Na Prince
Akbar wa Bin Zubeiry
MAHAKAMA Kuu
Kanda ya Dar es Salaam, leo asubuhi imemuachia kwa dhamana msanii wa filamu
nchini, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu, anayetuhumiwa kumuua msanii
mwenzake, Steven Kanumba ‘The Great’ baada ya kupitia vifungu vya
sheria.
Hatua hiyo
inakuja baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kubadilisha mashitaka ya
mwanadada huyo kutoka kesi ya mauaji hadi kuua bila
kukusudia.
Kutokana na
mabadiliko hayo, hata kama atashindwa kesi, Lulu hatapewa hukumu ya kunyongwa
kwa kuwa anatuhumiwa kwa kesi ya kuua bila kukusudia na kwa mujibu wa kifungu
cha sheria, anaweza kufungwa maisha au miaka
kadhaa.
Lulu
anakabiliwa na tuhuma za kumuua The Great Kanumba aliyefariki dunia, Aprili 7,
mwaka huu nyumbani kwake Vatican, Sinza Dar es
Salaam.
Lulu
aliyecheza filamu kadhaa na marehemu Kanumba waliyeibuka naye katika kundi la
Kaole, Magomeni, anadaiwa alimsukuma Kanumba nyumbani kwake Sinza Vatican,
ambaye pia inadaiwa alikuwa mpenzi wake.
Inaelezwa
baada ya tukio hilo, Lulu alikimbia nyumbani kwa Kanumba na mdogo wa The Great,
Sethi Bosco akaenda kuchukua gari kumpeleka kaka yake hospitali ya Muhimbili,
ambako alipofika iligundulika amekwishafariki
dunia.
Sethi
alikaririwa akisema kwamba siku ya tukio, Lulu alikwenda kwao usiku wa manane na
alipofika yeye (Sethi) alimuacha aongee na kaka yake. Sethi alidai aliwaacha
sebuleni akaingia chumbani kwake na baadaye akasikia wameingia chumbani (kwa
Kanumba).
Sethi
alisema baada ya muda alisikia kelele za dalili ya ugomvi na baada ya muda Lulu
alitoka kumwambia (Sethi) juu ya hali ya Kanumba kubadilika na kuwa
mbaya.
Sethi alidai
aliposikia hivyo akashituka na kwenda chumbani ambako alimkuta kaka yake katika
hali mbaya, povu likimtoka mdomoni hivyo kuchukua hatua ya kumuita daktari wake,
kabla ya kumkimbiza Muhimbili.
Lulu
alikamatwa asubuhi ya kuamkia siku ya tukio hilo, linalodaiwa kutokea usiku wa
manane na kuwekwa kizuizini katika kituo cha Polisi Oysterbay, Kinondoni, Dar es
Salaam, kabla ya kufikishwa mahakamani.
Uchunguzi wa
madaktari katika hospitali ya Rufaa ya Muhimbili ulisema pombe kali aina ya
Jackie Daniels ilisababisha kifo cha mwigizaji huyo.
Kifo cha
Kanumba kiliwaumiza wengi, kwani msanii huyo alikuwa mahiri na kipenzi cha
wapenzi wa filamu nchini.
Wapembuzi wa
mambo wanasema huu ni msiba wa kwanza kuteka hisia za watu wengi zaidi, tangu
kifo cha baba wa taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Oktoba mwaka
1999.
Post a Comment