TIMU ya Tanzania Bara leo imepata aibu kubwa baada ya kuchapwa mabao 3-0 na wenyeji Uganda katika mechi ya nusu fainali ya michuano ya soka ya Kombe la Chalenji iliyochezwa kwenye Uwanja wa Namboole mjini Kampala.
Kwa ushindi huo, Uganda sasa itamenyana na Kenya katika mechi ya fainali itakayopigwa Jumamosi kwenye uwanja huo. Kenya ilifuzu kucheza hatua hiyo baada ya kuitoa Zanzibar kwa penalti 4-2 baada ya timu hizo kumaliza dakika 120 zikiwa sare ya mabao 2-2.
Iliwachukua Uganda dakika 11 kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Emmanuel Okwi baada ya kuuwahi mpira uliopigwa na Hamza Muwonge. Jitihada za kipa Juma Kaseja kuzuia shuti hilo hazikuweza kuzaa matunda. Timu hizo zilikwenda mapumziko Uganda ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Uganda ilikianza kipindi cha pili kwa kasi na kufanikiwa kuongeza bao la pili dakika ya 51 lililofungwa na Robert Ssentongo baada ya mabeki wa Tanzania Bara kudhani ameotea.
Ssentongo alizitikisa tena nyavu za Tanzania Bara dakika ya 71 baada ya kipa Juma Kaseja kutema shuti kali la Moses Oloya.
Pambano hilo lililazimika kusimama kwa takriban dakika saba baada ya taa za uwanja wa Namboole kuzimika dakika ya 85.
Tanzania Bara sasa inatarajiwa kuvaana na Zanzibar keshokutwa katika mechi ya kutafuta mshindi wa tatu, inayotarajiwa kuwa ns ushindani mkali na wa aina yake.
Wakati huo huo, Zanzibar leo imetolewa kiume katika michuano ya Kombe la Chalenji baada ya kuchapwa kwa penalti 4-2 katika mechi ya kwanza ya nusu fainali iliyochezwa kwenye uwanja wa Namboole.
Mshindi wa pambano hilo ilibidi apatikane kwa njia ya matuta baada ya timu hizo kumaliza dakika 120 zikiwa sare ya mabao 2-2.
Khamis Mcha ‘Vialli’ na Issa Othma Ally ndio walioikosesha Zanzibar ushindi baada ya kupoteza penalti mbili za kwanza kabla ya Aggrey Morris na Samir Haji Nuhu kufunga penalti mbili za mwisho.
Kenya ilipata penalti zote nne kupitia kwa Mike Barasa, Joackins Atudo, Edwin Lavatsa na Abdallah Juma aliyepiga ya mwisho.
Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkali, Zanzibar ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 20 lililofungwa na Mcha, kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Jaku Juma.
Kenya ilisawazisha dakika ya 29 baada ya beki Nadir Haroub Cannavaro kujifunga kwa kichwa alipokuwa akiokoa mpira wa krosi huku akiwa amezongwa na Baraza na kipa Mwadin Ally akiwa ametoka langoni kuokoa hatari hiyo. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.
Zanzibar iliongeza bao la pili dakika ya 75 lililofungwa kwa njia ya penalti na Morris baada ya beki Joackins Atudo wa Kenya kumwangusha Jaku ndani ya eneo la hatari.
Zikiwa zimesalia dakika 10 pambano hilo kumalizika, Kenya ilisawazisha kwa bao lililofungwa na Baraza baada ya mabeki na kipa wa Zanzibar kushindwa kuokoa mpira wa krosi uliopigwa na Paul Were.
Post a Comment