Mahakama kuu ya katiba nchini Misri imesema haitasimamia mchakato wa kura ya maoni inayotarajiwa kuamua kuhusu katiba mpya
Tamko hilo linatolewa kufuatia kitendo cha waandamanaji kuizingira mahakama hiyo hivyo kuwazuia majaji kuingia ndani ya jengo la mahakama.
Mahakama hiyo imesema haiwezi kufanya kazi chini ya shinikizo na kwamba majaji hawatakutana hadi hapo watakapoona wanaweza kufanya kazi kwa uhuru.
Maandamano yaliyofanywa na wafuasi wa Rais wa taifa hilo Mohammed Mursi yalisababisha kufungwa kwa mahakama hiyo hapo jana na kuacha mzozo mkubwa baina ya majaji wakuu na vongozi wa ngazi za juu wa serikali.
Mamia ya watu wanaomuunga mkono Rais Mursi wameandamana nje ya mahakama usiku kucha kuamkia siku ambayo mahakama hiyo likuwa inataka kufanya kikao kutathmini kama bunge la katiba lililoandika rasimu ya mswada ni la halali au la. Chombo hicho kinaundwa na wanasiasa wengi kutoka chama cha udugu wa Kiislamu cha rais Mursi.
Uamuzi huo wa majaji unaonekana kuwa na athari kwa mpango wa Mursi wa kutaka kupitishwa wa katiba mpya kupitia kura ya maoni iliyopangwa kufanyika mwezi tarehe 15 ya Desemba. Majaji hao ndio wanaosimamia kura nchini Misri na Rais Mursi anawahitaji kutimiza malengo yale.