Michoro ya ujenzi wa
Kampasi ya Mloganzila iliyo kijijini Kwembe katikati ya Wilaya za Kisarawe Mkoa
wa Pwani na Kinondoni Mkoa wa Dar es salaam. Hii ni sehemu ya Chuo cha Afya na
Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) inayojengwa kwenye eneo la ekari 3800 kwa
ajili ya kutolea mafunzo kwa wanafunzi wa udaktari na huduma za Afya wapatao
15,000 kwa mwaka, na pia itakua sehemu ya kutolea matibabu ya maradhi yote makuu
na ya kawaida nchini. Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi
Shirikishi Muhimbili, ujenzi wa Hospitali hii, ambayo pesa ya ujenzi wake
imeshapatikana, unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Januari, 2013 na
unatarajiwa kukamilika miaka miwili baada ya ujenzi kuanza. Kwa maneno mengine
Kampasi ya Muhimbili ya Mloganzila inategemewa kuanza kazi mwanzoni mwa mwaka
2015. Tayari wataalamu na wafanyakazi wanaotarajiwa kufanya kazi katika kampasi
ya Mloganzila wameshaanza mafunzo ndani na nje ya nchi. Mara hospitali hiyo
kubwa na ya kisasa itakapokamilika itakua na uwezo wa vitanda vya kulaza
wagonjwa mia sita (600). Sambamba na kampasi ya MUHAS ya Mloganzila pia ujenzi
wa Kampasi ya Afya ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) umeshaanza na kufikia hatua
ya juu na ambapo pia hospitali hiyo inatarajiwa kuanza shughuli zake rasmi mwaka
2015. Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mfuko wa Afya ya Jamii (National Health
Insurance Fund) NHIF Bw. Emmanuel Humba mchakato wa kufanikisha uanzishaji wa
Chuo Hospitali hiyo vimeshaanza ambapo baadhi ya wataalamu wakiwemo Madaktari na
watumishi wengine wako nchini na nje ya nchi kwa ajili ya masomo na mafunzo
mbalimbali. Chuo hicho kinatarajia kuwa na vifaa vya kisasa vya tiba
vinavyokidhi mahitaji ya Afya na Elimu ya Udaktari wa kiwango cha Kimataifa,
ikiwa ni mikakati kabambe ya serikali ya awamu ya nne katika kuhakikisha nchi
ina wataalamu wengi na huduma za kisasa za afya ili kuondokana na adha ya
kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu. Kwa sasa MUHAS inachukua
takriban wanafunzi 2442 wa udaktari na huduma za afya kwa mwaka. Hivyo ujio wa
kampasi ya Afya Mloganzila na Kampasi ya afya ya UDOM utaharakisha mpango wa
serikali wa kupunguza wastani wa wagonjwa kwa daktari mmoja kwa kiwango kikubwa.
Hivi sasa wastani ni daktari mmoja anahudumia wagonjwa 30,000.
Na Michuzi
Na Michuzi
Post a Comment