Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dkt. James Nzagi akitoa salamu kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sherehe za ufunguzi rasmi wa maonesho ya 13 ya Nguvu Kazi/Jua kali katika viwanja vya Musee Vivant mjini Bujumbura Burundi tarehe 5/12/2012.
Mary
Mwakapenda,
Afisa Habari, Wizara ya
Kazi na Ajira
Makamo Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Burundi, Mhe. Jean Kabura akikata utepe kufungua rasmi maonesho ya 13
ya Nguvu Kazi/Jua kali katika viwanja vya Musee Vivant mjini Bujumbura Burundi
tarehe 5/12/201.
Maonyesho ya 13 ya Nguvu
kazi/Jua kali yamefunguliwa rasmi leo katika uwanja wa Musee Vivant mjini
Bujumbura Burundi.
Akifungua maonesho hayo kwa
niaba ya Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Pierre Nkurunziza, Makamo Spika wa
Bunge la Burundi, Mhe.Jean Kabura amesema maonesho haya huandaliwa kwa ajili ya
kuendeleza shughuli za sekta binafsi na kuongeza ajira kwa
wajasiriamali.
Mhe. Kabura amesema kwamba
maonesho haya yanaendana na sera ya Afrika Mashariki ya kuendeleza viwanda
ambayo ilipitishwa na Wakuu wa Nchi Wanachama katika mkutano wao wa kilele mwaka
2011 mjini Bujumbura, Burundi.
Aidha ameongeza kuwa
maonesho haya yatawasaidia vijana kujikita katika sekta isiyo rasmi ili kuongeza
ajira kwa vijana na kupunguza na hatimaye kuondoa kabisa umaskini wa
kipato.
Amewaomba wafadhili
kuangalia bidhaa za wajasiriamali ili kutafuta njia za kuwasaidia kuongeza ubora
wa bidhaa hizo na kuwatafutia masoko.
Mhe. Kabura amewashukuru
waandaji wa maonesho kwa maandalizi mazuri na kuweza kufanikisha shughuli nzima
ya uzinduzi.
Akitoa salam kwa niaba ya
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi wa Tanzania nchini Burundi,
Dkt. James Nzagi ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Burundi kwa maandalizi
mazuri ya maonesho na kwa mapokezi mazuri kwa washiriki wote waliofika
Bujumbura.
Aidha amewashukuru
watumishi wa mipakani kwa ushirikiano waliouonesha kwa wajasiriamali wa Tanzania
kupita kwa usalama na mali zao bila kusumbulia na kusema kuwa hii in ishara ya
kuonesha ushirikiano ulio imara katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Dkt. Nzagi amesema kuwa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayachukulia maonesho haya kama
njia ya kubadilisha Tanzania kuwa taifa la uchumi wa kati na unaoendeshwa na
viwanda.
Ameongeza kuwa kwa
kuzingatia umuhimu wake kwa watanzania, Serikali imeendelea kuwasaidia
wajasiriamali wa sekta isiyo rasmi kuweza kushiriki maonesho haya ili kukuza
shughuli zao na kuimarisha ajira zao.
Katika maonesho haya,
Tanzania ilipewa nafasi 185 za wajasiriamali kushiriki. Wajasiriamali 87 ndio
walioweza kushiriki wakiwa na bidhaa mbalimbali ambazo ni pamoja na nguo za
batiki, vyakula vya kusindika, bidhaa za ngozi, dawa za asili, dagaa wa
kukaushwa, mafuta ya ubuyu, vikapu vya kushona n.k.
Maonesho ya 13 ya Nguvu
Kazi/Jua Kali ya Afrika Mashariki hufanyika kila mwaka kwa mzunguko katika kila
Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kufunguliwa rasmi mwezi
Novemba, 1999 mjini Arusha Tanzania. Maonyesho hayo kwa mwaka huu yanafanyika
nchini Burundi ikiwa ni mara ya kwanza maonesho haya kufanyika nchini
humo.
Maonesho hayo yana lengo la
kukutanisha wajasiliamali wadogo kwa ajili ya kubadirisha uzoefu, kuwajengea
mtandao wa kibishara, kukuza vipaji vyao pamoja na teknolojia.
Post a Comment