Taarifa ya Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli
(CCM), kwa vyombo vya habari jana ilieleza kwamba kutokana na afya yake kuwa
nzuri atarejea nchini kutoka Munich, Ujerumani hivi karibuni.
“Namshukuru Mungu siha yangu ni imara na kwamba
madaktari walionifanyia uchunguzi wamejiridhisha pasi na shaka kwamba afya yangu
ni njema…nimeendelea kupata maendeleo na matibabu mazuri katika jicho langu moja
ambalo nilifanyiwa upasuaji miaka miwili iliyopita hapa hapa, Ujerumani,”
alisema katika taarifa hiyo.
Alisema “natarajia kurejea nyumbani wakati wowote
kuanzia sasa ili kuja kuungana na Watanzania wenzangu katika kulijenga taifa
letu.”
Alisema amekuwa jijini Munich kwa wiki nzima sasa
na kwamba amekuwa akifuatilia kwa karibu taarifa mbalimbali za kisiasa ndani ya
Chama Cha Mapinduzi na katika taifa kwa ujumla.
“Nikiwa mwana CCM na Mtanzania nasononeshwa sana
na taarifa za kukithiri kwa vitendo vya rushwa ndani ya chama chetu, serikalini
na katika taasisi mbalimbali,” alisema.
Alisema rushwa ni tatizo na kansa ambayo inapaswa
kutafutiwa ufumbuzi wa kimfumo badala ya kuendelea kufikiri kwamba linaweza
kumalizwa kwa njia ya kulalamika, kulaumiana na kupakana matope.
Alisema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), inatakiwa kupewa meno na kuimarishwa zaidi katika kukabiliana na
vitendo hivyo na kwamba rushwa inahitaji mikakati mipana zaidi na mijadala wa
kitaifa na ya kina katika kukabiliana nayo.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment