Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

TBS YAJA NA SHERIA MPYA



SHERIA zimetungwa na binadamu ili kuhakikisha dunia inakuwa mahala salama pa kuishi.
Hivyo ili raia aweze kuyatii mamlaka yaliyoko juu yake ni lazima nchi iwe na sheria zake ambazo ni lazima kila raia azifuate na akishindwa adhabu kali hutolewa kwa muhusika.
Katika nchi kuna sheria nyingi tu kulingana na mazingira halisi, zipo sheria zinazofanana kwa nchi zima na zipo sheria zinazotungwa na mabaraza ya madiwani wa maeneo husika ukiacha Bunge ambalo hutunga sheria kwa watu wote wa nchi.
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) likiwa ni chombo cha umma nalo limekuja na sheria inayolenga kuwalinda raia dhidi ya bidhaa feki zisizo na ubora wa viwango uliothibitishwa.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Leandri Kinabo, anasema ili kuhakikisha yote hayo yanafanyika sheria na kanuni mbalimbali zimetungwa lengo likiwa ni kuwabana wazalishaji au wafanyabiashara wasio waaminifu.
Anasema shirika limekuwa na mikakati ya kuwabana wafanyabiashara wa aina hiyo, hasa kwa kuanza kuitumia sheria mpya ya mwaka 2009 yenye meno ya kuwabana wazalishaji na wafanyabishara wanaovunja sheria kwa makusudi kwa lengo la kupata faida kubwa.
“Ninaposema ina meno maana yake ni kwamba sheria hiyo sasa itawabana wale wote wanaokiuka taratibu za kutumia alama ya ubora ya Tbs,”anasema.
Kinabo anasema wengine ambao sheria hiyo itawabana ni wale wanaoagiza bidhaa hafifu na wasiofuata taratibu walizopewa na shirika.
Kabla ya sheria hiyo anasema sheria zilizotangulia zilikuwa ni dhaifu na kuweza kuwabana watu wa namna hiyo na hivyo kuutumia udhaifu huo kwa maslahi yao.
“Kwa sasa mtu anapovunja sheria zetu atakwenda jela miaka miwili au atalipa faini ya kati ya sh milioni 50 hadi milioni 100,” anafafanua.
Naye Mwanasheria wa Tbs Bitaho Marco anasema hatua kali itachukuliwa kwa wale wataobainika kuvunja sheria kwa lengo la kujipatia faida zaidi.
“Kama anavyoeleza Kaimu Mkurugenzi ni kweli tutakuwa wakali kwa wanaovunja sheria na kwamba ni vema wadau wote tukazitekeleza sheria zetu,” anasisitiza Bitaho.
Kinabo anasema baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakitumia njia za kughushi na hatimaye kuingiza bidhaa hafifu nchini kitu ambacho kimesababisha soko letu kuwa na baadhi ya bidhaa zisizokidhi viwango vya ubora vilivyowekwa.
“Wengine wamekuwa wakigushi sahihi za maofisa wetu ili kuonesha bidhaa zao zina viwango, wengine wamekuwa wakigushi alama yetu ya ubora ili kuudanganya umma kwamba tumewathibitisha sasa watu kama hao hivi sasa sheria itawabana, zamani walicheza cheza kwa kuwa walijua faini ni sh 1500, sasa hali ni tofauti,” anasema kaimu mkurugenzi huyo.
Kwanini sheria ya mwaka 2009 ianze kutumika sasa?
Kinabo anasema: “Tulikuwa tunajipanga, ilibidi tujipe muda wa kurekebisha baadhi ya kanuni zetu ziendane na sheria hiyo, aidha ilitupasa tuongeze rasilimali watu ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za sheria hiyo mpya.
“Sasa tuko tayari kukabiliana na wajanja wote kwani sasa tuna meno tuliyoyalilia kwa muda mrefu.”
Ili kuhakikisha bidhaa zinazoingizwa nchini zinakuwa na ubora wa viwango vinavyokubalika, shirika lake lina mawakala katika nchi mbalimbali ambao kazi yao ni kuhakikisha bidhaa zinazoingia nchini zinakuwa na viwango vilivyothibitishwa.
“Tunao mawakala makini katika nchi ambazo ni vituo vya kuingiza bidhaa nchini mwetu, lengo ni kuhakikisha hakuna bidhaa ambazo hazijathibitishwa ubora wake zinaingia nchini,” anasema.
Anakumbushia kwamba ujumbe wa mwaka huu wa Siku ya Viwango Duniani, unasisitiza suala la ubora wa bidhaa sokoni katika kukuza uchumi na kulinda mazingira yetu.
Anasema kuna faida kubwa sana za kuzalisha bidhaa zenye viwango vya ubora kwani pamoja na bidhaa hizo kukubalika kwenye masoko ya kimataifa pia huchangia katika kutengeneza ajira endelevu.
Kuhusu sheria hii mpya anasema kanuni ya 13 ya sheria ya uagizaji inasema atakayekiuka taratibu za uagizaji atapata adhabu kama ilivyotajawa hapo juu.
Kinabo anasema kwa mujibu wa sheria hiyo, zipo adhabu ndogondogo ambazo wafanyabiashara wasio waaminfu wanaweza kukumbana nazo na kwamba sheria mpya inampa mamlaka Mkurugenzi Mtendaji wa TBS kutoza faini ya hadi sh milioni 20.
Anafafanua kwamba kwa kawaida sheria inataka sampuli ya bidhaa zinazoingizwa nchini zipite kwenye maabara za TBS ili zipimwe na matokeo ndiyo yatakayoamua kwamba bidhaa husika ziiingie sokoni, ziteketezwe au zirudishwe zilikotoka.
“Hakuna mbadala wa utaratibu huo, bahati mbaya baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakigushi nyaraka mbalimbali vitendo ambavyo kwa sheria ya sasa ni hatari kwao,” anasema.
Anasema ili kukabiliana na msongamano wa bidhaa bandarini, taasisi mbalimbali za serikali ikiwamo TBS zimeweka utaratibu wa kuifanya mizigo isikae bandarini kwa muda mrefu.
Moja ya njia ambayo TBS inaitumia ni kwa kumsainisha mteja fomu inayoitwa inayomwezesha mfanyabiashara kutoa bidhaa kwa masharti ya kuwa hataziuza hadi ukaguzi wa TBS uwe umekamilika.
Pamoja na nia njema hiyo ya serikali kwa wafanyabiashara hao, lakini baadhi yao baada ya kupatiwa fursa hiyo wamekuwa wakiingia mitini na kuiacha TBS ikihaha kuwatafuta na kwamba hadi sasa kuna matukio saba ambayo yamesharipotiwa kwenye vyombo vya dola kuhusiana na wafanyabiashara wa aina hiyo.
“Ni kutokana na tabia hiyo, ndiyo maana tumeamua sasa kutafuta taratibu za kuwabana wahusika ikiwamo kuleta taarifa zao mbalimbali kama barua ya serikali ya mtaa anakotoka ili iwe rahisi kwetu kuwapata, lakini pia tunaangalia utaratibu wa kuzitumia kampuni nyingine zitakayokuwa na kazi ya kuwafuatilia wafanyabiashara wa namna hii,” anasema.
Ili kuhakikisha kwamba sheria hiyo inafanya kazi vizuri, anasema mikakati mbalimbali inafanywa kwa kwa lengo la kutoa elimu kwa umma hususan polisi ili waifahamu sheria hiyo.
Anasema hivi sasa taasisi yake iko katika mkakati wa kutoa mafunzo juu ya sheria hiyo kwa jeshi la polisi ili kuhakikisha kwamba jeshi hilo linatoa mchango mkubwa katika kuchukua sheria kwa wahusika.
Beatus John ni mtaalam wa uchumi na mkazi wa Dar es Salaam, anasema sheria hiyo itasaidia kupambana na wa wajanja ambao wanaoingiza bidhaa hafifu nchini.
Lakini pia anasema wadau mbalimbali wakiwamo wazalishaji, waagizaji wanaotoa elimu juu ya sheria hiyo ili waweze kuwa na uhakika kwamba iwapo itatokea uvunjifu wa sheria na kanuni basi adhabu stahiki itatolewa.
Juma Ali, mkazi wa Dar es Salaam anasema sheria hiyo itawasaidia sana wao kama wafanyabiashara kwani hivi sasa wananchi wameamka katika kufuatilia ubora wa bidhaa zilizoko sokoni.
“Sheria hiii itasaidia kuondoa bidhaa hafifu maana yake tutakuwa na bidhaa nyingi bora ambazo wateja watazifurahia, siku hizi wateja wetu wanafuatilia sana nembo ya ubora ya Tbs, hilo ni jambo jema sana,” anasema.
Majukumu ya Tbs ni mengi lakini baadhi yake ni pamoja na kuhakikisha kwamba bidhaa zinazozalishwa nchini au zinazoagizwa zinakuwa na ubora wa viwango unaokubalika, kuondoa bidhaa hafifu zilizopo sokoni, kuweka taratibu za kuharibu bidhaa duni au kuzirudisha zilikoagizwa na kutoza faini.
Shirika hutekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na taasisi na mamlaka mbalimbali kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Baraza la Mazingira (NEMC), Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).

Chanzo: Tanzania Daima
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top