Uchaguzi wa viongozi wa
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA) na Chama cha Makocha wa Mpira
wa Miguu Tanzania (TAFCA) sasa utafanyika Desemba 22 mwaka huu.
Kwa mujibu wa ratiba za
uchaguzi za vyama hivyo, Kamati zao za uchaguzi zitatangaza kuanza mchakato wa
uchaguzi Novemba 10 mwaka huu wakati fomu kwa wanaotaka kugombea uongozi
zitaanza kutolewa Novemba 12 mwaka huu. Mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu ni
Novemba 16 mwaka huu.
Kamati ya Uchaguzi ya
Shirkisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetoa mwongozo huo kwa Kamati ya
Uchaguzi ya TAFCA baada ya kuomba hivyo kutokana na wagombea sita tu kujitokeza
kuomba nafasi tatu za uongozi katika mchakato wa awali.
Kwa waombaji ambao awali
walichukua na kulipia ada ya fomu za kugombea uongozi TAFCA na TAREFA,
hawatatakiwa kulipia tena ada kwa nafasi zile zile walizoomba, isipokuwa
watatakiwa kujaza fomu upya.
PONGEZI KWA UONGOZI MPYA FA
MWANZA
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Novemba 8
mwaka huu.
Ushindi waliopata
viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano
Mkuu wa MZFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo katika Mkoa
wa Mwanza.
TFF inaahidi kutoa
ushirikiano wa kutosha kwa Kamati za Utendaji ya MZFA iliyochaguliwa chini ya
uenyekiti wa Patrick Songora aliyechaguliwa kwa kipindi cha pili
mfululizo.
Uongozi huo mpya wa MZFA
una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira
wa miguu kwa kuzingatia katiba ya chama chao pamoja na vyombo vya mpira wa miguu
vilivyo juu yao.
Pia tunatoa pongezi kwa
Kamati ya Uchaguzi ya MZFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi
unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa
TFF.
Viongozi waliochaguliwa
kuongoza MZFA ni Patrick Songora (Mwenyekiti), Nassoro Mabrouk (Katibu) na
Richard Kadutu (Mwakilishi wa Klabu TFF).
Boniface
Wambura
Ofisa
Habari
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF)
Post a Comment