Kanumba akiwa na Lulu
********
Kesi ya mauaji ya kutokukusudia inayomkabili msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael `Lulu’, imepokelewa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kusajiliwa kwa namba 125 ya mwaka 2012.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana mahakamani
hapo, kesi hiyo imepokelewa kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na inasubiri
kupangiwa Jaji na tarehe ya kuanza kusikilizwa.
Awali Lulu alikuwa akikabiliwa na mashitaka ya
kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba, kwa kukusudia lakini baada ya upande wa
mashitaka kukamilisha upelelezi alibadilishiwa mashitaka na kuwa kuua bila
kukusudia.
Kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Augustina Mmbando, katika hatua za awali na
Lulu hakuruhusiwa kujibu mashitaka yanayomkabili kwa kuwa Mahakama hiyo haina
mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Kwa mujibu wa sheria, kutokana na Lulu
kushitakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia, anaweza kupata dhamana.
Desemba 21 mwaka huu, Lulu alisomewa maelezo ya
kesi na ushahidi utakaotumika na upande wa mashitaka katika kesi hiyo, ambapo
Wakili wa Serikali Shedrack Kimaro alidai kuwa watakuwa na mashahidi tisa,
ushahidi wa nyaraka, ripoti ya uchunguzi wa hospitali na ramani ya eneo la
tukio.
Baadhi ya mashahidi watakaotoa ushahidi ni
pamoja na mdogo wa marehemu, Seth Bosco, Sofia Kassim, Daktari wa marehemu
aitwaye Pancras Kageigwa, Morris Semkwao na Esther Zephania ambaye ni askari
Polisi wa kituo cha Oysterbay, Kinondoni.
Katika kesi hiyo, inadaiwa kuwa Aprili 7, mwaka
huu nyumbani kwa Kanumba, Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam, Lulu alimuua bila
kukusudia msanii huyo nyota wa filamu nchini.
Chanzo -
HabariLeo
Post a Comment