Amina Chifupa |
TAKRIBAN miaka 10 sasa tangu mwaka 2002 hadi mwaka
huu 2012, Tanzania imekuwa ikishuhudia nyota wake katika tasnia mbalimbali
wakipoteza maisha wakati nyota zao bado ziking’ara.
Vifo vya nyota hao licha ya kuacha mapengo yasiyozibika,
bado vimeendelea kugonga vichwa vya watu, vikiacha maswali na pengine yatima
katika familia zao.
Katika makala haya mwandishi wetu amejaribu kuainisha
baadhi ya wasanii wa fani tofauti, waliofariki kipindi ambacho nyota zao
ziking’ara na kupendwa na mashabiki.
SHARO MILONEA
Namna ya uigizaji
wake katika hali ya kitanashati na mikogo ya kipekee inayoendana na lugha ya ‘kisharobaro’, ilimfanya msanii
huyo kupoteza jina lake halisi ambalo ni Husseni Ramadhani Mkieti.
Ilikuwa vigumu kumsaka msanii huyo kwa jina lake halisi,
lakini ilikuwa ni rahisi kumpata iwapo ungemtafuta kwa jina la Sharo
Milionea.
Msani huyo alibadilisha jina lake la awali na Sharobaro na
kuwa Sharo Milionea, baada ya kuingia mzozo na msanii mwenzake, Bob Junior
ambapo kwa kuepusha wasikosane, aliamua kutumia jina hilo jipya lililokolea na
kumvaa kuliko maelezo.
Katika mahojiano mbali mbali Sharo Milionea aliwahi
kunukuliwa akisema kuwa alipenda kuigiza kama brazameni akitumia maneno kama
'usinichafue meen', 'nimechoka kuimba meen' kamata 'mwizi meen' ili
kujitofautisha na wasanii wengine nchini, akiiga staili ya msanii aliyekuwa
akimhusudu, Will Smith.
Sharo Milionea, aliyekuwa mahiri kwa kuigiza filamu na
uimbaji wa muziki wa kizazi kipya, alikiri kwamba karibu kila jambo katika sanaa
yake, ina chembe ya nyota huyo wa
Kimarekani anayetamba kwenye muziki na filamu ulimwenguni.
Mkali huyo aliyewahi kutamba na nyimbo kama 'Nahesabu
Namba','Tusigombane', 'Chuki Bure', 'Hawataki', 'Sondela', 'Tembea Kisharobaro'
ambaye pia alikuwa mbioni kuachia nyimbo nyingine za 'Vululuvululu' na
'Changanyachanganya', amefariki Jumatatu ya Novemba 26 saa mbili usiku maeneo ya
Maguzoni Muheza mkoani Tanga kwa ajali ya gari akitokea Dar es Salaam.
AMINA CHIFUPA
Nyota huyu alizaliwa Mei 20 mwaka 1981 na kufariki Juni 26
Juni, 2007 baada ya kuugua. Kifo chake kilitokea siku chache kabla ya kikao cha
Bunge la Bajeti, akiwa mbunge.
Chifupa alipata
umaarufu wa kuwa Mbunge kijana mwenye umri mdogo ambapo alitikisa kwa kula kiapo
mbele ya Bunge katika harakati za
kuwamata wauza na watumiaji wa madawa ya kulevya.
Ndani ya miezi 18 alishikilia bango msemo wake wa kutetea
vijana, kupunguza rushwa na pia elimu kwa watu
wote.
Kabla ya hapo alikuwa ni mtangazaji maarufu wa redio ya Clouds FM.
JAMES DANDU
Maarufu kama 'Cool James', Mtoto wa Dandu Mwanamuziki aliyezaliwa 1970 katika Jiji la Mwanza.
Alianza shughuli za muziki mwaka 1983, lakini album yake ya kwanza aliitoa
1986. Alijiunga na mwanamuziki Andrew
Muturi kutoka Kenya na kuanzisha kundi la Swahili Nation ambapo walifanikiwa
kutoa single iliyoitwa Mapenzi.
Mwaka 1990 alijitoa kundi hilo na kuanzisha kampuni yake
Dandu Planet Mwaka 1993 akiwa na Black Teacher. Alianzisha kampuni nyingine
Dandu Entertainment na kufanya kazi kadhaa kupitia wanamuziki wa Afrika
Mashariki.
Dandu hatasahaulika kwa wale wanaofahamu chanzo cha tuzo za
kila mwaka za muziki za Kilimanjaro Music Awards ambazo zilianza kwa jina la
Tanzania Music Awards (TAMA).
Alifariki katika ajali ya gari tarehe 27 Agosti 2002 akiwa
na umri wa miaka 32 huku kibao chake cha 'Mtoto wa Dandu' kikishika chati ya juu
vituo mbali mbali vya radio.
ISSA KIJOTI
Nyota yake ilizima ghafla kufuatia ajali ya gari
iliyogharimu maisha yake na wasanii wenzake, iliyotokea Machi 21 mwaka 2011,
maeneo ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, mkoani Morogoro.
Kijoti alipoteza maisha pamoja na wasani wengine 13 wa
kundi la Five Stars tukio ambalo
litabaki kuwa historia.
Kijoti alifariki akiwa na umri wa miaka 26 wakati nyota
yake inang'aa hasa baada ya kupata umaarufu mkubwa akiwa na kundi hilo baada ya
kutoa kibao cha 'Wapambe Msitujadili'.
STEVE KANUMBA
Aprili 10 mwaka huu, Tanzania ilimpoteza mmoja wa wasanii
wake mahiri katika tasnia ya filamu, Steven Kanumba.
Kanumba alifariki alfajiri ya Jumamosi Aprili 7, akiwa na
umri wa miaka 28, baada ya kile kilichodaiwa kuwa ugomvi wa kimapenzi na rafiki
yake wa kike, ambaye pia ni mwigizaji, anayefahamika kwa jina Elizabeth Michael,
maarufu ‘Lulu’.
Umati wa watu wakiwamo
Rais Jakaya Kikwete, maoafisa waandamizi wa Serikali, wasanii na watu wa
tabaka mbambali walihudhuria msiba huo, ambapo pia walikusanyika katika viwanja
vya Leader’s kutoa heshima zao za mwisho kabla ya mazishi yaliyofanyika makaburi
ya Kinondoni.
Idadi hiyo kubwa inayoingia katika rekodi za pekee ni ya
pili kutokea baada ya umati uliofurika wakati wa kuaga mwili wa Baba wa Taifa,
Mwalimu Julias Kambarage Nyerere.
Huo ni ushahidi tosha wa umaarufu mkubwa aliokuwa nao
Kanumba, ambaye hadi mauti yalipomkuta aliweza kutengeneza zaidi ya filamu 40
akishirikiana na wasanii mbali mbali ndani na nje ya nchi na hasa Nigeria.
PATRICK MAFISANGO
Alikuwa mchezaji wa klabu ya Simba ya Jijini Dar es Salaam,
aliyezaliwa Machi tisa mwaka 1980 na kufariki Mei 17 mwaka 2012 kwa ajali ya
gari iliyotokea maeneo ya Tanzara, alipokuwa akijaribu kumkwepa mwendesha
pikipiki, ambapo gari lake lilipoteza mwelekeo, kuacha njia na kutumbukia
mtaroni na kugharimu maisha ya mchezaji huyo, ambaye pengo lake hadi sasa Simba
wameshindwa kuliziba.
Mafisango aliagwa kwenye viwanja vya Chang'ombe na kwenda
kuzikwa kwenye Kijiji cha Lembe Kinshansa nchini Kongo.
Kifo chake kiliacha taaruki kubwa hasa kwa wapenzi wa soka
kwani alikuwa ni mchezaji wa aina yake Simba, hakuwahi kuwa nahodha wa timu kama
kwenye timu yake ya APR ya Rwanda na Amavubi, lakini alikuwa ni zaidi ya nahodha
kwani aliweza kuhamasisha wenzake kucheza bila kuchoka na kutokata tamaa hata
pale Simba inaposhambuliwa na timu pinzani na au hata kufungwa.
VIVIAN NA COMPLEX
Ilikuwa ni saa tatu asubuhi ya Jumapili, Agosti 21 mwaka 2005 ambapo nyota wawili wa muziki
nchini waliokuwa wakipendwa sana, Saimon Sayi maarufu kama Complex ambaye
kipindi hicho alikuwa akifanya kazi na studio ya Aigies Records na mtangazaji wa
Clouds FM na rapper Vivian Tillya walipofariki kwa ajali ya gari eneo la Mbwewe,
mkoani Tanga.
Wasanii hao ambao walikuwa wapenzi, walikuwa safarini
kutoka Morogoro kwenye tamasha la Fiesta iliyopewa jina la ‘Moto Zaidi’
wakielekea jijini Arusha kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya ndoa ya wazazi wa
Vivian.
Siku hiyo pia Vivian alikuwa akienda kumtabulisha Complex
kama mchumba wake kwa wazazi wake.
STEVE 2K
Alitamba na kundi la Mambo Poa, ambalo lilikuwa likisifika
zaidi kwa kuimba nyimbo zake kwa mtindo wa mduara, rap, zouk na raga. Kundi hilo
lilikuwa likiundwa na wasanii Steven Waymark ‘Steve 2K’, John Mjema wote ni
marehemu pamoja na Rashid Mustafa ‘Spider’.
Kupitia nyimbo za wasanii hao kama ‘Shani’, ‘Mimi Siyo
Mwizi’, ‘Nilikupenda’, ‘Spare Tyre’, ‘Kasuku’, ‘Mama Afrika’ na nyinginezo,
kundi hilo lililoanzishwa mwishoni mwa miaka ya 1990, liliweza kujipatia
umaarufu mkubwa nchini.
Steve 2K aliuawa kwa kuchomwa kisu na mtayarishaji, Castol
mwaka 2004 baada ya kilichoelezwa kuwa ni kutofautiama, hivyo kuzima nyota ya
msanii huyo ambayo kwa wakati huo iking'aa.
Mwaka 2008, msanii mwingine, John Mjema naye alipoteza
maisha baada ya kujinyonga huku sababu za kitendo hicho zikiwa kitendawili bado.
Post a Comment