Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Luteni Yusuf Rajab
Makamba ameipongeza Yanga kwa kubadili kocha wao haraka mwanzoni mwa msimu kwani
hatua hiyo ndiyo inayowsaidia kuwaburuza mahasimju wao Simba katika msimamo wa
Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Akizungumza leo
jioni wakati akimpigia debe rais Jakaya Kikwete mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu
wa CCM kumchagua kuwa mwenyekiti wa chama hicho kwa miaka mingine mitano,
Makamba alisema kuwa Yanga, timu asiyoishabikia kwa vile yeye ni mwanachama wa
Simba na pia Coastal Union anapokuwa kwao jijini Tanga, ilifanya vizuri kwa
kusajili wachezaji wenye sifa; lakini 'ikachemka' kwa kuteua kocha asiyewafaa
(Tom Saintfiet) na matokeo yake wakajikuta wakipata matokeo mabovu mwanzoni mwa
msimu.
"Yanga chini ya mwenyekiti ambaye ni rafiki
yangu Yusuf Manji, wakawa wajanja kwa kujua kuwa kocha hawafai na wakambadili
mara moja... na sasa wanapata matokeo mazuri na kuiburuza Simba," alisema
Makamba na kushangiliwa na wajumbe wa NEC wa CCM.
Makamba alitoa mfano huo wakati aklielezea
umuhimu wa kocha katika timu ya soka; akilinganisha ubora wa kiwango cha juu wa
'kocha' Jakaya Kikwete kwa chama chao cha CCM, akitaka wajumbe wampigie kura
nyingi za ndiyo ili aendelee kukiongoza chama chao kwa mafanikio
makubwa.
Yanga walianza vibaya mwanzoni mwa msimu kwa
kushikiliwa kwa sare ya 0-0 dhidi ya Prisons ya Mbeya na baadaye wakala kipigo
cha 3-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar na baada ya hapo, uongozi ukamtimua kocha kutoka
Ubelgiji, Tom Saintfiet na nafasi yake wakampa Mholanzi Brandts ambaye sasa
anaendelea kuipa mafanikio timu hiyo inayoongoza katika msimamo wa Ligi Kuu ya
Tanzania Bara kwa kuwa na pointi 29 na kufuatiwa na Azam yenye pointi 24 huku
mahasimu wao wa jadi, Simba wakishika nafasi ya tatu kwa kubaki na pointi zao 23
baada ya kumalizika kwa mechi zote 13 za mzunguko wa kwanza wa ligi
hiyo.
Post a Comment