Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imepongeza wazo la
kuanzishwa mbio za Uhuru Marathon ambazo zitakuwa zikifanyika kila mwaka, lengo
likiwa ni kudumisha umoja, amani na upendo miongoni mwa Watanzania na kuuenzi
uhuru wetu.
Pongezi hizo zilitolewa na
Waziri wa habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara wakati wa
uzinduzi wa mbio hizo katika hafla iliyofanyika kwenye hoteli ya JB Belmont
jijini Dar es Salaam juzi usiku.
Dk. Mukangara alisema kuwa,
kwa sasa kuna mbio nyingi za marathon hapa nchini, lakini hakuna ambaye alikuja
na wazo zuri la kuanzisha mbio kama hizo za kuuenzi uhuru wetu na kudumisha
amani nchini.
“Nawapongeza waandaaji wa
mbio hizi ambao ni vijana wa Kitanzania waliokuja na wazo hili zuri la kuanzisha
mbio za uhuru. Tunazo mbio nyingi sana hapa nyumbani, lakini hatukuwa tumewaza
kuanzisha mbio zinazolenga kuuenzi uhuru wetu na kudumisha amani
yetu.
“… Kwa niaba ya Serikali,
napenda kusema wazi kuwa tumefurahishwa sana na wazo hili la kuanzisha mbio hizi
za uhuru na nichukue fursa hii kuwaomba wadau na wapenda maendeleo ya michezo
kuungana na taasisi hii kufanikisha mpango huu ili uweze kuwa na
mafanikio.
“Serikali bado itaendelea
kuweka miongozo na mazingira rafiki ya kushirikiana na wadau wenye nia nzuri ya
kuendeleza michezo nchini. Nina hakika waheshimiwa mawaziri, wabunge, viongozi
mbalimbali wa Serikali, mashirika binafsi na viongozi wa dini wote watajitokeza
kushiriki mbio hizi,” alisema.
Awali Mkurugenzi wa Kampuni
ya Intellectuals Communications, Innocent Melleck, walio waandaaji wa mbio hizo,
alimuomba waziri afikishe ombi lao kwa Rais Jakaya Kikwete kuwa mlezi wa mbio
hizo.
Pia walimkabidhi Dk.
Mukangara fulana maalumu ya Rais Kikwete pamoja na ya Spika wa Bunge la
Tanzania, Anne Makinda, kutokana na mchango wao maalumu kwa mbio
hizo.
“Mbali na hilo tunapenda kuweka milango wazi
kwa taasisi, kampuni na watu mbalimbali kudhamini mbio hizo zenye malengo mazuri
kwa Taifa,” alisema.
Mbio hizo zinatarajiwa kuanza
rasmi mwakani na zitakuwa zikifanyika kila Desemba 8, kwa ushirikiano mkubwa wa
Berlin Marathon na London Marathon.
Post a Comment