Na Anna Nkinda – Maelezo,
Kagera
…………………………………………
Serikali
Mkoani Kagera imevikopesha vikundi mbalimbali vya maendeleo vya vijana kupitia
Vyama Vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) zaidi ya shilingi milioni 83 katika
kipindi cha miaka mitano iliyopita ilikuwawezesha vijana waweze
kujiajiri wenyewe na kujikwamua kiuchumi .
Hayo yamesemwa leo na Mkuu
wa Mkoa huo Kanali Mstaafu Fabian Massawe wakati akisoma taarifa fupi ya mkoa
kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara
aliyepo mkoani humo kwa ajili ya kuangalia jinsi fedha za mkopo kutoka mfuko wa
vijana zilivyoweza kuwasaidia vijana kujikwamua kimaisha.
Kanali Mstaafu Massawe
alisema kuwa Serikali inasimamia utekelezaji wa sera ya maendeleo ya vijana kwa
kuratibu shughuli za mifuko ya vijana na kufuatilia utoaji na urejeshaji wa
mikopo, kuhamasisha vijana na kufufua moyo wa kujitolea na kukuza na kuendeleza
vipaji mbalimbali walivyonavyo vijana ili kuwawezesha kujiajiri kupitia mafunzo
yanayohusu stadi za kazi na maisha
“Changamoto tunazokabiliana
nazo katika kuwakopesha vijana ni mahitaji makubwa ya mkopo ukilinganisha na
uwezo wa SACCOS au wakopeshaji wengine, urejeshaji hafifu wa mikopo kutoka kwa
wakopaji, ukosefu wa ajira, uvivu na uzurulaji, vijana kutaka mafanikio kwa
haraka na matumizi ya madawa ya kulevya kwa baadhi ya vijana”, alisema Mkuu wa
Mkoa huyo.
Aliendelea kusema kuwa ili
kukabiliana na changamoto hizo Serikali ngazi ya mkoa inafuatilia kwa karibu ili
kuona kwamba matamko ya sera ya Taifa ya Maendeleo ya vijana yanazingatiwa na
kuingizwa katika maendeleo ya Halmashauri lengo kuu ni mkoa kuwa na vijana
wenye ari ya kuwajibika na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii,
wazalendo, wenye maadili na kupenda nchi yao.
Kwa upande wake waziri Dk.
Mukangara alisema kuwa hivi sasa Serikali inaangalia uwezekano wa kuongea mkopo
kwa SACCOS zinazolenga shughuli za maendeleo ya vijana kutoka shilingi milioni
tano hadi kumi kwani mahitaji ni makubwa na hayakidhi
haja.
Mkoa wa Kagera unakadiriwa
kuwa na idadi ya watu 2,739,492 kati ya hao wanawake 1,386,669 na wanaume
1,353,123 ambapo vijana ni 903,608 wenye umri wa miaka 15 hadi 35 sawa na
asilimia 33 ya wakazi wote ambapo kati ya hao wa kike ni 459,867 na wa kiume
443,741.
Post a Comment