Na Mwandishi
Wetu
RAIS wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Novemba 6, 2012, amelitumia
Kanisa Katoliki Tanzania salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha Askofu wa
Jimbo Katoliki la Shinyanga, Mhashamu Baba Askofu Aloysius Balina aliyefariki
dunia majira ya saa tano asubuhi leo kwenye Hospitali ya Rufaa ya Bugando,
Mwanza.
Katika salamu zake za
rambirambi kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania Mshahamu Baba Askofu
Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea kwa mshtuko mkubwa
taarifa za kifo cha Mhashamu Baba Askofu Aloysius Balina ambaye nimeambiwa
ameaga dunia asubuhi ya leo kwenye Hospitali ya Rufaa ya Buganda, Mwanza, kwa
ugonjwa wa kansa.”
Amesema Rais Kikwete
katika salamu zake hizo: “Mhashamu Baba Askofu Balina alikuwa kiongozi hodari na
mwadilifu ambaye siyo tu alichangia kipekee katika mwenendo mzuri wa kiroho wa
waumini wa Kanisa Katoliki bali pia katika maendeleo ya Watanzania wote kwa
jumla.”
“Kifo chake
kimetuondolea kiongozi mwema ambaye tutazikosa busara zake na uongozi wake.
Lakini napenda kukuhakishia Mshahamu Baba Askofu kuwa sisi ndani ya Serikali
tutaendelea kutambua na kuthamini mchango wa Askofu Balina alioutoa kwa nchi
yetu katika maisha yake,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Baba Askofu, nakuomba
upokee salamu za rambirambi za Serikali ninayoiongoza na zangu binafsi kufuatia
msiba huu mkubwa. Aidha, kupitia kwako, naomba uwafikishie salamu zangu viongozi
na waumini wote wa Kanisa Katoliki kwa kuondokewa na kiongozi na muumini
mwenzao. Naungana nanyi kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweka pema
peponi roho ya Marehemu. Amen.”
Post a Comment