RAIS wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete Novemba 4, 2012, ameweka jiwe la
msingi kwenye mradi mkubwa wa maji unaolenga kumaliza tatizo la maji mjini
Singida. Rais Kikwete ameweka jiwe la msingi katika sherehe ya kufana
iliyofanyika katika eneo la Mradi la Mwankoko, nje ya mji wa Singida, mara baada
ya kuwasili Mkoani Singida kuanza ziara ya siku mbili kukagua na kuzindua miradi
ya maendeleo akitokea Mkoani Manyara ambako alifanya shughuli hizo hizo kwa siku
mbili pia.
Mradi huo ulioanza
kujengwa Novemba 2, mwaka 2009, umekamilika kwa kiasi cha asilimia 80 na
unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 31, mwaka huu wa 2012. Kwa mujibu wa
maelezo ya wasimamizi wa Mradi wa SUWASA, Mradi huo unagharimu dola za Marekani
milioni 19.7 sawa na Sh.bilioni 31.126. Kati ya fedha hizo, Serikali ya Tanzania
imetoa dola za Marekani milioni 10.42 sawa na Sh. 16, 463,600,000, Benki ya
Maendeleo ya Nchi za Kiarabu (BADEA) imetoa dola za Marekani milioni 4.57 sawa
na Sh. 7,220,600,000 na Mfuko wa OPEC kwa Maendeleo ya Kimataifa wa OFID umetoa
dola za Marekani milioni 4.7 sawa na Sh. 7,426,000,000.
Mradi huo unaotekelezwa
na Kampuni ya Spencon Services Limited unatarajiwa kutoa lita 17,208,000 kwa
siku kutokana na visiwa viwili vilivyoko Mwankoko vyenye uwezo wa kuzalisha lita
292,000 kwa saa na visima viwili vilivyoko eneo la Irao vyenye uwezo wa
kuzalisha tani 425,000. Mradi huo unatarajiwa kutoa huduma kwa jumla ya wateja
3,500 kati yao 2,500 katika awamu ya kwanza na wengine 1,000 katika awamu ya
pili.
Mradi huo utaongeza
upatikanaji wa maji kwa karibu kiasi cha asilimia 100 kwa wakazi wa mji wa
Singida na utaongeza muda wa kupatikana maji kutoka saa tano za sasa kwa siku
hadi saa 24 kwa siku.
Post a Comment