Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda
***************
Serikali imeviagiza viwanda vyote vya saruji
nchini kutoa mchanganuo wa gharama halisi za uzalishaji ili kuangalia uwezekano
wa kupunguza bei ya bidhaa hiyo.Kadhalika, imesema kuwa haiwezi kuweka vikwazo vya kibiashara dhidi ya Saruji inayoingizwa nchini kutoka nje kama wamiliki wa viwanda vya ndani vinavyozalisha bidhaa hiyo walivyoomba.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, wakati wa uzinduzi wa kinu kipya cha kuzalisha saruji cha Kiwanda cha Twiga Cement eneo la Wazo Hill, jijini Dar es Salaam.
Dk Kigoda alisema bila kujua gharama zinazotumika katika uzalishaji kwa kila kiwanda, itakuwa vigumu kwa serikali kutoa ushauri wa namna ya kupunguza bei ya saruji katika soko la ndani.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya uzinduzi huo, Dk. Kigoda alisema nia ya serikali ni kuhakikisha saruji inauzwa kwa bei ambayo wananchi wengi wanamudu na kwamba hilo halitawezekana kama gharama za uzalishaji hazitajulikana.
Aliahidi kwamba serikali ina mipango ya kuhakikisha viwanda hivyo vinakuwa na umeme wa kutosha, barabara nzuri pamoja na kuboresha usafiri wa reli.
Dk. Kigoda alisema mafanikio ya kiwanda hicho ni moja ya mikakati mizuri ya kubinafsisha viwanda iliyofanywa na serikali ya wamu ya tatu wakati akiwa Waziri wa Mipango na Ubinafsishaji ingawa alikiri kwamba zoezi hilo lilikuwa gumu kwa kuwa alikosolewa na watu wengi.
Kuhusu ombi la wamiliki wa viwanda vya saruji kutaka serikali iweke vikwazo vya kibiashara katika kuingiza bidhaa hiyo, Dk. Kigoda alisema suala hilo haliwezekani kwa kuwa bado uzalishaji wa ndani hautoshelezi mahitaji.
Alikiri kwamba Ssruji inayotoka nje inauzwa kwa bei ya chini na kwamba hiyo ni changamoto ili kuhakikisha viwanda vya ndani vinashindana katika soko.
Kwa sasa kuna viwanda vitatu vya saruji ambavyo ni Tanga Cement, Mbeya Cement na Twiga Cement ambavyo vinazalisha huku vinne vikiwa katika hatua za mwisho za ujenzi.
Mwenyekiti wa Heidelberg Cement, Jean Junon, alisema uzinduzi wa Kinu hicho utaongeza uzalishaji kutoka tani milioni 1.1 hadi tani milioni 1.3 kwa mwaka.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment