3.0 MAPENDEKEZO MAHSUSI
3.1 Vigezo na misingi ya kikatiba na kisheria
Kuna umuhimu wa kuwa
na Vigezo na misingi ya kikatiba-kisheria ya kuhakikisha kuwa watu, ambao ndio
wanaoiunda Katiba Mpya na kwa niaba yao Bunge la Katiba linatarajiwa kupitisha
hiyo Katiba, watakuwa na mamlaka kwa Serikali:
3.1.1 Nafasi ya watu katika kusukuma Serikali
Nguvu ya
watu katika kusukuma Serikali kutimiza
wajibu wake wa kusimamia kwa dhati na kistadi mambo ya kiutendaji ya huduma na
shughuli zote za umma ipate fursa za kufanya kazi kihalisia na kuifanya nchi
kuendeshwa vizuri kwa manufaa na maslahi ya wananchi, wakiwemo wanyonge kihali
na mali.
3.1.2 Nguvu ya watu kupewa nguvu kupitia vyombo vya kikatiba na kisheria
Jambo hili liwe wazi na
halisi, sio tu kwa njia ya vigezo na misingi, bali pia kimuundo kupitia vyombo
vya kikatiba-kisheria ambavyo vinashirikisha na/au kuwakilisha wananchi katika
maamuzi juu ya mambo muhimu kuhusu maisha na maslahi ya
kijamii/kitaifa.
3.2 Uwajibikaji na uzingatiaji wa maadili mema kikatiba na kisheria
Katiba ielekeze
uwajibikaji na uzingatiaji wa maadili mema, pamoja na udhibiti wa madaraka.
Tunasisitiza: Mambo haya ni ya msingi, yasiende kisiasa bali yapewe nguvu
kikatiba/kisheria. Ili kufanikiwa katika hili, haitoshi tu kuwa na Katiba bali
iwe niKatiba inayotekelezeka kikamilifu.
3.3 Maadili Mema
3.3.1 Mmomonyoko wa maadili kamajanga la kijamii na kitaifa
Kiwango cha maadili na
uwajibikaji kiadilifu na kizalendo nchini kimeshuka mno kiasi kwamba mmomonyoko
wa maadili ni janga la kijamii kitaifa. Hatua maalumu za dhati zinahitajika
kulinusuru Taifa letu kutokana na janga hilo:
3.3.1.1 Elimu
ya maadili iendeshwe mashuleni na vyuoni.
3.3.1.2 Serikali itakiwe na Katiba na sheria husika kuchukua
wajibu huu na kuutekeleza katika mfumo rasmi wa elimu kupitia Tume Huru ya
Elimu ambayo ndiyo iwajibike moja kwa moja katika kusimamia kazi
hii.
3.3.2 Tume Huru ya Elimu:
CPT inapendekeza kwamba,
kwa njia ya Tume Huru ya Elimu:
3.3.2.1 Katiba
au sheria mpya ielekeze Elimu kutolewa kwa umma ikilenga kuwezesha wananchi
kusaidia Mahakama na Bunge kutimiza wajibu wake wa kudhibiti, kuelekeza na
kuwajibisha Serikali katika utekelezaji wa wajibu wake kwa umma na
kuhakikisha utawala bora ambao unawajibika, unawajibisha na unawajibishwa; ni
shirikishi na wakilishi.
3.3.2.2 Aidha, uwepo wajibu kikatiba/kisheria, wa kuelimisha
watu juu ya maovu ya kijamii na athari zake hasi kwa jamii nzima na kila
mwana-jamii (social evils and their negative impact on the whole society and
each of its members) na kuhimiza maadili mema kwa viongozi, wafanyabiashara,
na raia wote.
3.3.3 Tume Huru ya Maadili na Udhibiti wa Ufisadi
CPT inapendekeza kuwa
kuwe na chombo kipya kitakachoitwa Tume Huru ya Maadili na Udhibiti wa Ufisadi
(Ethics and Anti-Corruption Commission) ambayo:
3.3.3.1 itapewa uwezo
wa kudhibiti na kupambana na rushwa na pia kudhibiti ukiukwaji hasa wa maadili
ya uongozi (ikiunganisha shughuli za TAKUKURU na za Tume ya Maadili ya Viongozi
ya sasa).
3.3.3.2 Hii itaondoa
haja ya kuwa na Tume mbili zenye uwezo na tija ndogo na kuwa na Tume moja yenye
sifa hizi mbili. Pia iwe na uwezo wa kuyashughulikia mambo yote ya ufisadi na
rushwa nchini yenye athari kwa sekta za umma, binafsi na asasi za
kijamii.
3.3.3.3 Tume
hii ikishafanya uchunguzi kuhusu rushwa na/au ufisadi na kujiridhisha kuwa kuna
kesi ya kupeleka mahakamani, ikabidhi jalada (faili) kwa Mwendesha Kesi za Jinai
Mkuu (DPP) kwa ajili ya kuendesha mashtaka mahakamani. Pale ambapo DPP atakuwa
na maoni kwamba hakuna ushahidi wa kutosha kwa ajili ya kesi ya jinai, ama
ashauri uchunguzi zaidi ufanywe kuhusu maeneo/masuala atakayoelekeza wazi wazi
kwa Tume au arejeshe jalada kwenye Tume kwa ajili ya hatua za kinidhamu
kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria husika isiyo ya jinai dhidi ya
mtuhumiwa.
3.3.3.4 Kwa
vyovyote vile, DPP awajibike kutoa sababu za maamuzi yake kuhusu mapendekezo
kwake ya Tume Huru hii kwa uwazi.
3.3.3.5 Aidha,
Katiba na sheria ziainishe misingi mihimili ya maadili hasa ya uongozi na hatua
zitakazochukuliwa kwa wakiukaji.
3.3.4 Udhibiti na uwazi katika mapato na matumizi ya mali ya taifa
CPT inapendekeza kuwa
kwa mujibu wa Katiba na sheria mpya husika:
3.3.4.1 ielekezwe kuwepo uwazi katika mapato na matumizi ya
mali ya taifa;
3.3.4.2 aidha izuiliwe/iwe marufuku kwa mtu au mamlaka yoyote
kuwa na madaraka au uwezo juu ya mapato na matumizi ya mali ya taifa bila
kuzingatia vigezo na/au masharti yaliyobainishwa na yenye kuwajibisha
kisheria.
3.4 Mgawanyo wa Mali na Rasilimali za Nchi
3.4.1 Kuna Upendeleo katika Mgawanyo wa Mali na Rasilimali za Nchi
Mwelekeo wa kugawia
kiupendeleo sehemu moja dhidi ya nyingine, au kundi moja dhidi ya jingine
imekuwa ndio kichocheo cha wabunge kutaka ama kutakiwa na wapiga kura wao
kuingia/kuteuliwa nafasi ya uwaziri. Licha ya mali na rasilimali za nchi, mambo
ni vivyo hivyo kwa misaada na mikopo toka nje. Maoni yetu kwa ajili ya zoezi la
Katiba yako katika sehemu mbili kama ifuatavyo:
3.4.1.1 Maliasili
(a) Kila
mara inapopasa, Serikali itathmini na kuhakiki maliasili husika ili ipate kujua
kwa uhakika na kwa misingi ya kisayansi kiasi na thamani yake kabla ya kuingia
katika mkataba na mwekezaji/wawekezaji. Hii ifanyike hata kama mkataba ni wa
aina ya ubia; makubaliano, kati ya mambo mengine, yazingatie, kwa misingi ya
haki navigezo vinavyokubalika, uwiano wa thamani hiyo na thamani ya uwekezaji
halisi utakaofanywa na mwekezaji/wawekezaji.
(b) Aidha, njia za kuwawezesha wananchi na taifa kufaidika
zizingatiwe – kuwekeza mahalia katika viwanda (Industrial Capital investments
in mining areas) km. kwa kutumia madini kutengeneza vidani/vito vya thamani
(Jewelry Industry); kuandaa wataalam ambao wataweza kupata ajira nje
baadaye; kuwezesha watu wa ndani kutumia fursa za uwekezaji na, hivyo, kuinua
hali yao ya kipato na kujiletea maendeleo; kushiriki katika faida ya wakati huo
– mkataba kunufaisha nchi na watu wake badala ya kufanya karibu kila kitu kwenda
kwa mwekezaji na wataalamu kutoka nje;
(c) Kushiriki umiliki
kwa njia ya ubia, inatupa nguvu ya kuhakikisha tunafaidika na pia utunzaji
mazingira unazingatiwa, tutashiriki kuweka masharti ya utumiaji na uuzaji wakati
uvunaji wa rasilimali unaendelea;
(d) Mikataba isifanyike
kwa siri bali kwa njia zinazokidhi kanuni na maadili ya uwazi katika masuala ya
mikataba ya kitaifa inayogusa maslahi ya taifa kiuchumi, kisiasa na
kiutamaduni (tukiondoa masuala nyeti ya ulinzi na usalama wa Taifa ambayo uwazi
wake sharti uwe ndani ya vyombo/wizara na idara husika za Dola); Mikataba
itakiwe kisheria kuwa na vifungu vinavyotoa fursa au upendeleo wa makusudi kwa
wananchi kutoa huduma za kawaida zinazoweza kupatikana nchini kwa matumizi ya
viwanda au shughuli za uwekezaji.
(e) Hivyo, wananchi wawe
na fursa kubwa ya kushiriki katika kutoa huduma zinazohitajika (service
industry) - ugavi na usambazaji wake - kwenye sehemu
husika.
(f) Haya yakizingatiwa, nchi na wananchi wake watafaidika
kwa wakati huo na kwa vizazi vijavyo. Tuwe na msimamo, kikatiba na kisheria,
kuwa kamwe tusiendelee kuvuna rasilimali bila kuhakikisha tunafaidika. Ni bora
kuwa na subira, kujipa nafasi ya kujiandaa kuliko kuwaachia nafasi wawekezaji wa
kigeni kuvuna faida yote kwa sababu ya kutokuwepo uwezo wa kutosha wa ndani wa
kuibakisha sehemu nono ya faida hiyo (a substantial share of the profit)
nchini.
(g) Hivyo, kuweko na Tume Huru ya Ardhi, Maliasili na
Mazingira (Land, Natural Resources and Environmental Commission)
kama chombo cha kikatiba/kisheria cha kutekeleza sera za kizalendo zinazoweza
kulifanya taifa na wananchi wake wanufaike na uwekezaji na uvunaji wa rasilmali
ya nchi yao bila kuathiri vibaya mazingira na
tabia-nchi.
3.4.1.2 Pato la
Taifa
(a) Mgawanyo wa pato la taifa (national revenue)
uwe ni wa kiuwiano kwa kuzingatia idadi ya watu na ukubwa wa eneo, maeneo na
makundi ya wasio na uwezo (vulnerable groups) yakipewa
kipaumbele.
(b) Katika kupanga Bajeti, kila sehemu – Mikoa wapate
kiwango sawa; na Mikoa iliyo nyuma ipate viwango vya ziada kutoka mfuko maalum
(equalization fund) kwa lengo hilo.
(c) Fungu la matumizi ya Serikali Kuu liwekwe bayana na
matumizi yasiwe ya kifujaji.
(d) Tume maalumu, Tume ya Mgawanyo wa Pato la Taifa na
Udhibiti wa Bajeti (Public Revenue Allocation and Budget Control
Commission) iundwe kwa ajili ya kazi ya kuweka misingi na vigezo vya
Mgawanyo wa pato la taifa na Udhibiti wa Bajeti; kusimamia/kuratibu utekelezaji,
uimarishaji, na tathmini yake kiendelevu kwakubainisha vema masuala ya Mgawanyo
wa pato la Taifa na ya Udhibiti wa Bajeti; ilmradi masuala hayo yasiingiliane
kwa kuasiana kisheria na kiutendaji.
3.5 Rushwa na Ufisadi
3.5.1 Penye
rushwa hakuna haki; kwani haki hugeuka na kuwa bidhaa. Wanaoweza kupindisha
sheria ili kujipatia haki yao ni wale wenye fedha na wenye nafasi za madaraka na
mamlaka. Tatizo hili limo nchini mwetu na ni la kijamii na mfumo mzima
unatawaliwa na uovu huu. Tiba yake ni nini? Tiba itaweza kupatikana hasa kwa
njia za kijamii na kisheria: Elimu na sheria inayotoa kipaumbele kwa umuhimu wa
maadili mema katika nyanja zote za kitaifa na kijamii (uchumi, siasa,
sheria/haki na utamaduni – dini, elimu, michezo, familia/ndoa na
malezi).
3.6 Uwajibikaji na Uwajibishwaji
3.6.1 Umuhimu wa mfumo unaotuwezesha kuwajibishana
Hili ni suala pana; kwa
hiyo, tunahitaji kujenga mfumo unaotuwezesha kuwajibishanakuanzia Rais na
Serikali/Utawala kwa ujumla, Bunge, Mahakama hadi raia. Mathalan,Bunge
liwajibike kwa wananchi, na wenye kushika nafasi za kuteuliwa wawe wanawajibika
kwa wananchi moja kwa moja au kwa njia ya vyombo wakilishi-shirikishi ambamo wao
ni watumishi, badala ya kuwajibika kwa yule aliyewateua
tu.
3.6.2 Rais na Dola Kikatiba na Kisheria
3.6.2.1 Ihakikishwe kuwa anayeteuliwa kugombea nafasi ya
Urais anakidhi vigezo msingi kimaadili na kiuongozi na kwamba umri wake usiwe
chini ya miaka 40 na usizidi miaka 65.
3.6.2.2 Rais
awe anawajibika kwa wananchi kupitia Bunge. Bunge lipewe uwezo wa kumwondoa
madarakani kwa vigezo na njia vinavyozingatia kwa dhati maslahi ya kitaifa ya
kutoyumbisha nchi bila kupuuzwa kwa athari za utovu wa nidhamu, uwajibikaji na
maadili mema ya uongozi wa Taifa.
3.6.2.3 Asiwe
na mamlaka ya kuteua wale wanaopaswa kumwajibisha – hasa viongozi wa Mahakama na
wa Bunge.
3.6.2.4 Uteuzi
wake wa viongozi uzingatie sifa na vigezo stahiki – hasa uzoefu, utaalam,
weledi, uadilifu, uzalendo na ridhaa ya Bunge. Unasaba na uswahiba viepukwe
kabisa.
3.6.2.5 Anapotakiwa kusaini sheria iliyopitishwa na Bunge,
apewe ukomo wa muda,km. siku kumi, bila kuhesabu siku zisizo za
kazi.
3.6.2.6 Kuna
haja ya kuwa na serikali ndogo lakini yenye ufanisi au tija. Wizara naMawaziri
wawe si chini ya 15 na wasizidi 20. Idara za wizara na Tume Huru zitashiriki
kuleta ufanisi wa Serikali.
3.6.2.7 Wabunge wasiwe mawaziri. Mawaziri wateuliwe na Rais
kwa kuzingatia sifa na vigezo stahiki tajwa katika 3.6.2.4 hapo juu. Na Rais
apendekeze na wajadiliwe na kuidhinishwa na Bunge kabla ya kuteuliwa rasmi.
Aidha, kusiwe na manaibu mawaziri.
3.6.2.8 Kwa
kuwa mawaziri watakuwa wataalamu na wenye uwezo wa kusimamia mipango na
utekelezaji wa programu za wizara, nafasi ya waziri itaunganisha kazi za
mawaziri wa sasa na makatibu wakuu.
3.6.2.9 Bunge
lipewe uwezo wa kumwondoa waziri asiyefaa kwa misingi au vigezo mwafaka vya
kisheria na kwa njia ya kura ya Wabunge ya kutokuwa na imani nayeambayo Rais
alazimike kuikubali.
3.6.3 Bunge Kikatiba na Kisheria
3.6.3.1
Wabunge wawajibike
kwa wananchi ambao wapewe uwezo wa kumwondoa madarakani Mbunge katika jimbo lake
la uchaguzi kabla ya ukomo wa muda wa kipindi chake cha kuwa mbunge ikiwa
hawajibiki. Kwa ajili ya kupokea taarifa za mara kwa mara kutoka kwa mbunge wao
na, panapopasa, kumwajibisha:–
(a) liweko baraza/jukwaa (forum) katika kila jimbo
la uchaguzi litakalokutana angalau mara nne kila mwaka na kuwasilisha
mapendekezo/maazimio na maamuzi yake kwa Spika wa Bunge
(b) Katiba Mpya impe Spika madaraka ya kuchunguza
mapendekezo au maazimio ya kuwajibisha mbunge kama inavyoelezwa kwenye kifungu
3.6.3.2 hapa chini.
(c) Utawala wa kila
Mkoa, ngazi ya wilaya, uwajibike juu ya maandalizi, uratibu na kumbukumbu za
baraza/jukwaa hili.
3.6.3.2
Wabunge wote wawe wa kuchaguliwa ili
wawajibike kwa wapiga kura wao na wawajibishwe nao. Katiba iweke vigezo vya
mbunge kusimamishwa au kutakiwa kuonyesha kwa nini asiondolewe katika wadhifa
wake wa kuwa Mbunge kwa kushindwa kukidhi matakwa ya vigezo hivyo. Km. Ukiukwaji
wa maadili ya uongozi; kitendo/vitendo vya rushwa/ufisadi vilivyodhihirishwa kwa
mujibu wa sheria; kosa/makosa mengineyo ya jinai; kufirisika; kutohudhuria vikao
vya Bunge bila sababu mwafaka mara tatu mfululizo; kutofuatilia kwa makini na
uweledi masuala muhimu ya jimbo lake; au uzembe uliokithiri katika kutimiza
wajibu wake wa Ubunge.
3.6.3.3 Spika
asiwe mbunge wala asiwe na cheo katika
chama cha siasa.
(a) Mfumo wa sasa unaonyesha udhaifu katika eneo hili kwa
kuwa Spika amekuwa akichaguliwa kutokana na chama tawala na waliopendekezwa au
waliojitokeza kugombea wametegemea hali yao ya kuwa wanachama wakereketwa wa
vyama vyao. Katika kuongoza shughuli za Bunge, kumekuwa na mwelekeo wa Spika
kushinikizwa na/ au kupendelea/kulinda chama chake. Hali hii haijengi mazingira
adili ya demokrasia ya vyama vingi katika Bunge, chombo kiteule cha uwakilishi
na kutunga sheria za nchi.
(b) Hivyo, ni jambo la msingi na adili kwamba Spika awe
mtu huru mwenye hekima na busara na ambaye si kiongozi katika chama chochote cha
siasa chenye uwakilishi Bungeni wala mbunge.
3.6.3.4 Viti
maalum viwe kwa:–
(a) wanawake watatu (3) kila Mkoa na kijana mmoja (1) tu
kila Mkoa ambao watapendekezwa na vyama kwa kila chama kupendekeza wawili wawili
na hao watachaguliwa kwa kura mkoani mwao na wananchi wakati wa Uchaguzi
mkuu;
(b) makundi ya wenye ulemavu yapate mwakilishi mmoja (1)
ambaye atapatikana kwa njia ya ushindani wa kupigiwa kura na makundi husika
wakati wa Uchaguzi Mkuu kutokana na mapendekezo ya mgombea mwenye ulemavu mmoja
mmoja kwa kila kundi.
3.6.3.5 Muundo
wa uwakilishi uwe wa kiuwiano nchi
nzima kwa kuzingatia idadi ya watu na ukubwa wa eneo kama itakavyobainishwa
kisheria, kutekelezwa na kuratibiwa kitaalamu. Suala la Muungano lisisababishe
kukiukwa kwa kanuni au msingi huu wa uwakilishi katika Bunge la Muungano au
chombo chochote cha Muungano chenye uwakilishi. Hii itaifanya hoja ya kwamba
Tanganyika/Tanzania Bara imemezwa na Muungano au kuwa Zanzibar imemezwa na
Tanganyika/Tanzania Bara ikose msingi halali kwani kila sehemu itapata stahili
zake kwa vigezo mwafaka vyenye kuzingatia kanuni za kisayansi na
haki.
Inaendelea.....
Post a Comment