**************
DAKTARI wa Taasisi ya Mifupa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MOI), Deodata Matiko (30) na Muuguzi, Erick Kimwomwe (28), wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili, likiwamo kuomba na kupokea rushwa.
Akisoma hati ya mashtaka jana, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Allen Kasamala alidai kuwa washtakiwa walifanya makosa hayo kinyume na kifungu cha 15 (1) cha sheria ya Takukuru, sura ya 11 ya mwaka 2007.
Kasamala alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Hellen Liwa kuwa Novemba 27 mwaka huu, katika Taasisi ya Mifupa iliyopo kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, washtakiwa hao walimwomba Sandford Harun Mhina, rushwa ya Sh1.5 milioni.
Alidai kuwa washtakiwa hao, walimwomba rushwa hiyo kama kishawishi cha kumsaidia na kuhakikisha kuwa ndugu yake Fanuel Daniel Gidion. aliyelazwa katika wodi ya Sewahaji anafanyiwa upasuaji.
Katika shtaka la pili, Kasamala anadai kuwa Novemba 29 mwaka huu, Matiko na Kimwomwe walipokea rushwa ya Sh1 milioni kutoka kwa Sandford kwa ajili ya kufanikisha upasuaji huo wa ndugu yake Fanuel.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wote walikana tuhuma hizo na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na kwamba hawana pingamizi na dhamana.
Hakimu Liwa aliwaambia washtakiwa hao kuwa dhamana ipo wazi ma kwamba wanatakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaofanya kazi katika taasisi zinazotambulika kisheria ambao kila mmoja wao atasaini bondi ya Sh1.5 milioni.
Pia aliwataka wasitoke nje ya Jiji la Dar es Salaam bila kibali cha mahakama.
Dk Deodata aliachiwa huru baada ya kukamilisha masharti hayo ya dhamana huku mwenzake Erick alipelekwa rumande baada ya kushindwa kukamilisha masharti hayo.
chanzo: Mwananchi
Pia aliwataka wasitoke nje ya Jiji la Dar es Salaam bila kibali cha mahakama.
Dk Deodata aliachiwa huru baada ya kukamilisha masharti hayo ya dhamana huku mwenzake Erick alipelekwa rumande baada ya kushindwa kukamilisha masharti hayo.
chanzo: Mwananchi
Post a Comment