wanafunzi wengi kadri
inavyowezekana.
Ndugu Wajumbe;
Upanuzi mkubwa wa elimu katika ngazi zote nchini umezua changamoto
mbalimbali kuhusu ubora wa elimu. Tunazitambua changamoto hizo kuwa ni pamoja
na zile za upungufu wa walimu, hususan wa sayansi; upungufu wa vifaa vya
maabara, vitabu na nyumba za walimu hasa kwenye maeneo ya vijijini.
Tumejipanga vyema kuzitafutia ufumbuzi na tumeanza kufanya hivyo. Tumeongeza
vyuo vinavyotoa mafunzo ya ualimu ili kuongeza idadi ya waalimu. Bajeti ya
elimu ni kubwa kuliko zote ili kusaidia kutatua tatizo la upungufu wa vitabu,
maabara, vifaa vya kufundishia na nyumba za walimu na mahitaji mengineyo. Hivi
karibuni nilipokuwa Mkoani Singida nimewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote
nchini kuhakikisha kuwa shule zote za sekondari katika maeneo yao zinakuwa na
maabara ya sayansi katika miaka miwili ijayo.
Afya
Ndugu wajumbe;
Suala la afya ya Watanzania tunalipa umuhimu mkubwa sana. Tumeongeza
bajeti ya afya kutoka shilingi bilioni 271 mwaka 2005 hadi shilingi
trilioni 1.5 mwaka huu. Nyongeza hii ndiyo iliyotuwezesha kutekeleza Sera
mpya ya Afya (2007) na Mpango wa Miaka Kumi wa Maendeleo ya Afya ya Msingi
(MMAM) wa kuitekeleza vyema Sera hiyo. Lengo kuu la sera na MMAM ni kuwapatia
Watanzania huduma ya afya iliyo bora katika umbali usiozidi kilometa tano. Vile
vile, ni kuimarisha huduma zinazotolewa katika hospitali za Wilaya, Mikoa, Kanda
na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Katika mpango huu pia tumeazimia kukabili tatizo la upungufu wa
madaktari, wauguzi na wataalamu wengi. Tunaendelea kupanua mafunzo ya wataalamu
hao katika vyuo vyetu hapa nchini na hata nje ya nchi. Tumejenga na tutaendelea
kujenga vyuo vipya, wakati huo huo tukipanua vilivyopo. Tumeendelea kujenga
uwezo wa kupambana na maradhi makubwa yanayoua watu wengi. Tumeelekeza nguvu
zetu kwenye maradhi yanayoambukiza kama vile malaria, UKIMWI na kifua kikuu na
yale yasiyoambukiza kama vile saratani, moyo, shinikizo la damu na vifo vya kina
mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka
mitano.
Ndugu Wajumbe;
Kwa maradhi yote mafanikio ya dhahiri yanaendelea kupatikana.
Maambukizi ya virusi vya UKIMWI yanapungua kutokaasilimia
8 hadi asilimia 5.7, vifo kutokana na malaria vimepungua
kwa asilimia 40 kwa Tanzania Bara na kwa Zanzibar tunakaribia kutangaza
kufutika kwa maradhi hayo. Tumepanua uwezo wa kutibu maradhi ya moyo ikiwa ni
pamoja na kufanya upasuaji wa moyo. Tumepanua uwezo wa kuchunguza na kutibu
maradhi ya kansa. Tunaendelea kujenga uwezo wa ndani kwa maradhi tunayopeleka
wagonjwa wengi nje na mafanikio yanaaza kuonekana. Safari ni hatua, naamini
tutafika kwani mwelekeo wetu ni mzuri.
Umeme na Maji
Ndugu wajumbe;
Tunaendelea kupanua uwezo wetu wa kuzalisha na kusambaza umeme nchini.
Tumeanza safari ya uhakika ya kupunguza kutegemea mno umeme wa nguvu ya maji.
Tunapanua umeme utokanao na vyanzo vingine hasa gesi asilia na makaa ya mawe.
Mipango ya kutumia upepo na mionzi ya jua nayo iko mbioni. Pamoja na hayo
tunayo mikakati ya kupunguza umeme unaozalishwa kwa kutumia mafuta kwa kubadili
mitambo hiyo iweze kutumia gesi asilia.
Hivi majuzi tu nilizindua ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar
es Salaam. Litakapokamilika nchi yetu itakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati
3,000 na kuung’oa mzizi wa fitina wa mgao na upungufu wa umeme nchini.
Tumeendelea kuwekeza katika usambazaji wa umeme nchini jambo ambalo
limetuwezesha kuwapatia umeme kwa asilimia 18.4 Watanzania
kutoka asilimia 10mwaka 2005. Kwa kasi hii naamini tutafikia lengo
la asilimia 30ifikapo 2015.
Kwa upande wa maji, jitihada za kuwapatia wananchi maji safi na salama
zinaendelea vizuri. Eneo hili lina changamoto kuu mbili. Kwanza ni ule ukweli
kwamba kuna baadhi ya maeneo ya nchi yetu hayana vyanzo vya maji karibu au
hayapati mvua za kutosha au yana ukame. Katika maeneo ya aina hii upatikanaji wa
maji huwa wa shida sana na hivyo kutulazimisha kujenga miradi ya maji ya bomba
kutoka masafa marefu. Changamoto yetu ya pili ni ule uwezo mdogo wa kifedha kwa
miradi mingi inayohitaji pesa nyingi. Mwaka 2006 tulianzisha Programu ya
Maendeleo ya Sekta ya Maji. Kufuatia utekelezaji ulio makini wa programu
ya sekta ya maji, asilimia 60 ya watu wa vijijini na asilimia
86 ya watu wa mijini wanaopata maji safi na salama. Ni matumaini yangu kuwa
tutafikia lengo letu la asilimia 65 la upatikanaji maji kwa vijijini
na asilimia 90 kwa mijini ifikapo 2015. Bahati nzuri tunayo miradi ya
maji inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini na itapokamilika
tutafikia lengo letu au hata kulivuka.
Pongezi kwa Kuchaguliwa
Ndugu Wajumbe;
Katika Mkutano huu, Ndugu Amani Abeid Karume, Makamu
Mwenyekiti wa Zanzibar na Ndugu Pius Msekwa, Makamu wa Mwenyekiti wa CCM kwa
upande wa Tanzania Bara watastaafu. Ndiyo maana NEC imeamua kuwapendekeza kwenu
Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na
Ndugu Philip Mangula kuchukua nafasi zao. Napenda kuchukua nafasi hii
kwashukuru kw dhati Rais Amani Abeid Karume na Mzee Msekwa kwa kazi kubwa na
nzuri waliyoifanya kunisaidia kuongoza Chama chetu. Wamekifanyia Chama chetu
mambo mengi mazuri ambayo hatuna budi kuwapongeza na kuwashukuru. Waliendelea
kuwa walimu wangu na washauri wangu kwa mambo mengi ya Chama na nchi.
Nawashukuru sana. Sote tuwatakie afya njema na maisha marefu. Na tumuombe Mzee
Msekwa asichoke kuandika ili hazina yake kubwa ya uzoefu na maarifa iwanufaishe
wengi kwa miaka mingi ijayo.
Kwa viongozi wa Mikoa, Wilaya na Jumuiya pamoja na Wajumbe, nirudie
kuwapongeza nyote kwa kuchaguliwa kwenu. Poleni kwa magumu ya uchaguzi
mliyokumbana nayo. Sasa uchaguzi umeisha, fanyeni kazi ya kujenga Chama.
Tibuni majeraha ya uchaguzi na hasa fanyeni kila muwezalo kuziba nyufa za
uchaguzi na migawanyiko miongoni mwa wanachama na viongozi. Kumbukeni wosia wa
Baba wa Taifa “Umoja ni Nguvu” Kumbukeni kaulimbiu ya Mkutano wetu huu
ya Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi! Kajengeni umoja katika maeneo
yenu ya uongozi kwa maslahi ya Chama chetu na nchi
yetu.
Hitimisho
Ndugu Wana-CCM;
Kwa kuhitimisha naomba nirudie kusema kuwa tumepata mafanikio
ya kutia moyo katika ujenzi wa Chama na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM
ya mwaka 2010 – 2015. Bado kazi kubwa iko mbele yetu kwa mambo yote hayo
mawili. Tunaitambua na tunayo mipango thabiti ya kutekeleza majukumu yetu.
Nina imani tutafanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kufikia malengo yetu.
Tukiendelea kushirikiana tutafika. Umoja ni Ushindi! Umoja na
Ushindi!
Baada ya hotuba yangu naomba sasa nitamke kuwa Mkutano Mkuu wa
Nane wa CCM umefunguliwa rasmi.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Kidumu Chama cha Mapinduzi
Asanteni sana kwa Kunisikiliza
Post a Comment