Ibrahim Haruna Lipumba -Mwenyekiti Chama Cha
Wananchi CUF
----
Siku
ya Alhamis nikielekea Muhimbili kumpeleka shangazi yangu hospitali
nilipata taarifa kuwa Imam wa msikiti wa Masjid Haq (ulioko jirani na Afisi Kuu
ya CUF na ambapo nasali sala ya Ijumaa nikiwa Afisi Kuu) na watu wengine watatu
akiwemo Sheikh Ramadhan S. Sanze (ambaye namfahamu kwa muda mrefu). Sadik Gogo
na Mzee Abdillah wamekamatwa na wamefikishwa kituo cha polisi cha kati (Central
Police Station). Nilistushwa na kamata kamata hii na nikahofia kuwa inaweza
kuongeza jazba miongoni mwa waumini wa Kiislam. Baada ya shangazi kupata tiba
katika hospitali ya Muhimbili nilimrudisha nyumbani na nikampigia simu
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na mahusiano ya umma, Abdul Kambaya, tukutane
kituo cha polisi cha kati kuulizia sababu za kukamatwa Imam wa Masjid Haq na
wenzake watatu na kama tunaweza kuwawekea dhamana.
Tulipofika kituo cha polisi tulibaini kuwa
Imam wa Msikiti wa Masjid Haq hajakamatwa bali kuna muumini mwingine kwa jina la
Mkadam Swalehe ndiye aliyekamatwa. Tulizungumza na RPC Kova na RCO Msangi kuhusu
kuachiliwa kwa wale waliokamatwa. Tukafahamishwa kuwa itabidi wafanyiwe
mahojiano na baadaye wataachiliwa isipokuwa Mkadam Swalehe ambaye ana faili
jingine pale polisi linaloendelea kufanyiwa upelelezi. Tulifahamishwa kuwa
nitume mtu saa 10:30 jioni ili aweze kufuatilia utaratibu wa kuachiliwa
watuhumiwa watatu akiwemo Sheikh Ramadhan Sanze, Sadik Gogo na Mzee
Abdillah.
Nilishauriana na Wakurugenzi wa CUF walioko
Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu, Julius Mtatiro hatua za kuchukua. Taarifa za
kukamatwa Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake zilikuwa zinaenea na kupandisha jazba
ya Waislam wengi. Tulipata wasiwasi kuwa jazba hii inaweza kupelekea Waislam
wengi kuandamana baada ya sala ya Ijumaa. Ikiwa Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake
wataachiwa na Waislam wakapata taarifa hiyo inaweza kusaidia kupunguza jazba na
watu wasishiriki maandamano baada ya sala ya Ijumaa.
Nilimpa jukum Abdul Kambaya afuatilie
Central PoliceStation, suala la kuachiliwa Sheikh Sanze na wenzake.
Niliwasiliana naye kwa simu na kuzungumza na RCO na nikaamini kuwa Sheikh
Ramadhan Sanze, Sadik Gogo na Mzee Abdillah wataachiwa baada ya kukamilisha
mahojiano. Ilikuwa inakaribia saa 12 jioni. Muda wa kuitisha Press Conference
haukuwepo.
Tukakubaliana Naibu Katibu Mkuu awasiliane
na wahariri wa habari wa vituo vya televisheni Channel 10, TBC1, Star TV,
Mlimani TV na ITV ili niweze kutoa taarifa ya kuwasihi Waislam warudi majumbani
na kwenye shughuli zao baada ya sala ya Ijumaa.
Niliweza kufanya mahojiano na Channel 10,
TBC1, na ITV. Kwa bahati mbaya Camera person wa Star TV alikuwa kwenye shughuli
nyingine na kwa hiyo sikuweza kufanya mahojiano na Star TV. Vilevile wapiga
picha wa Mlimani TV hawakuwepo kwenye studio. Pia nilipata bahati ya kuzungumza
na Radio Iman inayosikilizwa na Waislam wengi na kueleza maoni yangu kuwa
Waislam wasiandamane baada ya sala ya Ijumaa.
Baada
ya kutoa taarifa kwenye vituo vitatu vya televisheni na Radio Iman kuwa Sheikh
Ramadhan Sanze na wenzake wataachiliwa na kuwasihi Waislam wasishiriki
maandamano baada ya sala ya Ijumaa nilimpigia simu Abdul Kambaya kuulizia kama
naweza kuzungumza na Sheikh Ramadhan Sanze. Kambaya akanieleza mambo
yamebadilika na hawajaachiwa. Niliwasiliana na RCO na nikabaini kuwa suala hilo
haliko tena chini ya uamuzi wake na litakamilishwa siku
ijayo.
Usiku
wa alhamisi kuamkia Ijumaa nilijaribu kuwasiliana na Rais Kikwete kupitia
wasaidizi wake ili nimfahamishe mantiki na sababu ya hatua nilizochukua na
atumie uwezo wake alionao Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake waachiliwe. Kwa
bahati msaidizi mmoja alipata ujumbe wangu wa simu na akanipigia simu saa 6:50
usiku na kunifahamisha atajitahidi kuufikisha ujumbe wangu kwa Mhe. Rais ili
nipate kuongea naye kuhusu jamaa wanaoshikiliwa na polisi waachiwe ili kupunguza
jazba na kuepusha shari. Niliyezungumza naye alikuwa Dodoma na Rais alikuwa
Arusha na ratiba yake ilikuwa imebana sana na kwa hiyo hakuweza kupata fursa ya
kunipigia simu siku hiyo ya Ijumaa.
Siku
ya Ijumaa Abdul Kambaya aliendelea kufuatilia kuachiwa kwa Sheikh Ramadhan Sanze
na wenzake Central Police Station. Nami katika kuhangaika ili waliokamatwa
waachiliwe nilipata fursa ya kuzungumza na IGP na kumfahamisha sababu ya juhudi
nilizochukua na mategemeo yangu kuwa Sheikh Sanze na wenzake wangeachiwa.
Ninakiri kuwa katika mazungumzo ya simu, IGP Mwema alikuwa msikivu na mkarimu
sana katika kauli yake. Alinishukuru kwa kauli niliyoitoa katika vituo vya
televisheni na kuwa atafuatilia suala nililomueleza. Hatimaye Sheikh Ramadhan
Sanze na wenzake waliachiwa.
Naamini kama Sheikh Ramadhan Sanze na
wenzake wangeachiwa ingesaidia sana kupunguza jazba. Hata hivyo Waislam wengi na
wananchi wengine kwa ujumla walipokea vizuri wito wangu na hawakushiriki katika
maandamano. Baadhi wamenikosoa na kushauri kuwa ilifaa nisubiri mpaka baada ya
maandamano kufanyika na kama patatokea majeruhi na vifo ndipo nitoe tamko la
kulaani vitendo vya polisi na serikali.
Katika mitandao ya kijamii wengine
wamekejeli juhudi zangu. Nilikubali kushiriki katika kipindi cha Makutano show
kinachoendeshwa na Bi. Fina ambapo hupata maswali toka Jamii Forum. Moja ya
swali lililotolewa ni “Muulize very very solid, kuna agenda gani kati ya Cuf na
uislam? mtaani leo wanasema kauli ya Lipumba ya jana kusitisha maandamano
wameitii, na ukiangalia mikutano yake pale jangwani utafikiri kuna mawaidha ni
balaghashia na baibui.” Fina hakupata muda wa kuniuliza swali hili. Jibu lake ni
la wazi.
CUF
inasimamia Haki Sawa kwa Wananchi Wote. Kuna Watanzania wengi ambao ni Waislam
na wao pia wanastahiki kutendewa haki katika nchi yao. Kuhusu balaghashia na
baibui ni vyema vijana wakatazama picha za umati wa watu uliokuwa unahutubiwa na
Mwalimu Nyerere wakati wa kupigania uhuru wa nchi hii. Picha hizo pia
zinaonyesha waliokuwa wakipigania uhuru wengi walivaa balaghashia na baibui hata
Mwalimu Nyerere alipewa zawadi nyingi za balaghashia na akaamua
kuzivaa.
Kushamiri kwa demokrasia ya kweli msingi
wake mkubwa ni amani na utulivu. Amani ya kweli haipatikani bila kuwepo haki.
Kesi ya Sheikh Ponda msingi wake na madai ya kiwanja. Ki msingi kesi ya madai ya
kusuluhishwa na Mahakama ya ardhi. Sheikh Ponda ana haki ya msingi ya kupewa
dhamana hata kama kauli zake haziifurahishi
serikali.
Nasikitika sana katika kipindi hiki tete,
viongozi wa serikali wameshindwa kuchukua juhudi za makusudi kuzungumza na
Maimam wa misikiti na viongozi wa asasi za Kiislam kupunguza jazba. Badala yake
wameachia kauli za vitisho vya Kamanda Kova ndiyo viwe mawasiliano kati ya
serikali na Waislam. Ni vyema serikali ikatumia busara na kuwasiliana na Maimamu
wa misikiti na viongozi wa asasi za Kiislam kuelewa hoja na malalamiko
yao.
Hatimaye nimepata fursa ya kuzungumza na
Mheshimiwa Rais leo asubuhi na nikamueleza juhudi nilizozichukua kuweza
kupunguza jazba na kuwaomba Waislam wasishiriki kwenye maandamano baada ya sala
ya Ijumaa. Ni wazi hali hii ya mtafaruku ndani ya jamii inamsononesha sana
Mheshimiwa Rais na ninaamini atajitahidi kwa uwezo wake wote kutafuta
suluhisho.
Katika kutafuta suluhu ya mtafaruku huu
nitaendelea na jitihada za kutafuta fursa niweze kubadilishana mawazo na Rais
Kikwete. Nitazungumza na viongozi wa asasi za Kiislam. Nitazungumza na viongozi
wa Makanisa ya Kikristo. Madhumuni ya mazungumzo yangu ni kuwafahamisha mantiki
ya juhudi nilizofanya na kushauriana misingi muhimu ya Waumini wote kuheshimiana
na kuvumiliana ili tujenge Tanzania yenye haki sawa kwa
wote.
Ibrahim Haruna
Lipumba
Mwenyekiti
Novemba 4 2012
Mwenyekiti
Novemba 4 2012
Post a Comment