Akiahirisha mkutano huo
hadi desemba 17, 2012, kaimu mkuu wilaya Singida ambaye pia ni mkuu wa wilaya
mpya ya Ikungi, Manju Msambya alisema utafiti uliofanywa na shirika la “SIKIKA”,
la jijini Dar es Salaam, haujakamilika kutokana na halmashauri kutoipitia kwanza
taarifa hiyo, ndipo iwasilishwe.
Hali ya hewa ilianza
kuchafuka mapema saa nne asubuhi, baada ya watumishi wa shirika la SIKIKA kugawa
taarifa kwa wajumbe wa mkutano huo, lakini ikionesha udhaifu mkubwa wa
utekelezaji wa miradi ya halmashauri ya wilaya Singida, katika sekta ya
afya.
Baada ya wajumbe
(madiwani) na waalikwa, wakiwemo viongozi wa madhehebu ya dini kuipitia taarifa
hiyo kabla ya kikao kufunguliwa rasmi, ndipo manung’uniko yalianza, huku baadhi
ya madiwani wakidai miradi mingi kwenye maeneo yao
imechakachuliwa.
Hali hiyo ililazimu
wataalamu kutoka ukumbini kwenda kufanya kikao cha dharula kilichogharimu zaidi
ya saa tatu, chini ya mkuu wa wilaya Ikungi, Manju Msambya na mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri hiyo, Illuminata Mwenda, na kuchukua uamuzi wa
kuahirisha mkutano huo, hadi Desemba 17, mwaka huu.
Akitangaza uamuzi wa
kuahirisha, Msambya alisema baada ya kupitia taarifa hiyo, wamebaini kuna baadhi
ya vitu muhimu havikuorodheshwa, hivyo halmashauri nayo inapaswa kuipitia kabla
ya kuwasilishwa kwa wajumbe.
“Wenzetu wa Sikika
tumechukua muda mrefu sana kuwashawishi kuahirisha, kwa sababu wana maeneo mengi
ya kufanya shughuli hizi..sasa nikuombeni radhi na kuahirisha hiki kikao,
muungwana anapoomba kwa muungwana mwenzake, husikilizwa…kuna mambo
yamepungua,”alisema Msambya.
Msambya alisema kuna
baadhi ya vipengele havijafanyiwa kazi vizuri, na kukosea ni jambo la kawaida
kwa kila binadamu.
Hata hivyo kauli hiyo
iliamsha hisia kali kwa baadhi ya madiwani, akiwemo Teddy Augustino Daghau, kata
Ikungi (CHADEMA),aliyedai mkutano huo umelazimika kuahirishwa kutokana na
taarifa ya SIKIKA kukosoa utekelezaji wa miradi mingi sekta ya afya, wilaya ya
Singida.
Teddy alisikitishwa na
hali hiyo iliyojitokeza, na kushutumu wazi ofisi ya mkuu wa wilaya na mkurugezi
mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, hali inayotoa viaashiria vya ufujaji
mkubwa wa fedha za umma sekta ya afya, na ameiomba serikali kuingilia kati na
kufuatilia kwa kina sakata hilo.
Akiongea na waandishi wa
habari nje ya ukumbi baada ya mkutano huo kuahirishwa, mratibu wa shughuli za
SIKIKA, Mahindi Zakayo kutoka Dar es Salaam alisema kazi ya ufuatiliaji sekta ya
afya wilayani Singida, ilianza wiki nne zilizopita na kushirikisha wadau wote wa
afya, wakiwemo pia madiwani.
Alisema madiwani hao
walielekezwa mifumo mbalimbali jinsi inavyofanya kazi katika halmashauri yao,
kwa lengo la kufanikisha uwajibikaji, usimamizi wa raslimali za halmashauri,
utendaji na ufuatiliaji.
“Kimsingi timu imefanya
kazi zake, imeangalia mipango ya halmashauri, mgawanyo wa raslimali, matumizi na
utendaji….lakini pia timu zinazofuatilia utendaji kuona je zote zinafanya kazi
ya kuhudumia jamii?, sasa kwa bahati mbaya mrejesho siku hii ya leo haukuweza
kufanyika,”alieleza kwa masikitiko Mahindi.
Alisema binafsi hakuona
tatizo lolote kubwa, kwani kimsingi wajumbe wailikuwa wapokee taarifa ya kazi
nzima iliyofanyika katika hatua tano ila halmashauri wamedai hawajazipitia hoja,
badala ya kupokea na kuzinfanyia kazi baadaye, hapo ndipo tofauti
iliyotokea.
Mahindi alisema haoni
tatizo lolote lililojitokeza hadi mrejesho huo usifanyike, badala ya kukubali
kwanza hoja na baadaye ndipo zifanyiwe kazi
|
Post a Comment