Kampala
Kocha wa Timu ya
Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen amekiri kuwa kikosi chake
kilizidiwa na Cranes ya Uganda katika nusu fainali ya mashindano ya Cecafa
Challenge huku akisema licha ya maandalizi mazuri, Waganda walikuja na mbinu ya
kuwakabili.
Poulsen aliyasema hayo
jana baada ya mchezo huo ambapo Stars, inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro
Premium Lager ililala kwa kukubali kichapo cha mabao 3-0.
“Ukizingatia kuwa
walikuwa katika uwanja wa nyumbani, waliwapa wachezaji wetu taabu sana na
tulifanya makosa kuruhusu goli la haraka katika dakika ya kumi na moja hivi,”
alisema.
Alisema kuelekea mwisho
wa kipindi cha kwanza Stars ilijitahidi kuhakikisha hakuna bao lingine linaingia
na walikuwa na matumaini kuwa mchezo ungebadilika katika kipindi cha
pili.
“Hata hivyo tulifanya
makosa tena kuwaruhusu waganda kupiga krosi na kuziunganisha na kupata goli tena
na hapo wachezaji wa Uganda wakapata nguvu zaidi hasa ikizingatiwa mashabiki wao
walikuwa wamejaa uwanjani wakishangilia,” alisema Poulsen.
Kocha huyo kutoka
Denmark, alisema walikubali hali halisi kwani walicheza na timu yenye kiwango
cha juu.
“Ila nataka kusisitiza
tu kuwa hatujakata tamaa kwani vijana wamepata uzoefu mkubwa katika mashindano
haya na itatusaidia kusonga mbele kwani tumejitahidi kufikia hatua za mwisho za
mashindano ambayo yalikuwa magumu kwani timu zote zilikuwa zimejiandaa vizuri,”
alisema.
Alisema kwa sasa
wanajiandaa na mechi dhidi ya Zanzibar Jumamosi ili kupata mshindi wa tatu wa
mashindano hayo. “Huu nao utakuwa mchezo mgumu kwani tumeshaona namna Zanzibar
wanacheza,” alisema.
“Tulianza mashindano
vizuri na ombi langu tu sasa kwa wachezaji ni tumalize vizuri kama tulivyoanza
angalau tuweze kupata nafasi ya tatu katika mashindano haya,”
alisema.
Katika fainali, Kenya itamenyana na mwenyeji Uganda katika uwanja wa Mandela uliopo Nambole, Jijini Kampala.
Akizungumza kutoka Dar
es Salaam, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager aliipongeza Stars kwa
hatua iliyofikia katika mashindano ya Cecafa Challenge huku akisema sio mwisho
wa safari kwani bado kuna mashindano mengine.
“Tunaamini vijana
wamepata uzoefu mkubwa na sasa wana silaha ya kukabiliana na mashindano mengine
mbele yao…hatua waliofikia ni kubwa tu na tunawaomba wasife moyo,” alisema huku
akiwataka watanzania pia kuwa na subira kwani timu bado inaonesha
matumaini.
Stars inatarajiwa
kurejea nyumbani Jumapili hii baada y mashindano kumalizika ili kujiandaa na
mechi ya kirafiki dhidi ya Chipolopolo ya Zambia ambapo Kilimanjaro Premium
Lager inatarajiwa kuizindua Taifa Stars rasmi kwa watanzania.
Post a Comment