Gaudence Mwaikimba; Mfungaji bora Kombe la Hisani DRC |
Na Mahmoud
Zubeiry wa Bin Zubeiry, Kinshasa
MSHAMBULIAJI
Gaudence Mwaikimba wa Azam amekuwa mfungaji wa mashindano ya Kombe la Hisani
yaliyoandaliwa na FECOFA, Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC) baada ya kumaliza na mabao matatu, akifuatiwa na Kipre Herman Tchetche na
Ngulubi Kilua wa Shark FC waliofunga mawili kila
mmoja.
Jumla pamoja
na penalti za baada ya dakika 90 za mechi, Mwaikimba amefunga mabao matano,
Kilua matatu na Kipre matatu.
Hata hivyo,
kwa kuwa mashindano haya ni ya hisani, hakutakuwa na zawadi mwa bingwa wala
wachezaji bora, hivyo Mwaikimba anaondoka DRC na hadhi tu ya ufungaji bora.
Azam jana
iliwafunga wenyeji Dragons FC kwa penalti 4-2, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya
dakika 90 kwenye Uwanja wa Martyrs mjini hapa na kutwaa Kombe. Azam walikuwa wa
kwanza kupata bao katika dakika ya 12 kabla ya Dragons kusawazisha dakika ya
75.
Katika
mikwaju ya penalti, kipa Mwadini Ally alicheza mikwaju miwili ya Dragons, wakati
Gaudence Mwaikimba, Himid Mao, Joackins Atudo na Samih Hajji Nuhu walifunga
penalti za Azam.
Hata hivyo,
Azam jana hawakukabidhiwa Kombe uwanjani hapo baada ya waandaji kusema
wanakwenda kulipamba kwanza, hivyo sherehe za makabidhiano ya Kombe zinaweza
kufanyika leo.
Azam
iliingia fainali, baada ya juzi kufanikiwa kuitoa kwa mikwaju ya penalti 5-4
Shark FC ya hapa, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa
Martyrs. Azam inatarajiwa kuondoka hapa kesho mchana kurejea Dar es
Salaam.
Post a Comment