Na
Emmanuel J. Shilatu
Wakati tunapata uhuru wetu mwaka 1961
kutoka kwa Waingereza kila Mtanganyika alikuwa na maana yake kichwani ya
kuelewa nini maana ya uhuru. Wapo walioamini kuwa huo ndio utakuwa mwisho wa
ubaguzi wa rangi, hadhi, kabila uliokuwa ukifanywa na Wakoloni; wengine
waliamini kupata uhuru ni kufanikiwa kuziondoa tawala mbovu, nyonyaji na za
kidhalimu za Wakoloni.
Licha ya mawazo mazuri waliyokuwa nayo
baadhi yao, lakini kwa upande wa mwasisi mwenyewe wa uhuru wetu alikuwa na
mtazamo tofauti kabisa na zilivyokuwa mawazo ya watu. Yeye Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere alikuwa na maana ya kipekee kabisa juu ya dhana nzima ya
uhuru.
Kwa upande wa Baba wa Taifa letu
Mwalimu Nyerere aliamini na kusema ya kuwa “tumefanikiwa kuwaondoa Wakoloni na
hivyo tupo huru. Na uhuru maana yake ni kazi”. Mwisho wa kunukuu.
Hapa Mwalimu Nyerere alikuwa na maana
ili tuweze kupiga hatua kimaendeleo ni lazima tuutumie huu uhuru wetu vilivyo
katika kupiga hatua kimaendeleo kupitia kufanya kazi kwa bidii na maarifa yetu
yote ili kuleta maboresho ya kina katika Nyanja zote zile za kimaisha yaani
uchumi, kijamii na kisiasa. Bila ya kufanya kazi kwa bidii, uhuru wetu ni sawa
na mzoga.
Na ndio maana Mwalimu Nyerere kama
kiongozi alianza kwa kuonyesha mfano wa dhahiri wa kuanzisha mapambano kwa
vitendo dhidi ya maadui zetu watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini.
Sehemu kubwa ya mafanikio yake
yalitokana ama ni kupitia kuanzisha maazimio, mashirika, kauli mbiu na sera
mbalimbali. Hayo yote aliyafanya kwa vitendo zaidi na si porojo, lawama,
maandamano, wala manung’uniko.
Pia Mwalimu Nyerere alikuwa na falsafa
ama dhana ya kimaendeleo ambapo aliamini maendeleo sahihi hayawezi yakapatikana
nje ya uwepo wa mambo makuu manne ambayo ni “watu”, “ardhi”, “siasa safi” na
“uongozi bora”.
Naam!! “Watu” ni kiungo kimoja wapo
kikuu cha hakikisho la maendeleo chanya yeyote yale ndani ya familia, jamii ama
Taifa kwa ujumla wake. Mathalani, endapo tutakuwa na miundombinu bora ni watu
ndio wamechangia uwepo wake; ama kama tutakuwa na mazao ya kutosha kwa ajili ya
chakula, biashara na kiada basi ujue ni watu wameweka jitihada za kutosha.
Halikadhalika kama kuna amani na
utulivu nchini basi ujue ni watu wamechangia hilo. Jamani, hata Wahenga walisema:
“usione vyaelea, ujue vimeundwa” , na waundaji wenyewe ni Wananchi (mimi, wewe
na Yule).
Licha ya uwepo wa utajiri wa nguvu kazi
takribani Milioni 45 lakini bado watu hao hao ndani ya jamii wanachojua ni
utegemezi pekee. Kivipi?
Kwa jinsi tuanavyoishi utadhani
tunawangojea baadhi ya watu kutoka nje ili waje watuletee maendeleo yaani
imefika kipindi kwa mtu hata kutandika kitanda chake mwenyewe anacholalia
imekuwa ni kazi kubwa kwake.
Kikubwa ambacho kinaonekana ni kujikita
mizizi ya dhana nzima ya kibaguzi iliyojengeka akilini ama kwenye mitazamo ya
watu ambapo tumediriki kuwaachia viongozi pekee huku tukijiengua katika kapu la
dhana ya neno “serikali” wakati kiuhalisia na kimaantiki na Wananchi nao pia
wapo.
Ni kweli kabisa kwamba Serikali ni
chombo cha utawala kilichoshika dola ama nchi kwa lengo la kuwaletea maendeleo
Wananchi. Na wanaoiwezesha ama kuipa mamlaka hayo Serikali ni Wananchi. Bila ya
watu hakuna serikali na pia Serikali haina uhalali wa kuwepo bila ya kuwepo kwa
watu.
Na kundi lingine linalounda serikali ni
viongozi. Hivyo serikali ni muunganiko kati ya viongozi na Wananchi. Daima na
tena ni dhambi kubwa sana kuwatenganisha makundi haya (Wananchi na viongozi)
katika chungu hiki Serikali.
Wananchi siku hizi wamekuwa
washadidiaji wakubwa wa siasa na bila ya wao kujitambua ya kwamba hutumia muda
mwingi sana kushindia na kulalia katika dimbwi la porojo za kisiasa bila ya
kujibidiisha. Maendeleo yatapatikanaje bila ya sisi wenyewe kujishughulisha?
Utakuta vijana walio wengi kutwa
wanashinda kwenye kucheza “pool table” na kukaa vijiweni tu; Wazee ama akina
Baba nao kutwa wanacheza “bao” ama “draft” tu; na akina Mama nao kila kukicha
wapo vibarazani wakisutana na kupashana umbea tu. Hayo ndio maisha ya kila siku
ya baadhi ya wanajamii ya kutokupenda kufanya kazi kwa bidii.
Mwananchi huyo huyo anaitegemea
Serikali ije impatie fedha mikononi bila ya yeye kujishughulisha kwa kufanya
kazi yeyote ile ya kumpa kipato. Hakuna Serikali yeyote ile duniani inayoweza
kuwapatia wananchi wake pesa lukuki bila ya wao kujishughulisha.
Kama hauamini, jaribu kufanya utafiti
katika nchi zilizoendelea utakubaliana nami kuwa hakuna Taifa lolote lile lenye
raia wasiojibidiisha kwa kutegemea mteremko kutoka kwa Serikali zao. Yatazame
mataifa kama ya Marekani, Uingereza au Urusi wakazi wake wanavyotambua ya kuwa
thamani ya pesa yao na uchumi wa nchi unategemea zaidi ni kwa jinsi gani watu
wa ndani (wao wenyewe) wanavyozalisha mali.
Lakini sie hatujitambui na tupo bize
kwa kujiteketeza na porojo kila uchwao. Hapa tumesaliti Mwalimu Nyerere na
alivyoamini maana ya uhuru kuwa ni kufanya kazi kwa bidii, umasikini
hautatuacha kweli? Nani wa kulaumiwa ni serikali ya CCM na viongozi wake ama ni
sisi Wananchi?
Hii yote inatokana na jamii kuziasi
mitazamo miongozo na falsafa za Mwalimu Nyerere (mathalani ile ya “Uhuru ni
kazi”) hali inayosababisha kiwango cha idadi ya watu maskini kuzidi kukua
nchini licha ya kujaariwa rasilimali na mali za asili kwa kuyachakachua
maendeleo yetu wenyewe. Kisa? Porojo kutawala maisha yetu.
Tusiishie kuwalaumu tu Viongozi wetu
kila kukicha huku tukisahau jinsi sisi tulivyo wavivu sana wa kupindukia.
Watanzania tulio wengi hatupendi kufanya kazi kwa bidii na kwa ubunifu.
Watanzania tulio wengi hatupendi njia nyoofu na sahihi badala yake tunapenda njia
ya mkato ya kujipatia vipato vyetu. Watanzania wengi tunapenda sana kufanya
madili, ama “michongo” kama wanavyoita watoto wa mjini.
Kwenye salam zao ama maongezi mengi ya
Watanzania ni nadra sana kukosa kusikia maneno kama vile “mambo mengine niaje,
ishu vipi ama madili yakoje”. Ni dhahiri kuwa hapa inatafutwa njia ya mkato
katika maisha. Hali hii huzaa matokeo endelevu mabovu ndani ya jamii kama vile
utapeli; ujambazi; ongezeko la mihadarati na madawa ya kulevya; mauaji ya
maalbino na vikongwe; pamoja na uchafu ama uozo mwingine kadha wa kadha
unaofanana na huo.
Chanzo haswa cha uwepo wa utafutaji
mambo kwa njia ya mkato halijasababishwa na Viongozi ndani ya Serikali bali
msingi wake mkuu ni Watu tulio wengi kutaka matokeo chanya yenye faida na
matunda kwa haraka na hata pia kukata tama ya kimaisha kwa haraka zaidi
kutokana na kujinyima fursa ya uvumilivu na ustahimilifu ndani yetu.
Mapambano ya maisha ni sawa na vita
kali ambapo si tu jukumu la viongozi bali hata nasi Wananchi tuna wajibu mkubwa
wa kufanya kazi kwa bidii na si kulalama tu kila kukicha.
Kuna usemi mmoja unaosema
“Wanaofanikiwa zaidi ni wale walioshindwa mara nyingi” Je utashindwaje, kama
hujajaribu mara nyingi? Je mafanikio katika maisha yanapatikana kwa mara moja
tu? Haya ni maswali muhimu na ya msingi sana kwa Watanzania, kujiuliza.
Ifike mahali tujitambue ya kwamba
kelele, tuhuma, lawama, dharau kwa viongozi wetu hazitatusaidia endapo sisi kwa
sisi hatujaamua kujibidisha ipasavyo. Utakuta ndani ya jamii fulani tupo zaidi
ya watu laki mbili lakini tunamtegemea kiongozi mmoja tu awe ni Mbunge ama
Diwani ili aweze kutuletea maendeleo. Endapo sisi tulio wengi tumeshindwa kuwa
kitu kimoja wenye nia moja ya umoja, mshikamano na tukaamua kwa dhati kujiletea
maendeleo; Je, kiongozi mmoja pekee atawezaje?
Ndugu zangu, kwanini alaumiwe dobi
kutakasa kaniki wakati tunajua rangi ya kaniki? Ni lazima tutambue ya kwamba
sisi raia pia tunahusika vilivyo na huu umaskini wetu na si vyema kuwasukumizia
mzigo wote wa lawama viongozi wetu pekee. Watanzania tulio wengi tunapoteza
muda mwingi kwa kukaa vijiweni, kushabikia siasa tu, kupiga soga na kucheza bao
muda wote. Je, tukiamua kujishughulisha kwa kuutumia muda huo ipasavyo
tungekuwa wapi kimaendeleo hivi sasa?
Waswahili walisema usimuhadithie mtu
ndoto yako uliyoota jana usiku lakini hapa ni kinyume kwani siri tunasema na
bayana tunaambizana. Binafsi huwa Napata ukakasi pindi nionapo Serikali ina
sera na majukumu lukuki lakini Watanzania tulio wengi hatushiriki vyema na hata
hatutimizi wajibu wetu kwa wakati. Mwenye jukumu la kulifuatilia Taifa letu kwa
ukaribu na utendaji ni serikali pekee ama na Wananchi pia? Je, kwa uwajibikaji
huu, maisha bora kwa kila Mtanzania yatapatikana kweli?
Mara nyingi sera tulizonazo zinategemea
zaidi umoja, mshikamano, ushirikiano na nia ya dhati ya uwajibikaji wa pamoja
kiutekelezwaji. Kamwe maisha bora kwa kila Mtanzania hayaji kwa kuota au kupiga
soga ama kwa kungojea mpaka uone Tanzania (nchi yako) imekufanyia nini na
badala yake ujiulize wewe mwenyewe umeifanyia nini Tanzania?
Kuna wanamapinduzi, wanaharakati na
watu mashuhuri wengi tu hapa Duniani ambao hawakungoja mpaka waone nchi zao
zimewafanyia nini na badala yake walijiuliza wamezifanyia nini nchi zao?
Mwalimu Julius Nyerere, Nelson Mandela,
Martin Luther King Jnr, Kwame Nkurumah, Chifu Mkwawa ni baadhi tu ya
Wanaharakati na wakombozi wa kweli dhidi ya Uhuru na ubaguzi wa ngozi nyeusi
ambao milele na milele watabakia kuwa ni mashujaa maarufu wa ulimwengu. Jiulize
mwenyewe wewe je utakumbukwa, ama tutajivunia nini kutoka kwako? Je, ni kwa huo
ugoigoi wako ama kwa uwajibikaji wako?
Tuache uvivu na tujitume vilivyo kwa
kuchangamkia fursa na Baraka tulizojaaliwa. Mungu ametujaalia wingi wa ardhi
yenye rutuba ifaayo kwa kilimo, misitu, wanyama pori na vyanzo vingi vya
kujiletea maendeleo.
Tanzania isiyo na maradhi inawezekana;
Tanzania yenye uchumi imara mpaka kwa Wananchi wake inawezekana; Tanzania yenye
huduma bora zaidi za kijamii inawezekana; Hakika Tanzania yenye maisha bora
zaidi pia inawezekana. Hii itawezekana tu endapo kila mmoja wetu atatimiza wajibu
ipasavyo kwake na kwa Taifa lake.
Ndugu zangu, ndani ya miaka 51 tangu
tupate uhuru wetu tumezitumia vipi fursa na Baraka tulizojaaliwa kwa manufaa
yako, jamii inayokuzunguka na kwa Taifa lako kwa ujumla?
0717 488 622
Post a Comment