Wajumbe wa Kamati Kuu ya Taifa
ya Sensa ya watu na makazi wakiwa katika kikao cha Kumi cha Kamati hiyo
kilichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dar es
salaam.
Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu
ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi akikiongoza Kikao cha Kumi cha Kamati hiyo Jijini Dar es
salaam.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohd akiwa makini katika
majadiliano ndani ya kikao cha Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi
kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Waziri Mkuu Mjini Dar
es salaamu.
Waziri wa Fedha wa SMT Dr William
Mgimwa na mwenzake anayesimamia Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo wa SMZ Mh.
Omar Yussuf Mzee ambao ni wajumbe wa kikao cha Kamati Kuu ya Taifa
ya Sensa ya watu na makazi wakiendelea na majadiliano Mjini Dar es
salaamu
Baadhi ya wajumbe wa Kikao cha
Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya watu na makazi wakijumuika katika mijadala
tofauti ya kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya Waziri Mkuu
Mjini Dar es salaam.Na Othman Khamis Ame
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete Jumatatu ya Tarehe 31
Disemba 2012 anatarajiwa kuzindua matokeo ya Sensa ya
Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Uzinduzi huo
utakaoshirikisha wananachi wa Mkoa wa Dar es salaam na Vitongoji vyake wakiwemo
pia waalikwa kutoka sehemu mbali mbali za mikoa ya Tanzania utafanyika katika
Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam.
Wajumbe wa Kamati Kuu
ya Taifa ya Sensa ya watu na Makazi ya Mwaka 2012 walikutana pamoja na mambo
mengine katika kikao chao cha 10 walipitia ratiba ya shughuli hiyo kwa
matayarisho ya mwisho chini ya Mwenyekiti mwenza wa Kamati hiyo Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu
Mjini Dar es salaam.
Akiwasilisha Taarifa za
kazi mara baada ya kumalizika kwa zoezi la Sensa kwa wajumbe wa Kamati hiyo
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania Dr. Albina Chua alisema
kazi ya miongozo ya Takwimu hivi sasa inaendelea vyema.
Dr. Albina Chua
alifahamisha kwamba miongozo hiyo inakwenda sambamba na kuhakiki taarifa na
kuanza kwa zoezi la uingizaji Taarifa katika compyuta kazi inayofanywa na
wataalamu wa Takwimu baada ya kupata mafunzo maalum ya wiki
sita.
“ Jumla ya watu mia nne
walilazimika kuwajiriwa kufanya kazi hiyo muhimu inayohitaji
utaalamu na umakini wa hali ya juu katika kuikamilisha hasa kwenye
uchambuzi wa takwimu za Sensa “. Alifafanua Dr. Albina
Chua.
Naye Waziri wa Fedha wa
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. William Mgimwa alisema Wizara
ya Fedha itaendelea na uchambuzi wa Takwimu zitakazotokana na sensa hiyo kwa
lengo zaidi la kiuchumi.
Dr. Mgimwa alisema
katika kukamilisha zoezi zima la sensa ya watu na makazi Serikali imeshatoa
shilingi Bilioni sita kati ya Bilioni 12 zilizotengwa ambapo kazi ya
usafirishaji vifaa vya sensa imeshafanywa na hivi sasa uingizwaji
wa taarifa katika Kompyuta unaofanywa na Wahariri maalum
inaendelea.
“
Tumefanikiwa vyema katika kazi hii muhimu licha ya changamoto ndogo ndogo
zilizojichomoza katika zoezi hili ikiwemo madai ya Wenyeviti wa Vijiji
waliosaidia kusimamia zoezi hili katika maeneo yao”. Alifafanua Waziri
Mgimwa.
Kwa upande wake Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Dr.
Mwinyihaji Makame Mwadini kwa niaba ya Waziri anayesimamia Fedha, Uchumi na
Mipango ya Maendeleo Zanzibar alisema zoezi la sensa kwa kiasi kikubwa
limefanikiwa vyema licha ya changamoto za baadhi ya vikundi vya kidini kupinga
Zoezi hilo.
Dr. Mwinyihaji alieleza
kwamba sensa ya watu ambayo inakusanya takwimu tofauti itasaidia chachu ya
maendeleo hasa katika mpango wa maendeleo katika kipindi cha miaka kumi
ijayo.
Akitoa nasaha zake
Mwenyekiti mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya watu na makazi, Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewapongeza watendaji wa sekta
tofauti Nchini waliojitolea kufanikisha zoezi zima la sensa ya watu na makazi ya
mwaka 2012.
Balozi Seif alisema
zoezi hilo lilikumbwa na changamoto zilizopelekea kuongezwa kwa siku za
uandikishaji kutokana na sababu za baadhi ya makundi ya dini kushawishi wananchi
kutojiandikisha kwenye zoezi hilo.
Kikao cha kumi na moja
cha Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi kinatarajiwa kufanyika
Zanzibar mnamo Wiki ya Pili ya Mwezi wa Machi mwaka 2013.
Post a Comment