Nakusudia kutumia kifungu cha 10 cha Sheria ya ya Haki, Kinga na
Madaraka ya Bunge kutaka nakala ya mkataba wa mkopo wa masharti kiasi cha Dola
za Marekani bilioni 1.225 (shilingi trilioni 1.86) kutoka China.
Nitataka pia nakala za mikataba wa mradi wa miundombinu ya gesi
asilia ambayo itahusisha ujenzi wa mitambo ya kusafishia gesi asilia katika
mikoa ya Lindi na Mtwara na ujenzi wa bomba kuu la kusafirishia gesi asilia la
inchi 36 kutoka Mtwara kupitia Lindi, Pwani hadi Dar es Salaam lenye umbali wa
kilometa 532.
Hii ni kwa sababu mpaka sasa Wizara ya Nishati na Madini
haijatekeleza pendekezo nililowasilisha bungeni tarehe 27 Julai 2012 kwamba
kutokana na unyeti wa mradi huo kwa mustakabali wa nchi na maisha ya wananchi wa
sasa na baadaye Serikali ilipaswa kuwasilisha bungeni na kuweka wazi kwa umma
mkataba wa mradi husika.
Pendekezo hilo lingeliwezesha Bunge kuishauri na kuisimamia serikali
kuanzia katika hatua za awali kuhakikisha kwamba maslahi ya taifa yanalindwa
katika hatua zote na pia wananchi wananufaika kutokana na fursa za uwekezaji huo
mkubwa.
Kutokana na Serikali kutokuzingatia pendekezo hilo na badala yake
Rais Jakaya Kikwete kufanya uzinduzi wa mradi huo tarehe 8 Novemba 2012 Mkoani
Dar es salaam huku usiri ukiendelezwa malalamiko yameanza kujitokeza katika
maeneo ya mradi husika hususan katika Mkoa wa Mtwara.
Aidha, Serikali irejee katika mapendekezo niliyotoa bungeni na kutoa
maelezo kwa umma ya sababu za bomba hilo kujengwa kutoka Mtwara mpaka Dar es
salaam na kueleza kwa uwazi manufaa ya mradi huo na miradi mingine inayopaswa
kutekelezwa katika mikoa ya Kusini kwa maendeleo ya wananchi
husika.
Tarehe 27 Julai 2012 nilieleza bungeni kuwa pamoja na ujenzi wa
mitambo miwili ya kusafishia gesi asili Mnazi Bay na Songo Songo kama sehemu ya
mradi huo; Serikali inapaswa kueleza ni miradi ipi inayoambatana na mradi huo
ambayo imepangwa kuwanufaisha wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ikiwemo
kuharakisha utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa MW 300 Mtwara na MW 230
wa Somanga Fungu (Kilwa).
Kwa upande mwingine, utekelezaji wa mradi huo unaendelea bila kuwa na
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo ingepaswa kuishauri na
kuisimamia Serikali hivyo ni muhimu Spika wa Bunge akachukua hatua kutokana na
barua niliyomwandikia mwanzoni mwa mwezi Oktoba 2012 ambayo mpaka sasa
haijajibiwa.
Ikumbukwe kwamba katika barua hiyo nilitoa mwito kwa Spika
atumie madaraka na mamlaka yake kutangaza kwa umma kamati nyingine ya
kudumu ya Bunge itayoshughulikia nishati na madini ikiwemo masuala ya gesi asili
kwa sasa kufuatia hali tete na tata kuhusu sekta ndogo ya gesi asilia nchini na
kwa kuzingatia umuhimu na unyeti wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi na maisha
ya wananchi.
Pamoja na mambo mengine nilipendekeza Spika aelekeze kamati hiyo
kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge ya mwaka 2011
kuhusu Sekta Ndogo ya Gesi Asili ikiwemo juu ya hatua iliyofikiwa katika
kushughulikia tuhuma za ufisadi, madai ya mapunjo ya fedha za mauzo ya Gesi
asili na hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya sera, mpango mkakati na sheria
ya gesi asili.
Hatua hii ni muhimu kwa sasa kwa kuwa hata baada ya uamuzi wake
kuhusu tuhuma za rushwa kwa wajumbe wa Kamati husika, Spika hakueleza hatma ya
Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa hali ambayo imeacha ombwe la uongozi na
usimamizi wa kibunge (Parliamentary Oversight) kwenye sekta hizi nyeti kwa
uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
26/12/2012
Post a Comment