Na Mwandishi Wetu.
MWANAMUZIKI nguli wa dansi Afrika, JB Mpiana
akiwa na Bendi yake ya Wenge BCBG anatarajiwa kuwasili nchini leo kwa ajili ya
maonesho matatu tofauti ikiwa ni pamoja na litalofanyika Ijumaa kwenye Viwanja
vya Leaders Club Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa
Kampuni ya QS J Mhonda, Joseph Mhonda alisema kuwa mwanamuziki huyo atawasili
nchini kwa kutumia ndege ya Shirikika la Ndege la Kenya.
Mhonda alisema kuwa katika Onesho hilo ambalo
litakuwa sambamba na uzinduzi wa Albamu ya Bendi ya Mashujaa ijulikanayo kama
Risasi Kidole.
Alisema kabla ya kufanyika kwa onesho la jijini
Dar es Salaam, JB Mpiana na Bendi nzima ya Wenge BCBG wataelekea MKoani Arusha
ambako watafanya onesho maalum siku ya Alhamis na Ijumaa kufanya mambo yake
katika viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam na baadaye Mwanza Desemba
2.
Mhonda alisema wakiwa MKoani Arusha watafanya
onesho hilo katika Ukumbi wa Tripple A na Mkoani Mwanza watakuwa kwenye Ukumbi
wa Villa Park.
Alisema kuwa kila kitu kimekamilika kuhusu ujio
wa mwanamuziki huyo, ambaye atakuja na Wanamuziki wake wote 25 ambao yupo nao
katika bendi hiyo.
Alisema wameona ni bora aanze mikoani na baadae
amalizie hapa na kuondoka zake katika ziara za nchi nyingine. Mhando alisema
mwanamuziki huyo atawasiri nchini na wanamuziki wake kutoa burudani ya aina
yake.
Wakati JB akiwasili leo na Bendi ya Mashujaa
chini ya Charles Gabriel ‘Chaz Baba’, wameingia kambini jana kwa ajili ya
maandalizi ya uzinduzi huo.
Akizungumzia kwa upande wao Chaz baba alisema
kuwa bendi hiyo ipo hapa hapa jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kufanya mazoezi
maalum ya uzinduzi.
Chaz Baba alisema wamejipanga kufanya uzinduzi wa
aina yake katika albam yao hiyo ya pili huku kwa upande wake ikiwa ya
kwanza.
"Leo (Jana) ndiyo tumeingia kambini kwa ajili ya
maandalizi ya uzinduzi wetu kubwa ni kwamba tumejipanga kufanya kweli katika
uzinduzi huo ambao kwa upande wangu ni wa kwanza katika bendi ya
Mashujaa"alisema Chalz Baba.
Alisema albamu yao, wanayozindua iitwayo Risasi
Kidole ina nyimbo sita, ambazo ni Risasi Kidole yenyewe utunzi wake Chaz Baba,
Ungenieleza utunzi wake Raja Ladha, Umeninyima utunzi wa Freddy Masimango,
Hukumu ya Mnafiki utunzi wake Jado FFU, Kwa Mkweo utunzi wake Baba Isaya na
Penzi la Mvutano, ambao umetungwa na Masoud Namba ya
Mwisho.
Chaz Baba alisema kama ilivyopangwa, mbali na JB
Mpiana, wanamuziki wengine watakaopamba uzinduzi huo ni MB Dogg, H Baba, Ney wa
Mitego na wengineo ambao watajulikana baadaye.
“Sisi kwa upande wetu tumejipanga vizuri kuwapa
watu burudani ambayo tunajua kwa muda mrefu wameikosa, Mashujaa tunakuja
kushujaa, ushujaa wa kuwaburudisha watu na kukata kabisa kiu yao,”alisema Chaz
Baba.
Alisema wanataka kufanya shoo ambayo hata JB
mwenyewe akiona atakubali kwamba Tanzania kuna bendi yenye ubora sawa na bendi
za kwao, Kongo, ambayo ni Mashujaa.“Hadi sasa wapenzi wa muziki hapa Dar es
Salaam ambao wamebahatika kuona shoo zetu wanakiri sisi ndio mabingwa wapya wa
muziki wa dansi Tanzania, sasa tunataka tumdhihirishie hilo na JB
Mpiana,”alisema Chaz Baba.
Post a Comment