Waziri wa Nishati na
Madini Mhe. Profesa Sospeter Muhongo akipitia taarifakuhusu mikataba
iliyokwishaingiwa na Serikali ya Utafutaji mafuta na gesi mara baada ya kuipokea
kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC), Bw. Michael Mwanda.
Na: Afisa habari, Wizara ya Nishati na
Madini
Bodi ya Wakurugenzi ya
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imekabidhi rasmi kwa Mheshimiwa
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ripoti kuhusu mikataba
iliyokwishaingiwa na Serikali ya utafutaji mafuta na gesi asilia. Ripoti hiyo
ilikabidhiwa Ijumaa iliyopita, Novemba 30 mwaka huu ofisini kwa Waziri jijini
Dar es Salaam.
Ripoti hiyo iliandaliwa
kufuatia agizo la Mhe. Waziri kwa Bodi hiyo kuipitia mikataba yote 26 ya
utafutaji mafuta na gesi asilia. Lengo mahsusi lilikuwa ni kuhakikisha kwamba
endapo kuna mapungufu katika mikataba hiyo, mapungufu hayo yasijirudie tena
katika mikataba mipya ya baadaye, pamoja na kuwezesha Bodi hiyo kuelewa vizuri
kazi iliyo mbele yao.
Akipokea ripoti husika
kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi Bw. Michael Mwanda, Waziri Muhongo aliahidi
kuisoma na kuyafanyia kazi mapema mapendekezo yote. Aidha, aliipongeza Bodi hiyo
kwa kufanya kazi hiyo na kuwasilisha kwa wakati akisisitiza kuwa suala la kujali
muda ni moja ya mambo ya msingi anayoyasimamia ili kuwa na utekelezaji makini wa
majukumu mbalimbali hususan katika Wizara anayoiongoza.
Waziri Muhongo pia
alisema ni vyema kwa Wajumbe wa Bodi wakajifunza kwa haraka kutoka nchi
zilizofanikiwa kutokana na rasilimali za mafuta na gesi asili, kama Uholanzi,
Oman, Malaysia na Norway.
Kwa upande mwingine
alisema ni vyema pia kujifunza kutoka nchi ambazo hazijafanikiwa katika
kusimamia rasilimali husika kama Nigeria ili kupata ufahamu wa makosa
waliyofanya ambapo ufahamu huo utawasaidia kuepuka makosa ambayo nchi hiyo
ilifanya.
Aidha, Serikali inaandaa
Sera ya gesi asili kwa umakini ili iwe dira ya kuongoza shughuli za uzalishaji
na utumiaji wa gesi asili. Mikataba 26 ya TPDC ni sehemu ya nyaraka muhimu za
kuboresha utayarishaji wa sera ya gesi asili. Wananchi wote wanahusishwa kutoa
maoni ili kuiboresha Sera hiyo.
Post a Comment