Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam;
Mheshimiwa Balozi wa Serikali ya Jamhuri ya
Korea;
Waheshimiwa Wabunge na Madiwani;
Viongozi na Watendaji wa Serikali;
Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Mabibi na Mabwana:
Nakushukuru sana Mkuu wa Mkoa na viongozi
wenzako wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika tukio
hili muhimu la makabidhiano ya majengo yatakayotumika kama vituo vya kutolea
huduma ya afya kwa akina mama wajawazito na watoto katika Hospitali za Mnazi
Mmoja, Sinza na Mbagala Rangi Tatu. Pamoja na majengo hayo leo tutakabidhiwa pia
magari matatu ya wagonjwa na vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya kutolea huduma
kwenye vituo hivyo. Hii ni hatua kubwa katika jitihada za Serikli yetu za
kuboresha afya za akina mama na watoto katika mkoa wa Dar es Salaam. Sasa
tumeongeza uhakika wa kupata huduma zilizo bora zaidi kutoka kwenye vituo
hivi.
Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa
Tanzania na wananchi wote kwa ujumla, napenda kutoa shukrani za pekee kwa
Mheshimiwa Lee-Myung-bak, Rais wa Jamhuri ya Korea (Korea Kusini) pamoja na
serikali yake kwa zawadi hii kubwa waliyotupatia. Sina shaka ye yote kuwa vituo
hivi vitasaidia juhudi zetu za kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na
watoto. Hatuna neno zuri la kushukuru isipokuwa kusema asanteni sana.
Gharama zote za mradi huu, ikiwa ni pamoja na
majengo, vifaa na mafunzo kwa watoa huduma, ni shillingi bilioni 6.76 fedha
ambazo ni msaada kutoka Serikali ya Jamhuri ya Korea. Kabla ya msaada huu vituo
vilikuwa havina magari ya wagonjwa, huduma za uzazi, upasuaji, na maabara
zilikuwa hafifu na vyumba vya kutoa huduma vilikuwa vichache. Kwa jumla
mazingira ya kazi yalikuwa siyo mazuri sana na mambo yote hayo sasa
yamerekebishwa na huduma zinazotolewa ni bora kuliko ilivyokuwa mwanzo. Kwa
kweli marafiki zetu hawa wametuonesha upendo mkubwa na urafiki usio kifani. Bila
shaka wamethibitisha ule usemi usemao: Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa
kweli.
Ndugu wananchi;
Tangu nchi yetu ipate uhuru mwaka 1961 na
kufanya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964, Serikali yetu katika awamu zote
imefanya na inaendelea kufanya juhudi kubwa za kuboresha huduma ya afya ili
iwafikie Watanzania wengi zaidi na kwa gharama nafuu. Serikali ya Awamu ya Nne
ilipoingia madarakani mwaka 2005 iliendeleza juhudi hizo bila ajizi. Tulianza
kwa kuipitia upya Sera ya Afya ya Mwaka 1990 kwa lengo la kuihuisha ili iendane
na changamoto za sasa zinazoikabili sekta ya afya. Matokeo ya zoezi hilo ni
kuasisiwa kwa Sera ya Afya ya Mwaka 2007 na Mpango wa Miaka Kumi wa Maendeleo ya
Afya ya Msingi (2007-2017), kwa kifupi MMAM.
Ujenzi wa vituo hivi ni matokeo ya utekelezaji
wa Mpango huo kabambe wenye lengo kuu la kuongeza kasi ya uendelezaji na
uboreshaji wa huduma ya afya kwa kujenga na kuimarisha hospitali, vituo vya afya
na zahanati nchini. Kazi hiyo tumeianza na tunaendelea nayo vizuri. Tunataka
watu wasitembee zaidi ya kilomita tano kufuata huduma ya afya. Aidha,
tunaendelea kuboresha huduma zinazotolewa katika hospitali za Wilaya, Mikoa,
Rufaa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Tunafanya hivyo nchi nzima kwa
kushirikiana na wananchi, mashirika ya kijamii hasa ya dini, watu binafsi na
washirika wetu wa maendeleo waliopo ndani na nje ya nchi yetu.
Ndugu wananchi;
Wote mtakubaliana nami kuwa Mkoa wa Dar es
Salaam una changamoto ya pekee katika utoaji wa huduma ya afya kwa wakazi wa
Jiji. Mkoa wa Dar es Salaam una watu wengi kuliko mikoa yote nchini. Kuna
wagonjwa wengi kutoka hapa Mkoani na wengi huja ama wenyewe au kuletwa Dar es
Salaam kwa matumaini ya kupata huduma bora ya afya. Hali hii inasababisha
msongamano mkubwa katika hospitali za Serikali na za binafsi zilizopo Jijini
hapa.
Kwa kutambua ukweli huu na kwa nia ya kupunguza
adha wanayoipata wagonjwa, Serikali imekuwa inafanya jitihada kuongeza
hospitali, vituo vya afya na zahanati katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es
Salaam. Pia tunaongeza vifaa tiba, majengo ya kutolea huduma na idadi ya
wataalam wa afya. Kama nchi inayoendelea, uwezo wetu si mkubwa sana kutosheleza
mahitaji yote. Hiyo ndio sababu kubwa iliyonifanya mimi kuomba msaada Serikali
ya Jamhuri ya Korea nilipoitembelea nchi hiyo mwaka 2006. Bahati nzuri
wakakubali kutujengea majengo haya tunayokabidhiwa leo yenye maabara za kisasa
na kutuongezea vifaa tiba vya kisasa na magari matatu ya wagonjwa. Ndugu zetu
hawa pia wametupatia mkopo ambao tunajenga hospitali kubwa ya kisasa kule
Mloganzila, Kinondoni. Hospitali hiyo itatoa huduma na kutumika kufundishia
wanafunzi wa udaktari, uuguzi na taaluma nyinginezo za afya. Tumeamua
kukijengea Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili makazi yake mapya pale Mloganzila
ili kuongeza uwezo wa kufundisha wanafunzi wengi zaidi ili tujitosheleze kwa
mahitaji ya wataalamu wa afya.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa;
Ni kweli, ukilinganisha na tulivyokuwa huko
nyuma, kwamba tumepiga hatua nzuri kufikia Malengo ya Millenia ya Umoja wa
Mataifa ya kupunguza vifo vya watoto na akina mama vinayotokana na matatizo ya
uzazi. Idadi ya vifo vya watoto wachanga imepungua kutoka 99 mwaka 1999 hadi 51
mwaka 2010 na vifo vya walio chini ya miaka mitano imepungua kutoka 147 hadi 81
kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai. Kwa upande wa akina mama wajawazito idadi
ya vifo imepungua kutoka 578 hadi 454 kwa kila uzazi salama 100,000. Lakini
wastani wa watoto 562 (wachanga na walio chini ya miaka mitano) na akina mama
23 kufariki kila siku ni kubwa mno.
Tunaweza kupunguza zaidi vifo hivyo. Ni vifo
vinavyoweza kuepukika kwa kuongeza vituo vya kutolea huduma ya mama na watoto na
kuboresha huduma itolewayo kama tufanyavyo leo. Hivyo nawaomba wadau wote
wajitokeze kwa wingi kuunga mkono juhudi za Serikali za kupanua na kuboresha
huduma ya afya nchini. Hii itawafanya Watanzania wawe na afya bora na kuwezsha
nchi yetu kufikia malengo ya Umoja wa Mataifa ifikapo mwaka 2015. Ushirikiano
wa wadau wote ni muhimu sana katika kufanikisha azma hii. Hapa nina maana ya
Serikali, wananchi, watu binafsi na washirika wetu wa maendeleo kama tufanyavyo
leo. Tukiiachia Serikali pekee itachukua muda mrefu.
Napenda kutumia nfasi hii kurudia wito wangu
niliowahi kuutoa mwaka 2007 kwa Manispaa zote tatu za Dar es Salaam kujenga
hospitali na vituo vya afya vikubwa katika maeneo yao mbalimbali ili
kuzipunguzia mzigo hospitali zilizopo sasa za Temeke, Amana na Mwananyamala.
Hali kadhalika narudia wito wangu kwa Halmashauri za Miji ya Makao Makuu ya
Mikoa kujenga hospitali zao ili kuiacha hospitali ya Mkoa iwe ya Rufaa kwa
Wilaya zote za Mkoa husika. Mimi na wenzangu serikalini tunaahidi kutoa
ushirikiano kwa wadau wote ili kuhakikisha kuwa huduma ya afya nchini inazidi
kuboreka. Tunapenda kuona ahadi yetu ya maisha bora kwa kila Mtanzania ambapo
upatikanaji wa huduma bora ya afya ni sehemu muhimu, inaendelea
kutekelezwa.
Tutaendelea kuongeza fedha kwenye bajeti ya
serikali kwa ajili ya sekta ya afya ili vituo vya kutoa huduma viongezeke na
kumudu majukumu yao ipasavyo. Tutaendelea kuongeza nafasi za masomo kwa wataalam
mbalimbali wa afya ili idadi yao iongozeke na kuziba pengo lililopo. Kwa kufanya
hivyo mfumo wa utoaji wa huduma ya afya na miundombinu itaimarika zaidi na
afya za watanzania zitaboreka zaidi. Tuna imani kuwa vifo vya watoto na akina
mama vitapungua zaidi; magonjwa yatazidi kudhibitiwa na watu wengi watakuwa na
uhakika wa kuishi maisha marefu zaidi kuliko ilivyo sasa.
Ndugu wananchi;
Sasa majengo haya katika hospitali za Mnazi
Mmoja, Sinza na Rangi tatu yamekamilika. Nawaomba akina mama watumie vituo hivi
kupata huduma ya uzazi salama. Waache kujifungulia majumbani, ni hatari kwa
usalama wa mama na mtoto. Lolote linaweza kutokea. Vilevile, nawaomba madaktari,
wauguzi na watumishi wengine wa hospitali hizi watunze majengo haya na kutumia
vizuri vifaa tiba na magari ya wagonjwa kwani bila ya kufanya hivyo baada ya
muda si mrefu huduma zitadorora. Halmashauri zitenge fedha za kutosha za
uendeshaji wa hospitali, vituo vya afya na zahanati zake. Mazingira ya kazi
katika zahanati zetu hizo tatu yameboreshwa na vitendea kazi na vifaa
vimeongezwa. Hakuna sababu ya kushindwa kutoa huduma kwa kiwango cha hali ya
juu. Mshindwe wenyewe!
Kabla ya kumalizia napenda naishukuru tena
serikali ya Jamhuri ya Korea kwa msaada mkubwa waliotupatia. Balozi wao yupo
hapa. Namwomba atufikishie salamu na shukrani zetu nyingi kwa Rais na watu wa
Jamhuri ya Korea. Tunawashuru sana kwa ukarimu wao. Tunaomba tuendelee
kushirikiana pamoja katika kuboresha sekta ya afya na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa;
Ndugu wananchi;
Baada ya kusema maneno hayo machache, sasa nipo
tayari kufanya kazi iliyonileta ya kupokea majengo haya na kuyafungua
rasmi.
Asanteni kwa kunisikiliza.


Post a Comment