Kipa Mwadini Ally kulia akimpongeza Nahodha wake, Jabir Aziz baada ya kufunga penalti ya mwisho |
Na Mahmoud
Zubeiry wa Bin Zubeiry, Kinshasa
AZAM FC
imefanikiwa kutinga Fainali ya Kombe la Hisani, baada ya kuifunga kwa mikwaju ya
penalti 5-4 Shark FC ya hapa, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 kwenye
Uwanja wa Martyrs jioni hii.
Nahodha
Jabir Aziz Stima ndiye aliyekwenda kupiga penalti ya mwisho, Shark wakitoka
kupoteza, kufuatia mpira kugonga mwamba. Aiziz aliwainua vitini wachezaji
wenzake na makocha wake pamoja na viongozi wa wachache wa timu hiyo waliopo hapa
kwa kupiga penalti maridadi iliyotinga nyavuni.
Azam sasa,
itamenyana na mshindi wa mechi inayoendelea hivi sasa kati ya Dragons na FC MK
Jumapili katika fainali.
Azam
iliuanza mchezo huo vizuri na ikicheza kwa maelewano makubwa sambamba na
kushambulia kwa kasi kutokea pembeni, kulia Kipre Herman Tchetche na kushoto
Seif Abdallah.
Hata hivyo,
shambulizi la kushitukiza la Shark liliwapa bao la kuongoza dakika ya 16,
lililofungwa na Ngulubi Kilua, baada ya mabeki wa Azam kudhani
ameotea.
Iliwachukua
dakika 10 tu Azam kusawazisha bao hilo, mfungaji akiwa Gaudence Exavery
Mwaikimba aliyeunganisha kwa kichwa krosi maridadi ya nyota wa mchezo wa leo,
Kipere Herman Tcheche kutoka wingi ya kulia.
Baada ya bao
hilo, Azam iliendelea kuwashambulia Shark na dakika ya 37, Kipre Tchetche
aliifungia timu hiyo bao la pili, kufuatia kazi nzuri ya Mwaikimba. Mwaikimba
alipokea mpira mrefu, akatuliza na kumtangulizia kwa mbele mfungaji, ambaye
hakufanya makosa, alimchambua kipa wa timu inayomilikiwa na mdogo wa rais wa
DRC, Joseph Kabila.
Hadi
mapumziko, Azam ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-1 na kipindi cha pili Shark
waliingia kwa kasi na kufanikiwa kusawazisha kwa penalti dakika ya 47, iliyotiwa
nyavuni na Bukasa Kalambai, ambaye yeye mwenyewe alijiangusha kwenye eneo la
hatari baada ya kuzongwa na beki David Mwantika.
Baada ya
dakika 90 kutimu timu hizo zikiwa zimefungana 2-2, sheria ya matuta ilichukua
mkondo wake na wachezaji wote watano wa Azam waliopewa dhamana hiyo leo na kocha
Muingereza Stewart Hall, walitimiza wajibu wao
vizuri.
Kipre
Tchetche alifunga ya kwanza, Mwaikimba ya pili, Jaockins Atudo ya tatu, Himid
Mao ya nne na Stima akapiga ya ushindi.
Stewart
alisema amefurahishwa na matokeo ya mchezo wa leo na sasa ana matumaini ya timu
yake kurejea na Kombe hilo Dar es Salaam.
Katika
mchezo wa leo, kikosi cha Azam kilikuwa; Mwadini Ally, Himid Mao, Samih Hajji
Nuhu, Joackins Atudo, David Mwantika, Jabir Aziz, Kipre Balou, Seif
Abdallah/Uhuru Suleiman dk 77, Kipre Tchetche, Humphrey Mieno na Gaudence
Mwaikimba.
Post a Comment