Diwani (CHADEMA) wa kata ya Iseke tarafa ya
Ihanja jimbo la Singida Magharibi, Bw.Amos Rubein Mughenyi akizungumza na
waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) juu ya uamuzi wake wa kujiuzulu
udiwani.Amedai kuwa uamuzi huo unatokana na CHADEMA kumzuia kushirikiana na
viongozi wa serikali na pia kuchangisha wananchi michango ya maendeleo
yao.Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Singida, Illuminata Mwendwa,amekiri
kupokea barua ya Amos kujiuzulu na ameisha ijulisha TAMISEMI ili iweze kupanga
tarehe ya uchaguzi mdogo.(Picha na Nathaniel
Limu).
Na. Nathaniel
Limu.
Akitangaza uamuzi huo mzito mbele za waandishi
wa habari, Amosi amesema amejiuzulu nafasi ya udiwani huo kuanzia Desemba 21
mwaka huu.
Amesema uamuzi wake huo ambao haujatokana na
kushawishiwa wala kulazimishwa na mtu au chama chochote cha siasa, umetokana na
CHADEMA kumzuia kushirikiana na viongozi wa serikali ngazi ya wilaya na mkoa
katika kusimamia shughuli za maendeleo.
Amosi amesema amekuwa akishinikizwa
asikubaliane na changizo (michango) ya aina yoyote ya maendeleo ya Kata yake,
kwa madai kuwa jukumu la kuwaletea maendeleo wakazi wa kata ya Iseka ni la
serikali pekee.
“Hivi sasa Kamati ya maendeleo ya Kata ya
Iseke (WDC) imeazimia kufanya harambee kwa ajili ya kutafuta fedha za ujenzi wa
madarasa na maabara katika shule yetu ya sekondari. Tunapendekeza Waziri wa
Ujenzi Dk. John Pombe Magufuli awe mgeni rasmi katika harambee hiyo, CHADEMA
wamenigomea” ,alisema Amosi kwa masikitiko
makubwa.
Amesema viongozi wa CHADEMA wilaya wamemtaka
akae pembeni asijihusishe na harambee hiyo, na kama atalazimika ashiriki, basi
mgeni rasmi awe ni askofu yeyote na sio kiongozi wa chama chochote cha Siasa au
wa serikali.
“Nimeamua kwa ridhaa yangu mwenyewe kujiuzulu
wadhifa huu, ili wananchi wangu wawe huru kujipangia shughuli zao za maendeleo
bila kuzuiwa na itikadi ya CHADEMA baada ya mimi kuwa sio Diwani tena wa Kata
hiyo”, alisema Amosi kwa kujiamini.
Aidha ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa
serikali na hasa mkuu wa Wilaya ya Ikungi Manju Msambya, aendelee kuwaunga
mkono wananchi wa Iseke, wafanikishe zoezi lao la harambee, ili waweze kujenga
vyumba vya madarasa.
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa halmashauri ya
wilaya ya Singida lluminata Mwendwa amekiri kupokea barua ya Amos kujiuzulu
udiwani kata ya Iseke na kwamba wameishaijulisha TAMISEMI ili iweze kupanga
tarehe ya uchaguzi mdogo wa kata hiyo.
Tundu Lissu mara kwa mara amekuwa akisikika
kuwa wananchi wa Jimbo lake watakuwa na likizo ya kutochangia maendeleo yake,
hadi hapo Ubunge wake utakapokoma.
Hata hivyo uamuzi wake huo ambao inadaiwa
umechangia wananchi na hasa vijana wa jimbo lake kuwa wavivu kufanya kazi,
unapingana na utendaji wa viongozi wenzake wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti wa
Taifa Bw. Freeman Mbowe na Mh. Kabwe Zitto, ambao wananchi wa majimbo yao
wanashiriki kikamilifu kuchangia maendeleo.
Post a Comment