**************
WAZIRI wa Nishati na Madini,Profesa Sospeter Muhongo amewatoa wasiwasi Watanzania kuhusu utafiti na uchimbaji wa madini ya urani huku akiwaponda wanaharakati kwa madai kuwa wanapotosha Umma.
Hivi karibuni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),kiliitaka Serikali kusitisha shughuli za utafiti na uchimbaji wa madini ya urani, ili kunusuru afya za Watanzania. Pia, Serikali ya Ujerumani kwa kupitia Mtandao wa Uchimbaji wa Madini hayo, iliitaka Serikali ya Tanzania kufikiri na kufanya tathmini ya kina kuhusu madhara ya madini hayo ambayo yanadaiwa kuwa na uwezo wa kuathiri vizazi hadi vizazi.
Hata hivyo Profesa Muhongo akizungumza katika kipindi cha ‘Kumepambazuka’ cha Radio One Stereo jana alikosoa taarifa hizo huku akisema huo siyo msimamo wa Serikali ya Ujerumani.
Alisema utafutaji na uchimbaji wa madini ya urani, siyo kitu kigeni duniani na kwamba Tanzania siyo nchi ya kwanza kuchimba madini hayo.
“Ndugu zangu Watanzania lazima tufahamu tusiendelee kupotoshwa. Machimbo makubwa kabisa ya urani duniani yako katika nchi ya Kazakhstan, nchi ya pili ni Canada inayotoa zaidi ya asilimia 18, nchi ya tatu ni Australia inayotoa asilimia 11… nchi ya nne ni Namibia,.. wanatoa asilimia 8.4…kama Namibia wanachimba kwa nini Tanzania tusichimbe?” alihoji Profesa Muhongo na kuendelea:
“Nchi ya tano ni Niger inayotoa asilimia 7.8… nchi ya nane ambayo ni muhimu ni Marekani wanatoa asilimia 3.1 ya urani. Nchi ya 10 ni China, nchi ya 11 ni Malawi jirani zetu wanatoa asilimia 1.2 ya urani ya dunia nzima na nchi ya 12 ni Afrika Kusini wanatoa asilimia 1.1. Kwa hiyo tukichukua tu nchi za Afrika, Namibia, Niger, Malawi, South Africa, Malawi wanachimba Tanzania tusichimbe, je, Watanzania tunajua tunachokishabikia?”
Akizungumzia maandalizi ya uchimbaji huo, Profesa Muhongo alisema kuwa kampuni zinazojiandaa kuchimba urani, zimepitia taratibu zote, ikiwa ni pamoja na kupata cheti cha mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, taratibu za mionzi na kupata kibali cha tume ya mazingira.
Kuhusu madhara yaliyotokea nchini Japan mwaka jana baada ya mitambo ya nyuklia kulipuka kutokana na tufani, alisema kuna tofauti kati ya madhara hayo na uchimbaji unaotarajiwa kufanyika nchini.
“Madhara yaliyotokea nchini Japan ni tofauti na uchimbaji unaofanyika hapa. Kule ilikuwa ni Tsunami na matetemeko yaliyovunja nyuklia…ilikuwa ni urani ambayo tayari imeshaanza kutumika,” alisema na kuongeza:
Kuhusu taratibu zilizochukuliwa katika uchimbaji huo, Profesa Muhongo alisema taratibu zote za kimataifa zitafuatwa ikiwa ni pamoja na kulinda mazingira na kupima kiwango cha mionzi na hatari yake wakati wa uchimbaji.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu athari zitakazotokana na uchimbaji wa madini hayo nchini hivi karibuni, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Lulu Urio alisema, ingawa kuna faida ambazo taifa litazipata kama fedha za kigeni, bado madhara yanayotokana na uchimbaji wa madini hayo ni makubwa kuliko inavyofikiriwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtandao wa Utafiti wa Madhara ya Uchimbaji wa Madini hayo nchini Ujerumani, Gunter Wippel alisema hadi sasa nchi hiyo imetumia zaidi ya Sh7 bilioni kutibu magonjwa na madhara mengine yaliyosababishwa na uchimbaji wa madini hayo.
chanzo: Mwananchi
Post a Comment