HATIMAYE huduma katika
Hoteli ya Double Tree Hilton ya jijini Dar es Salaam zimerejea baada ya maofisa
wa Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuridhika na marekebisho
yaliyofanyika, hivyo kuifungulia.
Mkurugenzi wa Mauzo,
Florenso Kirambata, alisema kuwa shughuli zimerejea kikamilifu kuanzia Desemba
22, mwaka huu, baada ya maelekezo kutekelezwa.
“Uongozi wa hoteli
unapenda kutoa shukrani za dhati kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais
(Mazingira), Dk. Terezya Huvisa, pamoja na maofisa wa NEMC kwa ushirikiano mzuri
uliotuwezesha kutimiza maelekezo yote na hivyo kurejesha huduma katika hoteli
yetu,” alisema.
Kirambata alifafanua
kuwa, bomba dogo lililokuwa linatiririsha maji baharini awali limekwisha
kuzibwa, ambapo NEMC imeridhia marekebisho yaliyofanyika na kuwaondolea
zuio.
“Nawashukuru wateja wetu
wote na wadau wengine kwa uvumilivu wao wakati wote wa kipindi cha mpito, na
tunawaahidi kuendelea kuboresha huduma zetu kuifanya hoteli yetu mahali pazuri
kwa wageni,” alisema Kirambata.
Mwanzoni mwa juma
lililopita, Waziri Huvisa alitoa amri ya kufungwa kwa hoteli hiyo kufuatia
ukiukwaji wa taratibu za utunzaji bora wa mazingira.
Hata hivyo, uongozi wa
hoteli ulikiri kosa na kufanya marekebisho haraka na kueleza kwamba kwa kawaida
magari ya maji machafu huchukua maji hayo na kuyapeleka
kunakohusika.
Naye Naibu Waziri wa
Mazingira, Charles Kitwanga, amethibitisha kuruhusiwa kwa hoteli hiyo kurejesha
huduma zake kama kawaida baada ya kufanya marekebisho stahiki.
Post a Comment