Israil inasema imerusha
kombora nchini Syria, baada ya kituo chake kimoja cha jeshi katika milima ya
Golan kupigwa mzinga, ambao Israil inafikiri ni kutoka jeshi la Syria katika
mapambano yake na wapiganaji.
Hii ni mara ya kwanza
kwa Israil kushambulia jeshi la Syria, tangu vita vya Mashariki ya Kati vya
mwaka wa 1973.Tukio hilo linakuja wakati makundi ya upinzani ya Syria,
yanayokutana Qatar, yametangaza kuwa yametia saini mkataba kimsingi kuwa na
shirika moja litalokuwa na serikali ya mpito, na kuwa ndilo linalopokea misaada
kwa ajili ya maeneo yanayodhibitiwa na wapiganaji.
Jeshi la Israil limesema
kombora moja lilirushwa dhidi ya Syria, baada ya kituo cha Israil kwenye milima
ya Golan kupigwa kwa mzinga.
Hakuna mtu
aliyeumia.
Mizinga kadha ya Syria
imeshawahi kuangukia upande wa Israil; na waIsraili walisema kuwa watajibu iwapo
itatokea tena.
Ni wazi kuwa vita vya
Syria vinafurika katika nchi za jirani.
Huku nyuma, upinzani
umetangaza kwenye mkutano wao mjini Doha, Qatar, kwamba umekubaliana kimsingi
kuunda uongozi wa mseto utaojumuisha makundi yote makubwa yalioko ndani ya Syria
na nje.
Mataifa ya magharibi
yameahidi kuwa yatatambua na kusaidia ushirika.
Post a Comment