Na Walter Sawe
NIKIRI kwamba mimi si mtaalamu wa nyota na kwa maana hiyo kile nitakachokijadili hapa siyo suala la unajimu. Naangalia tu mambo halisi yaliyopo, yanayoendelea na yanayotokea nchini kwa sasa mwaka huu ukiwa ukingoni.
Nakumbuka mwanzoni Karatu ilipokuwa ikitawaliwa na CCM (Mbunge CCM, na viongozi wote kipindi hicho kama unakumbukumbu hadi mashina walikuwa CCM). Nadhani kwa kipindi hicho wananchi waliishi kwenye hali mbaya sana kimaendeleo na kimaisha (Umaskini) baada ya kuingia kwa mfumo huu wa vyama vingi mwaka 1992, ( kama walivyofanya Kawe 2010) wakaona hapana, kwa nini tusibadilike?
Wakamweleza Mbunge wao wa wakati huo, “Ee bwanae kwa vile umeshindwa kutuletea maendeleo na kutatua kero zetu tutakunyima kura.”
Mwaka uliofuata, 2000 kweli wananchi wakaamua kumchagua Dr. Willbroad Slaa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwa Mbunge wao. Sina sababu ya kuelezea ni nini kilichopo jimboni Karatu kwa sasa.
Ninachopenda kusema ni kwamba nilipomsikiliza hivi karibuni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka wakati akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Chasimba Tegeta Wazo Hill.
Akisema Serikali imewataka wananchi 903 wenye mgogoro wa ardhi eneo la viwanja namba moja, nne na saba kuhama. “Serikali itawajibika tuwatafutie eneo kama ilivyoamriwa na mahakama’’ Mwisho wa kunukuu.
Nilipatwa na wakati mgumu jinsi ya kuandaa makala haya kutokana na kauli za mara kwa mara, Mbunge wa Jimbo hilo la Kawe Halima Mdee alizozitoa wakati wa mkutano na wananchi kwenye uwanja wa Panga, pamoja na mambo mengine aliwahi kusema hivi “Nitahakikisha Kituo cha Polisi kinaondoka ndani ya Kiwanda cha Wazo, lakini Chatembo, Chasimba hakuna mtu kuhama ukitaka kujenga ghorofa jengeni”
Binafsi nilijiuliza hapa kati ya Mdee na Tibaijuka nani anafanya siasa na nani anatatua kero?
Leo imebidi nianze na mfano huo wa Karatu baada ya mwaka 2010 ndani ya nchi ulipofanyika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani. Pamoja na mambo mengine bahati nzuri Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilishinda kwa kishindo kiti cha ubunge Jimbo la Kawe.
CHADEMA kushinda Kawe hakukuwa kwa matarajio ya wengi bali kulitokana na CCM kufanya makosa (Kura za maoni/wengi wape), kuwanyima baadhi ya waliokuwa wagombea kipindi hicho nafasi hiyo likawa kosa.
Hadi naandika makala hii tangu ufanyike uchaguzi huo mkuu mwaka 2010, huu ni mwaka wa tatu unaelekea wa nne sasa kata nyingi katika jimbo hilo hakuna kilichofanyika.
Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa, wakati akifungua mkutano mkuu wa chama hicho Jimbo la Kawe na Kinondoni. Alikaririwa na moja ya magazeti yanayochapishwa nchini akisema hivi “Nadhani Kinondoni kuna tatizo, hali hii inajionyesha wazi udhaifu wa jimbo,……. Unapojitokeza hautazembewa na uongozi wa juu kwani ukiachiwa utasababisha majimbo mengine kusambaratika”
Naomba niseme kwamba nimewahi kuelezea kwa kina na kwa kirefu kwenye baadhi ya makala zangu namna Mdee alivyokiuka sheria ya manunuzi ya umma (PPRA) 2004 na kutoa tenda (Zabuni) kwa mkandarasi aliyekimbia na fedha za umma hadi leo haijulikani zipo wapi na hatua gani alichukuliwa na kusababisha mradi wa shule ya msingi Ununio kusimama.
Sina tena sababu ya kuyarudia yote niliyowahi kuyasema ndani ya makala husika. Ninachopenda kusema ni kwamba kwa nyakati tofauti tofauti katika maandishi yangu, (makala) nyingi nimeandika nikielezea wasiwasi wangu wa utendaji kazi na staili ya uongozi alionao Mbunge wa Jimbo la Kawe Halima Mdee.
Nikisema kwamba matumaini makubwa ya wananchi juu yake sasa yamegeuka kujilisha upepo tu. Pia ile miujiza iliyokuwa ikitarajiwa itendwe na kiongozi aliyejipatia sifa ya kuwa tumaini la (Rejea wakati wa ziara ya Tibaijuka). Wanyonge leo inaonekana kuhitaji maombi zaidi kuliko ilivyotarajiwa!.
Kilichonisukuma kuyasema haya 2012 ukiwa ukingoni ni baada ya ziara ya Waziri Tibaijuka pale Chasimba na namna sasa ninavyowasikia baadhi ya wapiga kura wakianza kulalamikia aina mpya hii ya utendaji wa viongozi wa, kuanzia mbunge, madiwani kuwa hauendani na matarajio ya walio wengi.
Naomba nikiri kwamba inawezekana wakati ule wa uchaguzi 2010 wengi walikwenda kiushabiki wakiwa hawajui walichokifanya au wanachotarajia.
Nikiri kwamba nakumbuka nikiwa kwenye moja ya ziara ya Mdee wakati akiwashukuru wananchi alisema hivi: “Nawashukuruni sana wapiga kura wangu wote kwa kunichagua; lakini nataka kuwaambia kitu kimoja kazi niliyonayo ni kubwa kwani sina madiwani wa kutosha nina madiwani wawili tu”. Mwisho wa kunukuu.
Alianzia Bunju hadi Tegeta alipomalizia mkutano wake maneno yalikuwa ni hayo hayo. Nikajiuliza kwani hizo shukurani, maneno au habari za madiwani yana mchango gani katika utendaji? Au tulimchagua mtu kuwa kiongozi wakati hawezi kuongoza eti kigezo ni madiwani?.
Si nia yangu kumsakama Halima Mdee kama baadhi ya wavivu wa kufikiri waliomzunguka wanavyodhani, hapana maana mambo mbona yapo wazi?
Naandika makala haya kwa nia ya kumtahadharisha sasa na huko tuendako juu ya utafunaji, kufisadi huku kwa fedha za umma kwa watu walio karibu naye na staili yake ya kiongozi kwa faida yake.
Nachopenda kusema ilinishangaza hata wakati ule wa kampeni kuwaona baadhi ya watu tena wasomi wakitoa vigezo vya ajabu vya uchaguzi ule, eti ulitakiwa kuwa uzuri wa sura, kuwa na gari, nyumba nzuri, kitambi, udogo kiumri, undugu au ukabila!
Hii ilikuwa ni hatari sana wakati ule, maana leo haya yote hayana mchango wowote katika utendaji. Hivi kulikuwa na haja gani ya (Rejea kauli yake dhidi ya Chasimba eti wahame!) kumchagua mtu kuwa mbunge au diwani wakati kumbe hawezi hata kujenga hoja ya kutetea wananchi wake? Au asiyejua hata idadi ya wakazi katika Jimbo ama Kata eti kwa kigezo cha uzee au ujana? Kwa kigezo cha rangi, kabila au sura?
Ni kwa mwelekeo huo, watu leo wanabashiri mwisho wa Halima si mwema, kwamba historia ya jimbo huenda ikageuka na jimbo likarudi mikononi mwa CCM!
Kitendo cha Katibu Mkuu wake Dr. Slaa kukaririwa na vyombo vya habari wakati wa ziara yake Kinondoni akisema “Sasa hivi si wakati wa kusema CCM haijafanya nini kwa miaka 50 tunatakiwa tuisome katiba yetu na tuonyeshena tuwaeleze wananchi inasema nini na tunaisimamia vipi katika utekelezaji wake”. Mwisho wa kunukuu.
Sasa utabiri wangu unanisukuma nianze kuamini katika sinema hii ya maendeleo ya wananchi yasiyoendelea jimboni Kawe hakuna mwisho hadi imwangushe muhusika mkuu. Masuala ya migogoro ya ardhi, maji safi, barabara yalivyomkalia Mdee kooni.
Kabla sijafika mwisho wa makala haya; nimpongeze Waziri wa Nyumba Ardhi na Maendeleo ya Makazi Prof. Anna Tibaijuka kwa kuweka wazi mgogoro wa muda mrefu kati ya wananchi wa Chasimba na Uongozi wa Kiwanda cha Saruji Wazo Hill uliodumu kwa takribani miaka 10 iliyopita.
Katika mkutano huo Prof. Tibaiajuka alisema “Wizara ina mapungufu mengi uzembe sio wa wananchi bali umesababishwa na watendaji ambao sio waaminifu kazi yao kula fedha tu huku wananchi wakiambiwa nenda rudi nenda rudi na kusababisha mgogoro kati ya serikali, wananchi na kiwanda”.
Nilistuka kusikia kauli hiyo ya waziri, kwani kwa nyakati tofauti mbunge wa Kawe aliwahi kufanya ziara kama hiyo akiongozana na msafara mkubwa wa maofisa ardhi toka manispaa na usalama wa Taifa, lakini hawakufua dafu kumaliza mgogoro huo licha ya kutumia mamilioni ya walipa kodi!
Hongera Mama Tibaijuka kwa hili! Katika muelekeo kama huu inakuwa vigumu kutambua namna Mdee atakavyojinasua na `mawaa’ pamoja na staili yake hii ya uongozi! Inakuwa ni vigumu kuendelea kuamini kwamba zile kelele, tambo kama zinaweza kumwokoa na haya niyoelezea kwenye makala haya nadhani itakuwa hukumu yao 2015 watakaporudi kwa wapiga kura wao.
Nihitimishe kwa nukuu ya Mwalimu Nyerere enzi za uhai alipata kusema hivi “Uhuru na maendeleo ni vitu vinavyohusiana sana; uhusiano wao ni sawa na uhusiano baina ya kuku na yai. Bila ya kuku hupati mayai na bila mayai kuku watakwisha. Vile vile bila uhuru hupati maendeleo na bila maendeleo ni dhahiri kwamba uhuru wako utapotea”.
on Friday, December 28, 2012
Post a Comment