Na
Emmanuel Shilatu
Novemba 19 mtandao wa
kijamii ulimualika Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Mhe. Zito Zubery Kabwe kwenye
mjadala wa moja kwa moja kupitia safu ya Jukwaa la Kisiasa ambapo Watu walikuwa
wakiuliza maswali na Zito alikuwa akiyajibu.
Binafsi sikukeleka na
mtindo huo bali kilichonikera ni namna ambavyo Mhe. Zito alivyokuwa akijibu
maswali ya wana globu ya jamii. Nitakupa mifano rahisi tu miwili ya maswali
ambayo aliulizwa na alivyoyajibu kiuwepesi wepesi.
Zito
aliulizwa: “Unaiongeleaje
sera ya Majimbo ya CHADEMA”?
Swali
lingine aliloulizwa lilikuwa ni: “Unaona tofauti ya msingi kati ya CCM
na CHADEMA ni ipi?”
Zito akajibu: “CCM imeshindwa
kupambana na adui ufisadi, CHADEMA tunapambana natutapambana na ufisadi kwa
nguvu zetu zote. CCM inaamini katika sokoholela, CHADEMA tunaamini katika soko
linalojali. CHADEMA inaamini katikanguvu ya Umma, CCM inaamini katika nguvu ya
Dola”.
Majibu ya maswali hayo yalinifanya
nihoji uweledi na uzalendo wa Mheshimiwa Zito ambao kadri siku zinavyozidi
unaonyesha kuyeyuka kama barafu juani. Ngoja tuyachambue majibu ya Zito.
Tuanze na sera ya utawala wa Majimbo.
Suala hili lilianzishwa kuzungumzwa na Wanasiasa ambapo 5 Mei 2012, Mbunge wa
Arumeru Mashariki, Mhe. Joshua Nassari alitamka wazi wazi kuwa umefika wakati
kwa ukanda wa Kaskazini kujitenga na kuunda Taifa lao huru, linalohusisha Mikoa
ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara.
Ubaguzi huo haukuishia hapo, hali
iliendelea hadi kwa Wananchi nao pia
kuidandia hoja hii na kuianza kuizungumzia mpaka imefikia hatua Watu wakasema
nchi ya Zanzibar nayo pia iwe jimbo. Lahaula!!
Watu hawa wanashindwa kuielewa sera
ya majimbo kuwa ulikuwa ni mfumo wa kiutawala ulioasisiwa na Wakoloni ambapo
kabla ya kupata uhuru wetu hapo tarehe 9 Desemba 1961, iliyokuwa Tanganyika
ambayo sasa ni Tanzania Bara, ilikuwa ni koloni la utawala wa Ujerumani na
baadaye chini ya utawala wa Uingereza, ilitawaliwa chini ya mfumo wa majimbo.
Baada ya uhuru na hatimaye Jamhuri,
Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika chini ya uongozi wa TANU, Hayati Mwalimu
Julius Nyerere alifuta utawala wa majimbo
na kuanzisha sera ya Madaraka mikoani ya
kuanzisha mfumo wa Serikali za mitaa katika kila Mkoa na Wilaya.
Mwalimu Nyerere aliamua
kuitoa Tanganyika kwenye makucha ya kikoloni na mambo yake yote (ikiwamo sera
ya majimbo) ili kudumisha haki, usawa, amani, umoja wa Kitaifa na maendeleo ya Taifa letu ili matumizi ya Dola
na rasilimali za nchi ziwanufaishe na kuwaendeleza Wananchi wote. Hiyo ndio
misingi ya Mwalimu Nyerere aliyoijengea Taifa hili.
Wanong’ang’ania sera ya
majimbo wanataka kutuaminisha kwamba wako radhi kuivunja misingi iliyowekwa na
Mwalimu Nyerere? Watu hao wanataka kuirudisha Taifa letu kwenye mifumo ya
kikoloni? Wameamua kuwagawa Watanzania? Wanataka kuondoa sera ya madaraka
mikoani, ili wananchi watumikiwe na nani? Kwa kufanya hivyo maendeleo
yatachochewa na kuletwa na nani?
Utawezaje kuimarisha Halmashauri za
Wilaya/Miji/Manispaa/Majiji endapo utataka kuondoa sera nzima ya madaraka
mikoani ambayo ndiyo msingi mkuu wa uimara wa Halamshauri na Manispaa zetu?
Kitendo cha kung’ang’ania sera ya majimbo ni kuchochea moto
wa ubaguzi kupitia ukanda kwani Taifa letu linaendelea kuwa na hali ya amani na
utulivu kutokana na kutokuwa na mipaka ya kuishi na kila mmoja ananufaika na
rasilimali za mwenzake hata kama hajabarikiwa kuwa nazo.
Watanzania wataweza kuboresha hali zao za kimaisha kwa
kuondokana na umaskini kupitia mfumo wa Tawala za mikoa na serikali za mitaa
zenye mamlaka kamili, uwezo, ufanisi na
uwajibikaji na siyo kupitia sera ya utawala wa majimbo.
Hivyo sera ya Majimbo inayochochewa na wanasiasa mithili ya
Zitto Kabwe ina malengo ya kubomoa na kudhoofisha sera nzima ya madaraka
mikoani na hivyo itaathili utendaji kazi wa Halmashauri na Manispaa zetu.
Halikadhalika sera ya
majimbo itawagawa na kuwabagua Wananchi kwa misingi ya majimbo na inakiuka
Katiba ya nchi yetu na haki za raia wa Jamhuri ya Muungano. Hivyo yatupasa
tuipinge vikali kwani haina nia nzuri kwa mustakabali wa Taifa letu.
Tuje
kwenye suala la utofauti kati ya CCM na CHADEMA ambapo Mhe. Zitto alijibu “CCM imeshindwa kupambana na adui
ufisadi, CHADEMA tunapambana natutapambana na ufisadi kwa nguvu zetu zote. CCM
inaamini katika soko holela, CHADEMA tunaamini katika soko linalojali. CHADEMA inaamini
katikanguvu ya Umma, CCM inaamini katika nguvu ya Dola”.
Kitendo cha Zitto kutoa
majibu haya yanaonyesha dhahiri amemezwa na mambo makuu mawili, aidha amekosa
uweledi wa kujua Taifa hili lilipotoka, lilipo na linapokwenda ama anaongozwa
na ushabiki zaidi kuliko uzalendo kwa Taifa lake.
Zito anaposema utofauti
kati ya CCM na CHADEMA unatokana na mapambano dhidi ya ufisadi ambapo wao
CHADEMA wameliweza hili na CCM wamelishindwa ananipa wasiwasi mkubwa juu ya
uweledi wake.
Zito anashindwa kuelewa ya kuwa mojawapo kati ya
sera na itikadi ya CCM ni chama kinachozingatia na chenye mapigano ya chati
dhidi ya ubadhilifu wa mali za umma, rushwa, uhujumu na aina yeyote ile ya
ufisadi. Na katika kulithibitisha hili hata katika ilani ya CCM ya 2005-2015
imebainishwa dhahili na ushahidi wa utekelezaji wake upo wazi.
Kwenye katiba ya CCM kifungu cha 1 ibara ya 8(2)
inatoa masharti kwa kila mwanachama kuwa mtu anayefanya juhudi za kuielewa
kuieleza na kuitekeleza itikadi na siasa ya CCM. Hivyo mojawapo ya kazi ya
mwana CCM ama kada wa CCM ni lazima awe mstari wa mbele katika mapigano dhidi
ya ufisadi na mafisadi nchini. Hii haijalishi awe anatoka katika kamati kuu
(C.C) ama katika tawi.
Serikali imekuwa ikisikiliza kupokea na kutimiza
wajibu wa utekelezaji wa mambo yote yahusuyo rushwa na ufisadi nchini kupitia
kwa “makomandoo” mbalimbali wa upiganaji wa maovu nchini.
Tusimsahau Mzindakaya ‘Mzee wa
Mabomu’ alivyomlipua Idd Simba kwenye sakata la sukari. Pia tumkumbuke
Sokoine na machukizo dhidi ya wahujumu uchumi. Pia tusimsahau Dr. slaa
alipojitoa muhanga kuwataja mafisadi (10 list of shames) wa EPA pale Mwembe
Yanga. Tuendelee kukumbuka harakati za mapigano ya Dialo dhidi ya
uwekezaji ndani ya maliasili.
Yapo mambo mengi mno yaliyoibuliwa na baadhi ya
wanaharakati lakini nayo Serikali haipo nyuma kwenye uchukuaji wa utekelezaji
wa dhahiri wa mapigano dhidi ya ufisadi bila ya kuangalia hadhi, umaarufu wala
wadhifa wake. Pia tumeshuhudia viongozi waandamizi na makada wakubwa wa chama
wakijiuzulu na wengine kulala rumande na hata kupelekwa mahakamani.
Ila sisi wananchi tu wepesi sana wa kusahau. Tusisahau kukumbuka jinsi
gani watuhumiwa wa EPA wanavyoendeshwa mahakamani pia tu mashuhuda wa jinsi
gani vigogo wa BOT wanavyosota rumande kwa ajili ya kashfa za majengo pacha,
uzidishaji wa utengenezaji wa noti EPA.
Jamii pia imeshuhudia watuhumiwa wa nyara za
Serikali za kontena lililokuwa na meno ya tembo waliburuzwa mahakamani hivi
karibuni.
Pia tusisahau jinsi gani Chifu Abdallah Fundi Kira
alivyochapwa voboko kutokana na kupokea rushwa ya sh. 25/-. Pia wahujumu uchumi
hawatakaa wamsahau Edward Sokoine kwa jinsi alivyopambana nao. Tusisahau sakata
la minofu ya samaki na kitita cha sh. Million 900 kule Mwanza akina Mzindakaya
na Lamwai walimpelekea kilio Profesa Mbilinyi hatakaa alisahau hili. Pia
tukumbuke dhoruba iliyompata Aron Chiduo enzi ya utawala wa Mwinyi.
Kwa haya, napenda kuzipongeza Serikali zote kwa
kuonyesha uhai kwenye mapigano dhidi ya rushwa na ufidadi nchini.
Naam, mtu akifanya vizuri lazima apewe haki
(pongezi) zake tena kwa roho moja. Wale wanaobeza harakati hizi sijui tuwaweke
kundi gani ambalo jamii itawaelewa.
Ni jambo la kushangaza kuona ni jinsi gani watu ama
kundi la watu linavyojipa sifa ambazo sio zao. Mathalani vyama vya upinzani
wanajitutumua kwa kauli zao kwamba wao ndio waanzilishi wa mapambano ya rushwa
na ufisadi nchini ama wao ndio waasisi wa mapambano ya vita dhidi ya vita vya
ufisadi ama rushwa wakati mapambano haya yalikuwapo tangu enzi za Mwalimu
Nyerere hata kabla wao hawajazaliwa ama kuianza siasa.
Historia inajidhihirisha hivyo kwamba harakati hizi
zilikuwapo tangu enzi za TANU na ASP (Rejea fundisho alilopata Chifu Fundikira
na Aron Chiduo; pia tusisahau harakati za hayati Sokoine) kinanachobadilika
hapa ni kiitikio cha msamiati kutoka uhujumu uchumi na sasa ni ufisadi.
Kutokana na
mdudu huyu (ufisadi wa rushwa) kuzidi kukua na kukomaa zaidi huku akitumia
mbinu kali na za ajabu amezidi kuwajeruhi umma na hatimaye kuwaacha katika
dimbwi kubwa la umasikini wenye kutia aibu. Hivyo kimtazamo utaona ni jinsi
gani Taifa linahitaji mahodari wa upambanaji dhidi ya mdudu huyu rushwa na
ufisadi na kamwe hawataweza kufungwa mdomo.
Rushwa na ufisadi ni majanga ya kitaifa
yanayohitaji mapambano ya kweli na wala si zima moto ambao kamwe tusihusishe na
itikadi na utashi wa kisiasa, wadhifa husika, utegeano, chuki wala malipizo ya
aina yeyote ile wala ushabiki upofu ama siasa maji taka.
Kwa mantiki hii, ni
dhahiri tofauti alizozitoa Zitto ni batili kwani zimeegemea kwenye ushabiki wa
kisiasa zaidi.
Zito alitakiwa kuwa
wazi na kueleza tofauti kati ya CCM na CHADEMA ni kuwa Chadema inaamini katika
maandamano na uanaharakati huku CCM ikiamini katika utekelezaji wa ilani ya
uchaguzi na kuwahimiza Wananchi kufanya kazi; CCM inaamini katika sera ya ujamaa na kujitegemea
huku Chadema ikiamini katika ubepari; CCM
ina katiaka utawala wa kisheria na si hisia huku Chadema ikiamini katika
hisia na utawala wa ksheria si kitu kwao na ndio maana inataka watu waburuzwe
mahakamani hata pasipo ushahidi.
Post a Comment