MKURUGENZI wa Habari na Uenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika amemtaka Katibu Mkuu Kiongozi (Ofisi ya Rais-Ikulu) Balozi Ombeni Sefue na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi (Ofisi ya Rais) Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Yambesi watoe kauli kwa umma kuwa Serikali imetoa waraka mpya kwa watumishi wa umma kuhudhuria mikutano ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoa taarifa kama sehemu ya kazi zao kama wanavyofanya sasa na chama hicho.
Mnyika ametoa kauli hiyo
katika taarifa yake kwa vyombo vya habari baada ya hivi karibuni CCM kuwatumia
watumishi wa umma kutoa taarifa katika mikutano yake jambo ambalo amedai ni
kinyume na sheria. “Kwa sasa utumishi wa umma katika nchi yetu unaongozwa na
Sheria ya Utumishi wa Umma na. 8 ya mwaka 2002 pamoja na marekebisho yake ya
mwaka 2007 pamoja na kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003 kama
zilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2009 na kanuni za maadili ya utendaji katika
utumishi wa umma za mwaka 2005.”
“Itakumbukwa kwamba
awali utumishi wa umma Tanzania ulikuwa ukiongozwa na Sheria ya Utumishi
Serikalini namba 16 ya mwaka 1989 na Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma Toleo
la 1994 pamoja na marekebisho yake. Kifungu cha 4(1) cha Sheria hiyo kilimpa
mamlaka Mkuu wa Utumishi wa Umma, ambaye ni Katibu Mkuu kiongozi kutoa waraka
kuhusu taratibu mbalimbali za utumishi wa umma.” Alisema Mnyika katika taarifa
hiyo.
“Chini ya Mamlaka hayo,
aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Martem Y.C. Lumbanga tarehe 26 Juni, 2000 alitoa
Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma na. 1 wa mwaka 2000 wenye kumb. Na.
SHC/C.180/2/113 uliohusu maadili ya Watumishi wa Umma katika mfumo wa vyama
vingi vya siasa. Waraka huo unawataka watumishi wa umma kutekeleza wajibu wao wa
utumishi bila kufanya upendeleo wala ubaguzi wa chama chochote cha siasa. Waraka
huo unawakataza watumishi wa umma kuzungumza na kutoa taarifa kwenye mikutano ya
vyama vya siasa na haujatoa ruhusa kwa watumishi hao kuzungumza katika mikutano
ya CCM pekee; hivyo Balozi Sefue na Yambesi wanapaswa kutoa kauli kwa umma iwapo
Serikali imetoa waraka mwingine kwa siri wenye kuagiza watumishi wa umma kutoa
taarifa katika mikutano ya CCM.”
Aidha aliongeza kuwa
kanuni za maadili ya utendaji katika utumishi wa umma hazielekezi watumishi wa
umma kuwa na utii au kuwajibika kwa CCM bali zinaeleza kwamba watumishi wa umma
watawajibika kwa umma na watakuwa na utii kwa Serikali na sio chama
kinachotawala na zimeweka mipaka ya matumizi sahihi ya taarifa za kiserikali
wanazowajibika kuzitoa kwa nafasi zao.
“…mapendekezo ya Tume ya
Nyalali ya mwaka 1991 na marekebisho ya Katiba ya mwaka 1992 kuingia katika
mfumo wa vyama vingi na marekebisho ya sheria yaliyofuata yameweka uhuru wa
watumishi wa umma katika kujiunga na vyama vya siasa (isipokuwa watumishi wa
kada maalum) na mipaka ya mahusiano kati ya kazi zao za kiserikali na shughuli
za vyama vya siasa kikiwemo chama kinachotawala. Hivyo maagizo au waraka wenye
kuwalazimisha watumishi wa umma kuhudhuria mikutano ya CCM na kutoa kutoa
taarifa ni kinyume cha uhuru wa kikatiba, sheria za nchi, kanuni za utumishi wa
umma na misingi ya utawala bora,” alisema Mnyika katika taarifa hiyo.
Post a Comment