Kamati ya Utendaji ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemteua Idd Mtiginjola kuwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF iliyoundwa kutokana na marekebisho ya Katiba
yaliyofanyika hivi karibuni.
Mtiginjola ambaye ni Wakili wa
kujitegemea ataongoza kamati hiyo yenye wajumbe watano ambayo sasa itakuwa
chombo cha mwisho kusikiliza rufani zinazotokana na uchaguzi wa TFF, na
wanachama wa TFF ambao hawatakubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya
TFF.
Kabla ya uteuzi huo, Mtiginjola
alikuwa mjumbe wa Kamati ya Nidhamu ya TFF inayoongozwa na Kamishna wa Polisi
(CP) mstaafu Alfred Tibaigana. Nafasi yake katika kamati hiyo na ile ya mjumbe
mwingine Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Shabani Semlangwa aliyefariki dunia
Julai mwaka huu zitajazwa hivi karibuni.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya
Rufani ya Uchaguzi ya TFF ambayo vinara wake (Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti)
wanatakiwa kitaaluma kuwa wanasheria ni Francis Kabwe. Kabwe ni Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu ya Tanzania.
Wajumbe wengine walioteuliwa na
Kamati ya Utendaji ya TFF katika kikao chake cha jana (Desemba 23 mwaka huu) ni
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi
wa Polisi (SACP), Mohamed Mpinga ambaye pia kitaaluma ni
Mwanasheria.
Wengine ni mshambuliaji wa
zamani wa timu ya Reli Morogoro, Profesa Madundo Mtambo ambaye kwa sasa ni
Mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichopo mjini
Morogoro, na mdau wa soka Murtaza Mangungu ambaye pia ni Mbunge wa Kilwa
Kaskazini
Post a Comment