SHIRIKA lisilo la
kiserikali linaloshughulika na kuinua hali ya maisha ya masuala ya
kielimu,kiuchumi na kiafya la ‘Community Educational Foundation’ (CEF)
limeanzisha mpango wa kupunguza tatizo la ajira kwa vijana unaojulikana kama
‘kazi nje nje’
Akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa CEF John Shusho, alisema programu ya
kazi nje nje yenye lengo la kuelimisha vijana juu ya stadi za ujasiriamali,
imeasisiwa na Shirika la Kazi Duniani(ILO) na hapa nchini inafanya kazi kwa
ushirikiano wa karibu na Wizara ya Kazi na Maendeleo ya Vijana pamoja na Wizara
ya Utumishi.
Alisema mpango huo wa
Kimataifa utatekelezwa hadi Mwaka 2014 katika mikoa ya Tanga, Tabora,
Singida, Mwanza, Mbeya, Pwani, Lindi na Mtwara, ambapo pia unaendeshwa katika
nchi za Kenya na Uganda.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi
huyo, stadi hizo ni kuwajengea uwezo wa kijasiriamali, kubuni wazo la Biashara,
kuandaa andiko na kuanzisha biashara zitakazowawezesha kukabiliana na hali ngumu
ya maisha.
Shusho alisema makundi
lengwa katika program hiyo ni pamoja na vijana wasio na ajira, wafanyabiashara
katika sekta zisizo rasmi na vikundi vya uzalishaji mali vilivyopo katika maeneo
ya mikoa hiyo.
Alitanabaisha kuwa moja ya
mambo yanayopewa kipaumbele na CEF ni kutoa changamoto kwa walengwa kutobweteka
na kuwaachia wageni kuendelea kutumia fursa nyingi za kazi zilizojaa kwenye
maeneo yao husika na nchini kwa ujumla.
“Tayari ILO imeshatoa mafunzo
kwa wakufunzi kutoka CEF ambao jukumu lao litakuwa ni kuibua na kuchechemua
vipaji vya kazi miongoni mwa vijana ambao wengi wao wamekaa vijiweni bila kujua
la kufanya” alisema Shusho.
Kwa mujibu wa Shusho,
rekodi za Shirika la Taifa la Twakwimu (NBS), zinaonesha takwimu za mwaka 2006,
kiwango cha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana kilikuwa ni wastani wa asilimia
13.4 kwa vijana, idadi aliyosema ni kubwa ukilinganisha na idadi ya vijana
iliyokuwepo wakati huo.


Post a Comment