Beki wa Manchester United,
Mfaransa Patrice Evra akiwajibika dimbani katika moja ya mechi za timu
yake
MANCHESTER, England
“Nadhani Ferguson atamfukuza kima mmoja miongoni mwetu
kama tutafanya jambo hilo tena. Hapana, niko ‘serious’ atatutimua. Litakuwa pigo
kuu na aibu kwa mashabiki, wachezaji, kwa kila mtu hapa Old Trafford. Mimi
nakumbuka kilichotokea mwaka jana. Tulikuwa vinara kwa tofauti ya point nane na,
mwishoni, tukapoteza ubingwa wa ligi”
BEKI wa kimataifa wa Ufaransa na klabu ya Manchester
United, Patrice Evra amesisitiza kwamba kocha mkuu wa Mashetani hao Wekundu wa
Old Trafford, Sir Alex Ferguson anaweza kumfukuza kila mchezaji wa klabu hiyo,
iwapo itashuka katika kilele cha uongozi wa Ligi Kuu.
Man United ina kumbukumbu mbya ya kufuta pengo la point
inane ililokuwa nalo kileleni, kabla ya kujikuta ikipoteza nafasi ya kutwaa
ubingwa kwa tofauti ya mabao, dhidi ya waliotwaa ubingwa huo majirani na
mahasimu wao wakuu Manchester City.
Kauli ya Evra ilitokana na swali aliloulizwa kuwa anahisi
United inaweza kurejea anguko la msimu uliopita, ambapo alijibu: “Nadhani
Ferguson atamfukuza kima mmoja miongoni mwetu kama tutafanya jambo hilo tena.
Hapana, niko ‘serious’ atatutimua.
“Litakuwa pigo kuu na aibu ya kila mmoja, kwa mashabiki,
wachezaji, kwa kila mtu hapa Old Trafford. Mimi nakumbuka kilichotokea mwaka
jana. Tulikuwa vinara kwa tofauti ya point inane na, mwishoni, tukapoteza
ubingwa wa ligi.”
Man United ilipanua wigo wake wa pointi kileleni mwa
msimamo na kufikia sita, baada ya kuwachapa watetezi hao kwenye Uwanja wa Etihad
Jumapili, kwa mabao 3-2.
Lakini Evra, 31, anasema kwamba matokeo hayo kwao yatakuwa
na maana kubwa kama watafanikiwa kushinda mechi moja baada ya nyingine, wakianza
na mtanange wao wa Jumamosi dhidi ya ‘Paka Weusi’ Sunderland.
Evra akaongeza: “Uongozi wa pointi sita kileleni... ligi
bado haijaisha kabisa, kuna safari ndefu kuelekea mwishoni mwa msimu. Lakini
kusema kweli nina uhakika tuko tayari kwa mpambano dhidi ya Sunderland.”
Ushindi wa Man United Etihad dhidi ya Man City,
ulihitimisha rasmi mbio za mabingwa hao kucheza mechi 37 nyumbani bila kufungwa,
iliyoanzia msimu uliopita, lakini pia ikihitimisha ubabe wao katika msimu huu wa
Ligi Kuu – ambako ilikuwa haijawahi kufungwa nyumbani wala ugenini.
Evra anaamini kwamba ushindi huo umewaongezea faida kubwa
kikosini kisaikolojia na kuwapa nguvu yam bio za ubingwa msimu huu; “Ilikuwa ni
jambo muhimu kuishinda Man City na kuwawashia indiketa. Kisaikolojia, ilikuwa
muhimu mno.”
Post a Comment