Meneja wa shirika la SEMA Ivo Manyaku akitoa nasaha zake kwenye mkutano wa wadau wa afya na usafi wa mazingira wa wilaya ya Nzega.
Mwenyekiti wa halamshauri ya wilaya ya Nzega mkoani Tabora, Patrick Mbozu akifungua mkutano wa siku moja uliohudhuriwa na wadau wa afya na usafi wa mazingira wa wilaya ya Nzega.
Mkuu wa afya na usafi wa mazingira makao makuu Dar-es-salaam, Marco Msambazi akitoa nasaha zake kwenye mkutano wa wadau wa afya na usafi wa mazingira uliofanyika Nzega mjini.
Mratibu wa mradi wa afya na usafi wa mazingira wa shirika la WaterAid makao makuu Simon Chiwanga akitoa taarifa yake kwenye mkutano wa wadau wa afya na usafi wa mazingira uliofanyika mjini Nzega.
Baadhi ya wadau wa afya na usafi wa mazingira wilaya ya Nzega mkoa wa Tabora wakifuatilia kwa makini mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya wilaya ya Nzega.
Baadhi ya sehemu ya mji wa Nzega mkoani Tabora.(Picha zote na Nathaniel Limu).
Imeelezwa kwamba kati ya kata 37 za wilaya ya Nzega mkoani Tabora ni kata saba tu ndizo zenye wataalam wa afya kitendo kinachochangia kuzorotesha utoaji wa huduma.
Akitoa taarifa yake ya hali ya afya na usafi wa mazingira mbele ya mkutano wa ushawishi ulioandaliwa na kufadhiliwa na shirika la SEMA, Kaimu Afisa Afya katika halmashauri ya wilaya ya Nzega Majile Sayenda, amesema pamoja na uhaba huo mkubwa wa watumishi, wataalam hao saba waliopo, pia hawana usafiri kitendo kinachochangia washindwe kuwafikia wananchi mapema hasa wenye matatizo ya kiafya.
Sayenda amesema wakati umefika sasa kwa serikali kuangalia uwezekano wa kuondoa tatizo hilo la uhaba wa wataalam, ili wananchi waweze kupata huduma ya afya kwa urahisi na kwa wakati.
Ametaja baadhi ya changamoto zingine kuwa ni pamoja na mila potofu ndani ya jamii kuhusu matumizi ya vyoo ikiwemo ya baadhi ya wakazi kutokuwa tayari kuchangia choo na wakwe.
Awali akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Nzega Patrick Mbozu, amewataka wataalam wa afya kuhakikisha kila kaya inatunza mazingira yake kikamilifu, ili pamoja na mambo mengine, kuondoa uwezekano wa kutokea kwa magonjwa ya mlipuko.
Alisema zoezi linaloendelea hivi sasa la kuhimiza ujenzi na matumizi sahihi ya vyoo, liende sambamba na kuhimiza usafi wa mazingira katika kaya zote za wilaya ya Nzega.
Kwa upande wake Meneja wa Shirika la SEMA lenye makazi yake mjini Singida Ivo Manyaku, amesema kuwa madhumuni ya mkutano huo ni kutoa ushawishi na kubadilishana uzoefu kwa wadau wa usafi wa mazingira.
Meneja huyo amesema “tumeanzisha mkakati ambao unajulikana kwa jina la ‘mtumba’ wenye lengo la kuhamasisha ujenzi wa vyoo bora pamoja na matumizi yake”
“Katika mkakati huu, tunaunda vikundi vya ujenzi wa vyoo bora kwa lengo, ili baada ya kuwahimiza wananchi kuwa na vyoo bora, basi wapate kwa urahisi huduma ya kujengewa”. .
Kwa mujibu wa Meneja Ivo mkakati huo unatekelezwa katika wilaya ya Nzega Iramba na Mbulu na umeonyesha matunda mazuri kwa muda mfupi.