WAKATI mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) ukitarajiwa kuanza kesho mkoani Dodoma hatma ya uchaguzi wa mjumbe wa mkutano mkuu (Nec) wilayani Longido mkoani Arusha imebaki kitendawili mara baada ya uchaguzi huo kushindwa kujulikana utafanyika lini hadi sasa.
Uchaguzi huo ulikwama kufanyika mwezi uliopita kutokana na wagombea waliojitokeza katika uchaguzi huo kushindwa kufikisha idadi ya nusu ya kura ambapo mbunge wa jimbo hilo Lekule Laiser alipata kura 417,Peter Lemshau alipata kura 381 huku mgombea mwingine aliambulia kura 58.
Uchaguzi huo ulidaiwa kukumbwa na mizengwe na fitina mbalimbali ambapo matokeo yake yalitangazwa usiku wa manane huku baadhi ya wajumbe wake wakipigia kura ndani ya mabasi,kura kuhesabiwa nje ya chumba cha uchaguzi sanjari na jenereta la umeme kuzimika ghafla wakati wa zoezi la kuhesabu kura lilipowadia hali iliyopelekea kura kuhesabiwa gizani.
Hatahivyo,taarifa zisizo rasmi zinadai ya kwamba kumekuwa na njama za chini kwa chini zinazodaiwa kusukwa kwa ustadi mkubwa kwa lengo la kutaka kumpitisha kwa nguvu Laiser lakini baadhi ya makada na viongozi wa CCM wilayani longido wamepaza sauti kwamba watapinga na kuandamana kwa nguvu zote endapo mbunge huyo akishiriki mkutano mkuu wa CCM unaoanza kesho mkoani Dodoma kupitia tiketi ya Nec wilaya ya Longido.