Viongozi wa nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki wamekubaliana kujenga miundombinu ya usafiri wa reli na bandari ili kuimarisha uchumi wa nchi wanachama.
Kwenye makubaliano hayo, Viongozi wa mataifa wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki wameafikiana kwa pamoja kuanzisha mpango wa ujenzi wa miradi ya miundombinu katika kipindi cha miaka kumi ijayo. Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa barabara, reli, bandari na uzalishaji kawi.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwenyekiti anayeondoka wa Jumuiya hiyo, Rais Mwai Kibaki, amesema hatua hiyo itasaidia sana eneo hilo.
“Kwa wakati huu mizigo inayosafirishwa kwa reli ni chini ya asilimia tano na hiyo inaweka mzigo mkubwa kwa usafiri wa barabara. Huku kiwango cha mizigo kikitarajiwa kuongezeka mara tatu katika kipindi cha miaka 15 ijayo, tatizo la usafiri litazidi kuwa kubwa. Kwa hivyo ipi haja kwetu sisi kuwekeza ipasavyo na kupanua mifumo yetu ya reli”.
Viongozi hao wamesema kwamba kuna haja ya ushirikiano kati ya mataifa wanachama wa jumuia ya Afrika mashariki na nchi jirani ili kujenga miundonsingi ya kuunganisha maeneo ya kiuchumi yuanayopakana na Jumuiya ya Afrika Mashariki.