Uganda watatetea ubingwa leo? |
BINGWA wa
Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge,
anatarajiwa kupatikana leo kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole mjini Kampala,
Uganda, wakati wenyeji The Cranes watakapomenyana na jirani na mahasimu wao
wakubwa katika ukanda huu, Kenya, Harambee Stars kuanzia saa 1:00
usiku.
Mchezo huo,
utatanguliwa na mechi ya kusaka mshindi wa tatu, kati ya Tanzania Bara na
Zanzibar, itakayoanza saa 10:00 jioni kwenye Uwanja huo huo, unaomilikiwa na
serikali ya Uganda.
Mechi zote
zinatarajiwa kuwa na upinzani mkali, kwani ukiacha fainali, hata mchezo wa
kusaka mshindi wa tatu utakutanisha majirani na timu zinazofahamiana vema.
Zanzibar
ilitolewa na Kenya katika Nusu Fainali kwa kufungwa kwa penalti 4-2, kufuatia
sare ya 2-2 ndani ya dakika 120, wakati Bara ilichapwa 3-0 na Uganda juzi.
Kulingana na
tathmini ya viwango vya timu zote tangu kuanza kwa mashindano haya, Uganda,
ambao pia ni mabingwa watetezi, wanapewa nafasi kubwa ya kutwaa Kombe
leo.
Hata hivyo,
fainali ni mchezo wa maarifa mengi zaidi ya uwezo, hivyo haitakuwa ajabu hata
Kenya ikiibuka na mwali leo.
Zanzibar na
Bara, itakuwa mechi ya kuonyeshana ufundi na nani zaidi, kwani wachezaji wengi
wanafahamiana kwa mfano, leo mshambuliaji wa Bara, John Bocco atakuwa
anadhibitiwa na beki anayecheza naye klabu moja, Aggrey
Morris.
Au Mrisho
Ngassa wa Bara pia, ambaye yuko mbioni kuhamia El Merreikh ya Sudan akipangwa
kulia, atakuwa anakabiliana na beki aliyekuwa anacheza naye klabu moja, Simba
SC.
Kenya ni
mabingwa mara tano wa Kombe la Challenge la CECAFA katika miaka ya 1975, 1981,
1982, 1983 na 2002, wakati pia imeshika nafasi ya pili mara nne na Uganda ndio
timu iliyotwaa mara nyingi zaidi taji hilo, (mara 12) katika miaka ya 1973,
1976, 1977, 1989, 1990, 1992, 1996, 2000, 2003, 2008, 2009 na 2011 na pia
imeshika nafasi ya pili mara nne.
Michuano ya
mwaka huu, imedhaminiwa na Kampuni ya Bia Afrika Mashariki (EABL), kupitia bia
yake ya Tusker Lager, kwa dau la la dola za Kimarekani 450,000 na lengo ya
michuano ya mwaka huu ni kuzisaidia maandalizi timu za Afrika Mashariki na Kati
katika kuwania tiekti ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 nchini
Brazil.
Udhamini wa
mwaka huu ni ongezeko la aslimia 5, kutoka michuano ya mwaka jana mjini Dar es
Salaam, ambayo Uganda waliibuka mabingwa.
Ni udhamini
ambao umehusu usafiri, malazi na huduma nyingine, wakati jumla ya dola za
Kimarekani 60.000 zitakuwa kwa ajili ya zawadi, bingwa akipewa dola 30.000,
mshindi wa pili dola 20.000 na dola 10.000 mshindi wa tatu na michuano imekuwa
ikionyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Super Sport ya Afrika
Kusini.
Michuano
hiyo ambayo huandaliwa na CECAFA, Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na
Kati, ambalo lina wanachama 13, ndiyo ya kwanza kabisa mikubwa kufanyika barani
Afrika, ilihusisha mataifa manne, Kenya, Uganda, Tanganyika (sasa Tanzania Bara)
na Zanzibar, ikijulikana kwa jina la Kombe la
Gossage.
Michuano
hiyo ya Gossage ambayo sasa imekuwa Kombe la Challenge, ilifanyika mara 37
kuanzia mwaka 1926 hadi 1966, ilipobadilishwa jana na kuwa michuano ya wakubwa
ya soka kwa mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, ilifanyika mara saba kati ya
mwaka 1965 na 1971, ilipozaliwa rasmi CECAFA
Challenge.
Tanganyika
ilianza kushiriki michuano hiyo tangu mwaka 1945, wakati Zanzibar ilijitosa
miaka minne baadaye, 1949.
Michuano
hiyo ilikuwa ikidhaminiwa na bepari aliyekuwa akimiliki kiwanda cha sabuni,
William Gossage, aliyezaliwa Mei 12 mwaka 1799 na kufariki dunia Aprili 9, mwaka
1877.
Michuano
hiyo mikongwe zaidi barani, imekuwa ikiandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka
Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), ikihusisha timu za taifa za ukanda
huo.
Hadi
inafikia tamati michuano ya Gossage, Uganda ilikuwa inaongoza kwa kutwaa taji
hilo, mara 22, ikifuatiwa na Kenya iliyotwaa mara 12 na Tanzania mara
tano.
Mwaka 2005,
michuano hiyo ilifanyika chini ya udhamini wa bilionea wa Ethiopia mwenye asili
ya Saudi Arabia, Sheikh Mohammed Al Amoudi na kupewa jina la Al Amoudi Senior
Challenge Cup, lakini sasa Tusker ndiyo mambo yote. Je, nani ataibuka bingwa wa
Challenge mwaka huu, ni Uganda tena au Kenya? Bila shaka hilo ni jambo la
kusubiri na kuona.
Post a Comment