CAIRO, MISRI
SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limetoa ratiba
ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
Simba ya Tanzania, ambayo ni klabu
inayoaminika zaidi Afrika Mashariki kwa kufanya vizuri kwenye michuano ya
kimataifa inaanza Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kucheza na Recreativo do Libolo ya
Angola.
Azam FC, ambayo itacheza Kombe la Shirikisho
kwa mara ya kwanza mwakani imepangwa na vibonde Al Nasir Juba ya Sudan
Kusini.
Simba itaanza nyumbani jijini Dar es Salaam
Februari 17 na itarudiana na mabingwa hao wa Angola wiki mbili baadaye jijini
Luanda, Angola.
Simba ikivuka kigingi hicho cha mabingwa wa
Angola, itakumbana ana kwa ana na El Merreikh ya Sudan ambayo inataka kumnunua
Mrisho Ngassa wa Azam aliyekuwa akicheza Simba kwa mkopo.
Kwa upande wa Azam ambayo nayo itaanzia
nyumbani Dar es Salaam ikicheza siku moja kabla ya Simba yenyewe ikivuka hatua
hiyo ya kwanza itacheza na mshindi kati ya Johansens ya Sierra Leone dhidi ya
Barrack Y. C. II ya Liberia.
Kwa upande wa Zanzibar, Jamhuri itacheza na
St. Georges ya Ethiopia kwenye Ligi ya Mabingwa na ikivuka itakwaana na Djoliba
ya Mali.
Hata hivyo kwa upande wa Simba watakuwa
wakikutana na timu ambayo ilianzishwa mwaka 1942 na inayotumia Uwanja wa
Manispaa unaoitwa Calulo wenye uwezo wa kubeba mashabiki
10,000.
Mabingwa hao wa Angalo ambao katika historia
wametwaa ubingwa mara mbili tu mwaka 2011 na 2012 makao makuu yao yapo Libolo
katika Jimbo la Cuanza Sul.
Baadhi ya wachezaji wa timu hiyo
inayofundishwa na Kocha Zeca Amaral ni Mendes, Ze Kalanga, Yuri, Nuno Silva na
Andres Madrid.
Kocha wa timu ya taifa ya Rwanda, Sredejovic
Milutin 'Micho' alisema jana Jumatatu kuwa Simba imepangiwa timu
ngumu.
"Ni ratiba ngumu sana kwa Simba, wana nafasi
ndogo ya kusonga mbele. Hii timu ndio mabingwa wa Angola, ni wazuri sana,"
alisema Micho.
Simba ambayo makamu wake mwenyekiti Geofrey
Nyange 'Kaburu' amesisitiza kwamba kesho Jumatano watamtangaza Kocha Mkuu, bado
haijakamilisha usajili wake mdogo.
Simba na Azam ndizo zinazoiwakilisha Tanzania
Bara mwakani huku Yanga ikiwa haina nafasi yoyote ya kushiriki michuano mikubwa
zaidi ya Kombe la Kagame Julai nchini Sudan.


Post a Comment