SIKU moja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,
kuwahukumu adhabu ya kifo askari wa wiwili wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na
mmoja wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) kwa kosa la kumuua kwa kukusudia Swetu
Fundikira, wafungwa hao jana wamewasilisha hati mahakamani hapo ya kusudio la
kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.
Wafungwa hao ni MT 1900 Sajenti Roda Robert (42), MT 85067
Koplo Mohamed Rashid wa JKT Mbweni na MT 75854 Koplo Ally Ngumbe (37) wa kikosi
cha JWTZ Kunduchi.
Wakili wa askari wa wafungwa hao, Mluge Karoli, alisema
ameishawasilisha hati hiyo mahakamani hapo jana kwa madai kuwa wateja wake
hawakubaliani na hukumu hiyo iliyotolewa juzi na Jaji Zainabu Mruke ambaye
aliwatia hatiani kwa kosa la kuua kwa kukusudia kinyume na kifungu cha 196 cha
Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.
Karoli alieleza kuwa sababu zilizomsukuma yeye na wateja
wake kuwasilisha hati hiyo ni kwamba
kesi yoyote ya ugomvi
haiwezi kuwa na kusudio la kutaka
kuua na kwamba hakuna shahidi wa upande wa jamhuri aliyefika mahakamani hapo na
kueleza kuwa wateja wake ndiyo wamemuua Swetu Fundikira.
Alieleza kuwa, aliyepambana na wateja wake ni Swetu
Fundikira na uchunguzi wa daktari unaonyesha jina la Swetu Ramadhani Fundikira
hivyo ni watu wawili tofauti, na kwamba hakuna hata shahidi mmoja alifika
mahakamani na kueleza aliwahi kuuona mwili wa marehemu au kuhudhuria kwenye
msiba.
Askari hao kwa pamoja walidaiwa kuwa walimpiga Fundikira,
Januari 23 mwaka huu saa 7:30 usiku wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam na
baadaye kufariki dunia usiku huo huo wa kuamkia Januari 24, mwaka 2010, katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Akisoma hukumu hiyo juzi , Jaji Muruke alisema ingawa
hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa washtakiwa hao ndio waliomuua Fundikira,
ushahidi uliotolewa na upande wa
mashtaka (Jamhuri) ulikuwa ni ushahidi wa mazingira, kwamba Jamhuri imeweza
kuthibitisha mashtaka hayo.
Source:Habari Leo
Post a Comment