WAKATI mkutano wa Uchaguzi Mkuu wa CCM, unaanza Jumapili mjini hapa, joto limezidi kupanda kwa vigogo kadhaa wakiwamo mawaziri wanaowania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (Nec), kupitia kapu.
Habari zilizopatikana jana zinaeleza kuwa, hivi sasa wagombea hao wanahaha kusaka kura wengi wao wakipita kwa baadhi ya wajumbe wa mkutano huo katika maeneo mbalimbali wakiwamo wabunge ambao ni wajumbe wa mkutano huo kwa mujibu wa katiba ya chama hicho kujinadi.
Baadhi ya mawaziri wanaowania nafasi hiyo, viti vyao katika Bunge linaloendelea mjini hapa vimekuwa moto kwani hawahudhurii vikao inavyopaswa ikielezwa kwamba wapo katika harakati za kusaka ushindi.
Vita kubwa inaonekana kuwa katika nafasi 10 za ujumbe wa Nec kwani mawaziri sita ni miongoni mwa wanachama 31 wa Bara watakaopambana kupata nafasi hizo.
Hali ni hivyo pia kwa upande wa Zanzibar kwani kati ya wanachama 28 wanaowania nafasi 10 za Nec visiwani humo, wapo mawaziri wanne.
Mbali na mawaziri sita, nafasi 10 za Tanzania Bara pia zinawaniwa na wabunge watatu, mkuu wa wilaya mmoja na vigogo wawili wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho.
Mawaziri watakaochuana Bara ni Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Dk David Mathayo David; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira; Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Pia wamo Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama na Mbunge wa Iramba Magharibi na Katibu wa Fedha na Uchumi wa CCM, Mwigulu Nchemba. Wote hao ni wajumbe wa Kamati Kuu.
Wengine ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Shy-Rose Bhanji; Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Martine Shigela na Mbunge wa Nkenge, Assumpter Mshama.
Pia wapo Otieno Peter Baraka, Twalhata Ally Kakurwa, Godwin Kunambi, Innocent Nsena, Richard Tambwe, Anna Magowa, Christopher Mullemwah, Salehe Mhando, Fadhili Nkurlu, Tumsifu Mwasamale, William Malecela, Rashid Kakozi, Dk Luteni Kanali Kesi Mtambo, Nicholaus Haule na Nussura Nzowa.
Wengine ni Hadija Faraji, Dk Hussein Hassan na Mwanamanga Mwaduga, Mbunge wa zamani wa Muleba Kaskazini, Ruth Msafiri na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Jackson Msome.
Kwa upande wa Zanzibar, wamo mawaziri wanne akiwamo Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi; Mbunge wa Uzini, Mohamed Seif Khatib; Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi; Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Abdallah Juma Sadallah na Waziri wa Fedha, Omar Yussuf Mzee.
Wengine ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Wagombea wengine ni Kidawa Hamid Saleh, Abdisalaam Issa Khatib, Khadija Hassan Aboud, Abdalla Ali Hassan, Mohamed Ahmada Salum, Abdulhakim Chasama, Ali Mohamed Ali, Haji Makame Ali, Ibrahim Khamis Fataki, Moza Jaku Hassan, Nassir Ali Juma, Jecha Thabit Kombo, Khamis Mbeto Khamis, Mohamed Hassan Moyo, Bhaguanji Mansuria, Moudline Castico, Yakoub Khalfan Shaha, Rose Mihambo, Ali Omar Mrisho na Mariam Omar Ali.
Duru za siasa mjini hapa zinasema, wajumbe wa Kamati Kuu na wale wa Sekretarieti ambao wanawania ujumbe wa Nec, huenda wakapata kura nyingi kutokana na kuwatumia makatibu wa wilaya na mikoa kuwaombea kura.
Hata hivyo, makundi ndani ya chama hicho huenda yakawapa wakati mgumu baadhi ya mawaziri wanaogombea ikielezwa kwamba huenda baadhi ya wajumbe wakapiga kura kutokana na makundi wanayoyashabikia.
Post a Comment