Uchumi unaendelea kuimarika kutokana na usimamizi bora wa uchumi mkuu, lakini watu masikini waishio vijijini hawajaona bado manufaa ya kukua huko.
 
Uchumi wa Tanzania unaendelea kukua kwa kiwango kizuri cha zaidi ya asilimia sita kwa kipindi cha mwaka uliopita, ukiongezea kwamba nakisi ya fedha imepungua kwa kiasi kikubwa licha ya kuwepo kwa mazingira magumu nje ya nchi. Ukuaji huu mzuri unaovutia wa uchumi unatokana na uwezo wa Serikali kufanya mabadiliko yanayostahili katika kutumia sera za hazina na fedha, hususani katikati ya ongezeko kubwa la mfumuko wa bei ulioonekana kuanzia mwezi Novemba, 2011.
Haya yote yanaonyeshwa katika dondoo muhimu za ripoti ya hivi karibuni kuhusu Hali ya Sasa ya Uchumi wa Tanzania inayojulikana kama ‘Kutanua Mbawa: Kutoka Ukuaji wa Uchumi hadi Ustawi wa Pamoja’, ambayo ni ripoti ya pili katika mfululizo wa ripoti zinazotolewa mara mbili kila mwaka zilizozinduliwa na Benki nchini Tanzania mwezi Februari 2012. Lengo la mfululizo wa ripoti hizi ni kukuza mjadala wa sera unaojenga kati ya wadau na watunga sera na kuchochea mijadala kuhusu masuala muhimu ya uchumi.
Ikiwa na ukuaji wa uchumi unaofikia asilimia 6.5 kwa kipindi cha mwaka 2011/12, na nakisi ya hazina na fedha za matumizi ya kawaida iliyodhibitiwa, Tanzania imefanya vizuri zaidi kuliko nchi nyingi zinazoibukia kwa haraka kiuchumi, ikiwemo India na Brazil,” anaandika Bw. Jacques Morisset, mtunzi mkuu na Mchumi Mkuu kwa nchi za Tanzania, Uganda na Burundi.
Utendaji imara kifedha ulioonyeshwa na Tanzania unatokana zaidi na makusanyo makubwa ya kodi na jitihada za serikali katika kuzuia matumizi yasiyokuwa ya kipaumbele. Marekebisho haya hayahusiani na matumizi ya maendeleo, ambayo yaliendelea kuongezeka kwa lengo la kushughulikia mapungufu yaliyopo katika miundombinu nchi nzima.
Aidha, pamoja na mafanikio haya licha ya kiwango kikubwa cha mfumuko wa bei usiopungua, Tanzania itaendelea kuonyesha ukuaji chanya wa uchumi, Pato Ghafi la Taifa likitarajiwa kukua kwa asilimia 6.5 hadi 7.0 kwa mwaka 2014 ili mradi pasiwepo na athari nyingine kutoka nje ikiwemo mabadiliko ya bei ya bidhaa na chakula. Hata hivyo ripoti hii inaonya kwamba mafanikio ya sasa yataendelea iwapo tu Serikali itaweka msisitizo katika uendelevu wa sera za fedha na madeni na matumizi mazuri ya rasilimali za umma, ufuatiliaji wa karibu wa fedha za umma, zikiwemo zile za mawakala na mashirika ya umma yanayofanya kazi katika sekta ya nishati.
Hata hivyo, Taarifa za Hali ya sasa ya Uchumi zinasisitiza kwamba ukuaji imara wa uchumi wa Tanzania umeendelea kuziacha pembeni kaya za vijijini ambazo zina watu takribani theluthi mbili ya idadi ya watu wote nchini na asilimia 80 ya watu masikini ambao wanaendelea kuishi katika mazingira magumu. Kuwezesha kujumuishwa kwa kaya za vijijini katika mchakato wa ukuaji wa uchumi wa nchi unapaswa kuwa msingi wa mjadala wa sera nchini Tanzania.
Wakati hakuna mpango makini wa kufanikisha mageuzi ya kijamii na kiuchumi, Tanzania inaweza kutiwa moyo na uzoefu wa nchi zilizofanikiwa ambazo zilikuwa na sifa za kiuchumi zinazofanana nayo miongo michache iliyopita.
“Uzoefu wa nchi za Vietnam na Malaysia umeonyesha kwamba umasikini uliokithiri vijijini si lazima uendelee kuwepo,” anasema Philippe Dongier, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Uganda, na Burundi. Nchi hizi zimeweza kusimamia nguvu kuu tatu ambazo zina uwezo wa kuleta mageuzi nchini Tanzania. Nguvu hizo ni: kufanya mageuzi ya kilimo na kukifanya kiwe cha kibiashara; kupanua wigo wa biashara kuelekea bidhaa zenye thamani ya juu na kufanya shughuli nyingine mbali na kilimo; na uhamiaji kuelekea mijini.